John Mrema: Vunjo watanipa ubunge


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 02 June 2010

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
John Mrema

MIONGONI mwa wanasiasa vijana wanaotarajiwa kutikisa kampeni za uchaguzi mkuu huu, ni John Mrema anayewania ubunge katika jimbo la Vunjo, mkoani Kilimanjaro.

Mrema amejitosa katika kinyang’anyiro cha ubunge kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI wiki hii, Mrema pamoja na mambo mengine, anasema amejitosa katika kinyang’anyiro hicho ili kuwatumikia wananchi wa Vunjo ambao anasema kwa kipindi cha miaka 10 wamekosa mwakilishi imara bungeni.

Mrema anasema wananchi wa Vunjo wana matatizo mengi, ikiwamo uhaba wa maji katika mji wa Himo. Kuna tatizo la upungufu wa walimu wa kufundisha katika baadhi ya shule, lakini kubwa ni kushamiri kwa ubadhilifu wa fedha za umma ndani ya halmashauri.

Anasema, “Nataka kuingia bungeni kukabiliana na matatizo haya. Kwamba Vunjo kuna vyuo vitatu vya walimu – Marangu, Mandaka na chuo kikuu Tumaini – lakini hakuna walimu wa kutosha wa kufundisha vijana wetu.”

Anasema, “Nataka kusaidia vijana kupata elimu ili waweze kujikwamua kimaisha. Hicho ndiyo kipaumbele changu cha kwanza iwapo nitakuwa mbunge.”

Kuhusu ubadhilifu wa fedha, Mrema anasema, taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa ndani ya Halmashauri ya wilaya ya Moshi Vijijini iliyoko jimbo la Vunjo, kuna udanganyifu wa fedha zikiwamo zile zinanazotolewa na wahisani.

Mfano hai ni fedha zilizotolewa na serikali ya Ujerumani kufadhili mradi wa maji wa Kirua – Kahe. Ujerumani ilitoa Sh. 15.3 milioni kwa kazi ya uchimbaji mitaro na kutandaza mabomba.

Hata hivyo, Mrema anasema ripoti ya fedha iliyowasilishwa kwa wahisani, inaonyesha kuwa wananchi walilipwa ujira kufanya kazi hiyo.

“Lakini ukweli ni kwamba wananchi walilazimishwa kuchimba mitaro na wale walioshindwa kufanya hivyo, walinyanganywa mali zao na kuuzwa kwenye mnada,” anasema Mrema kwa sauti ya masikitiko.

Mfano mwingine ni ujenzi wa nyumba ya mwalimu katika shule ya sekondari Kisangesangeni, Kata ya Kahe. Katika mradi huo, wafadhili walitoa Sh. 7 milioni.

Anasema fedha hizo pamoja na zile Sh. 15.3 milioni zilizochangwa na wananchi, hazikutumika kama ilivyopangwa.

Anasema, “Nataka kwenda bungeni kukomesha unyama kama huu. Fedha zinatolewa, lakini hazitumiki kwa kazi iliyokusudiwa. Ubadhirifu ni mkubwa hata kwa mradi wa umwagiliaji wa Kahe.

Anasema, “Kati ya Sh. 150 milioni zilizotolewa, tayari zimeshatumika Sh. 118 milioni kujenga banio ambalo hadi sasa halijakamilika, huku viongozi wakilinda watuhumiwa.”

Mrema anajivunia historia yake ya kupigania haki za wanyonge tangu akiwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambako alikuwa waziri mkuu wa serikali ya wanafunzi.

Kati ya mwaka 2003 na 2004 alichaguliwa kuwa katibu mkuu wa chama cha haki za binadamu (University of Dar es Salaam Human Rights Association).

Wengine waliokwishajitokeza kugombea ubunge jimbo la Vunjo, ni pamoja na Aloyce Kimaro ambaye ni mbunge wa sasa (CCM) na Augustine Lyatonga Mrema, mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP).

Alipoulizwa kwanini asijitoe na kumwachia jimbo hilo Augustine Lyatonga Mrema ili kuondoa uwezekano wa Vunjo kuangukia tena katika mikono ya CCM, Mrema alisema, “Huu ni uamuzi wangu sahihi.”

Amesema, “Huwezi kumuachia jimbo Lyatonga (Augustine Mrema). Huyu hana tofauti na CCM. Wakati Rais Jakaya Kikwete anakataa kura za wananchi kwa kauli za dharau dhidi ya wafanyakazi, Mrema anahaha kumtafutia kura Kikwete.”

Anasema, “Wananchi wa Vunjo wanaangalia mbele na huko wameona kuwa mtu wa kuwawakilisha si mwingine bali ni mimi, John Mrema kutoka Chadema,” anasema kwa kujiamini.

Katika miezi michache iliyopita, wanachama wengi wa TLP wamehama chama chao na kujiunga na vyama vingine wakidai kuwa Augustine Lyatonga Mrema, mwenyekiti wao, anafanya kazi ya CCM kwa kuisifia na kuitetea.

Mgawanyo wa kura kwa wagombea wa upinzani, ndiyo uliyonufaisha mgombea wa CCM, Aloyce Kimaro mwaka 2005. Katika uchaguzi huo, kura za Kimaro zilikuwa chache ukilinganisha na zile za wagombea wa vyama vya TLP, Chadema na NCCR- Mageuzi kwa pamoja.

Hata hivyo, Mrema anasema uchaguzi wa mwaka 2005 ni tofauti na sasa na kwamba “mwaka huu wananchi wameshaamua kuweka kura zao kwenye kapu moja.”

Ndani ya Chadema, Mrema ni Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri, akiwa na jukumu la kuratibu shughuli zinazofanywa na wabunge wa Chadema bungeni na kufanya utafiti wa masuala mbalimbali yanayotokea ndani na nje ya nchi.

Akizungumzia tuhumza za ukabila zinazohusishwa na chama chake, kutokana na hasa kinachoitwa na wapinzani wao kuegemea zaidi mikoa ya kaskazini mwa nchi, Mrema anasema, “hizo ni propaganda tu.”

Anasema, “Mimi sikuteuliwa kwa misingi ya ukabila. Ni baada ya Kamati Kuu (CC) ya chama changu kuona kuwa nina uwezo wa kufanya kazi.”

Anasema, “Nimesimamia kurugenzi hii tangu ianzishwe mwaka 2007 na hakuna ambaye hajui kazi ambayo wabunge wetu wameifanya bungeni.”

“Hao wanaoendeleza ujinga huo wana malengo yao ya kisiasa, bali wanapaswa kujua jambo moja kuwa nasi wachagga tuna haki katika nchi hii na wasitake kuaminisha umma kuwa ukizaliwa mchaga basi huna haki ya kuwa kiongozi,” amesema.

Alipoulizwa nani atakuwa mgombea urais Chadema wakati viongozi wa ngazi ya juu wa chama chake – Dk. Willibrod Slaa na Freeman Mbowe wakiwa tayari wametangaza hawataki nafasi hiyo, Mrema alijibu:
“Nadhani ni sualala muda tu, ndilo linalogomba. Tutasimamisha mgombea urais mwenye uwezo na anayekubalika kwa wananchi,” anasema bila kutaja jina la mgombea huyo.

John Edward Mrema alizaliwa tarehe 7 Oktoba 1979 akiwa mtoto wa tatu katika familia ya watoto wanane wa Edward Mrema na Radegunda Shirima.

Alipata elimu yake ya msingi mwaka 1988 katika shule ya Msingi Mawanjeni, Kata ya Mwika Kusini, wilayani Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro.

Alijiunga na shule ya Sekondari ya Vunjo kwa masomo ya kidato cha kwanza hadi cha nne mwaka 1995 hadi 1998. Mwaka 1999 hadi 2001 alikuwa Agape Seminari kwa masomo ya kidato cha tano na sita.

Mwaka 2002 hadi 2006 alikuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambako alichukua shahada ya kwanza ya elimu ya siasa na utawala.

Ni Mrema huyuhuyu ambaye anakumbukwa na wanafunzi aliosoma nao chuo kikuu, kwa uwezo wake wa utetezi, hasa suala la mikopo kwa wanafunzi.

Akishirikiana na Profesa Seith Chachage (sasa marehemu), Mrema alipigania hata haki za wafanyakazi wengine UDSM, wakiwamo wahadhiri.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: