JK ukipuuza katiba, utajipuuza


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 01 February 2012

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

BAADA ya Rais Jakaya Kikwete kukutana na vyama vya upinzani ikulu jijini Dar es Salaam ili kushauriana nao juu ya mchakato wa katiba mpya, kuna mambo mawili makubwa yamejitokeza yanayoweza kumpotosha rais na kumwingiza katika mgogoro.

Kwanza, wapo washauri wake pamoja na Wanikulu kadhaa wanaoeneza fitina kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilijifanya kumsusa rais, lakini sasa kimenywea na kuanza kumbembeleza ili awasamehe na kujadiliana nao.

Kundi hili wamo hata baadhi ya mawaziri waandamizi, hasa wale wanaofanya kazi ikulu na wale wanaofanya kazi ofisi ya waziri mkuu.

Pili, liko kundi la wabunge wanaopoteza muda mwingi kumsengenya rais kuwa ni mwoga na anawaendekeza CHADEMA na kwamba watakwamisha mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya uundwaji katiba mpya. Hawa wanadai rais amewadharau wabunge wa chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – hatua yake ya kukubali kuongea na upinzani baada ya kususia muswada kumewadhalilisha hata wao.

Makundi yote mawili, yanajaribu kumshawishi rais kuwa awapuuze CHADEMA na aendelee mbele na ratiba yake ya kuhakikisha anaipatia nchi katiba mpya ifikapo mwaka 2014.

Hapahitajiki ujuzi wa ajabu kugundua uzembe mkubwa wa kufikiri uliojikita katika hoja za makundi haya mawili. Ni makundi ya kawaida katika utawala wowote, ambayo huishi kwa kutegemea fitina. Kwa kundi la kwanza, sababu ya kueneza fitina inaeleweka wazi.

Hili ni kundi la washauri na wanikulu ambalo kwa muda mrefu limelaumiwa sana na wananchi kwa kushindwa kumshauri rais na kuiyumbisha serikali. Ni kundi ambalo lina mkono katika kila tuhuma ya ufisadi uliotanda ndani ya serikali na chama tawala.

Ni hawa wanaotuhumiwa kushindwa kabisa kumsaidia rais na kuishia kufanya biashara chafu ndani na nje ya nchi, huku wakimdanganya na kumchonganisha na watu ambao wangeweza kumsaidia rais na taifa. Baadhi yao wanatuhumiwa kumgombanisha rais na viongozi wastaafu.

Kwa kuwa muda wao mwingi umekuwa katika biashara na miradi binafsi iliyosambaa nchi nzima, wanaona wivu rais akipata ushauri wa maana kutoka kwa watu wengine. Baadhi ya washauri hawa, wamefikia hata hatua ya kuwatoza fedha au kuwaomba fadhila watu wema wanaotaka kumwona kiongozi wa nchi ili kumpa ushauri unaojenga taifa.

Kundi la pili ni la wabunge wasiofurahishwa na mkutano wa rais na CHADEMA. Wengi wa wabunge hawa ni wale ambao wameshindwa kuishauri na kuisimamia serikali na kuishia kuipongeza na kuipigia makofi kila wakati. Ni hawa hawa waliokuwa wanazomea wakati CHADEMA inapinga muswada wa uundwaji wa katiba mpya.

Wabunge hawa ndio pia wanaotumika kukuza mipasuko ndani ya CCM huku wakizurura kila kambi kujipatia maslahi binafsi. Kwao hawa, urais wa mwaka 2015 ndiyo agenda kuu na mambo ya muhimu kama katiba mpya, uchumi, muungano na mfumuko wa bei hayana uzito wa kutosha kumfanya rais akutane na wapinzani.

Ni wabunge hawa hawa ambao hata rais amekuwa anawashangaa wanaposimama kuzungumza bungeni. Kitendo cha rais Kikwete kukaa na wapinzani na kuwasikiliza kuhusu udhaifu wa sheria iliyopitishwa kwa mbwembwe na wabunge wa CCM, sasa ni wazi kuwa rais ametuma ujumbe mzito kwao na onyo kuwa waache wanaojipendekeza na kumpotosha.

Wengi wa wabunge hawa wameingia bungeni kwa umaarufu wa Kikwete binafsi. Wengine wameingizwa na baadhi ya marafiki zake. Baada ya kuingia katika ubunge, wamejikuta hawana kazi nyingine ila kumsifia rais na kumsengenya hapo hapo.

Wengine walizoea kumdanganya kuwa hali ni nzuri na kwamba serikali yake inakubalika. Sasa wameona rais amekubali kukutana na wapinzani na kugundua ukweli na hivyo vibarua vyao vinaelekea mwisho.

Mchakato wa katiba mpya ni suala tete na wakati huo huo ni suala mtambuka. Washauri wa rais na wabunge wa CCM wanaojaribu kulifanya kuwa la kiitikadi wanafanya makosa makubwa sana.

Katiba inagusa maslahi ya wengi; ni hatari kwa mtu aitwaye mbunge kutanguliza maslahi ya chama chake katika jambo hili.

Rais Kikwete anapaswa kuona hili: Ikiwa bunge la sasa lenye zaidi ya asilimia 75 ya wabunge wanatoka CCM linapitisha muswada ambao unalazimika kurudi bungeni ndani ya miezi mitatu, ni wazi kuwa kuna kitu kisichoenda sawa. Hivyo basi, sasa anapaswa kutumia hekima aliyoitumia kukutana na wapinzani na kushangaa kila hoja wanayomweleza kuhusu udhaifu wa sheria yake, sharti aangalie uwezo wa mwanasheria sheria wake mkuu, waziri wa sheria na katiba, lakini zaidi sana, wabunge wa chama chake waliopigia talumbeta muswada huu.

Watanzania hawatamani kuombwa radhi na wabunge wa CCM. Wanachohitaji ni kuona tangu sasa, Rais Kikwete anapata ujasiri wa kupambana na wale waote wanaompotosha na kuhakikisha mambo yanayohusu mustakabali wa kitaifa hayaingizwi katika misigano ya kiitikadi.

Vinginevyo rais akikosa ujasiri wa kutosha; akaamua kuacha kumbukumbu ya maamuzi ya kizalendo kwa kukubali kuyumbishwa na wasaidizi wake, atakuwa amejipuuza yeye mwenyewe

tutikondo@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: