Jua lawachwea Salma, Ridhiwani


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 06 October 2010

Printer-friendly version
Wazo Mbadala
Mama Salma Kikwete

KUNA wakati Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) huzusha tafrani kubwa kwenye Idara ya Zimamoto na hospitali mbalimbali inapofanya zoezi la uokozi.

Mamlaka hiyo huwasha moto feki na kisha hupiga simu Idara ya Zimamoto na makampuni mengine yenye huduma hiyo kuwajulisha kwamba ndege imeanguka na inawaka moto.

Vilevile TAA hupiga simu Hospitali ya Taifa Muhimbili na hospitali nyingine za halmashauri kwamba zijiandae kupokea majeruhi kutokana na ajali hiyo mbaya kabisa kuwahi kutokea.

Hapo hutokea pilikapilika nyingi; Muhimbili hujiandaa vilivyo, hupanga wagonjwa, huandaa wodi, vitanda na kikosi cha uokozi huchukua gari la wagonjwa kwenda kwa kasi eneo wanaloambiwa kuna ajali.

Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), makampuni ya mafuta kama BP huwa yanafanya zoezi kama hilo ili kupima utayari wa wafanyakazi wa idara ya zimamoto, uokoaji pamoja na vifaa vyao.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete naye alijifunza kuwasha moto, kwa makusudi, ili kupima uwezo wa zimamoto wa CCM.

Loo, moto aliowasha Kikwete unaunguza vibanda vya CCM kwenye matawi na sasa anajutia, moto unaelekea kuunguza nyaraka za maombi yake ya urais Oktoba 31, 2010.

Kikwete, akizungumza kwa hisia kali alitoa tamko kuwa hataruhusu asilani mikataba mipya katika shughuli za uchimbaji madini nchini hadi iliyopo boreshwe kwa maslahi ya taifa.

Hee, siku chache baadaye akawasha moto kwa makusudi, akaruhusu mkataba wa uchimbaji madini ya dhahabu katika Mgodi wa Buzwagi.

Pamoja na nyaraka zote za serikali kuonyesha utata na mbaya zaidi mkataba huo kutiwa saini usiku nje ya nchi, wabunge kwa kujali maslahi ya CCM wakavaa koti la ujinga wakajitosa kuzima moto na wakaunga mkono hoja mbunge aliyeibua kashfa hiyo, Zitto Kabwe (CHADEMA- Kigoma Kaskazini) aadhibiwe.

Halafu mawaziri na manaibu waziri wakachotewa mamilioni ya shilingi kwenda mikoani kusiliba kwa uongo akili za wananchi kwamba hakuna kosa lililofanyika katika mkataba ule.

Wananchi, asasi za kiraia, asasi zisizo za kiserikali na wasomi walioko nje ya CCM walijitahidi kueleza kasoro katika mkataba ule, lakini wapi. Ule ndio ulikuwa mwanzo wa Kikwete kuchafua CV ya dhamiri yake.

Mei mwaka huu Kikwete aliwasha moto bila sababu za msingi. Alikataa kura za wafanyakazi wote na akatishia kuwatwanga endapo wangeandamana kudai mishahara na maslahi mazuri.

Kikwete aliwathamini wazee wa CCM waliomshangilia kwa nguvu bila kujua walikuwa wanatia petroli zaidi kwenye moto ambao asingeweza kuzima. Leo, anahaha nchi nzima kuomba kura zao kwa ahadi hewa kwamba ataongeza kufikia chini kidogo ya kile walichoomba.

Sijui alijiamini vipi maana Agosti aliwasha moto, kwa makusudi, kwenye vibanda vya CCM (majimbo) kwa kukata majina ya wagombea vipenzi, na kuwaweka wale ‘aliopendezwa’ nao kwa matarajio kuwa angetuma zimamoto.

Majimbo yote yanawaka moto wa uasi. Baadhi ya majimbo yameteketea yameangukia upinzani baada ya zimamoto Salma Kikwete, Ridhwani pamoja na wateule kushindwa. Wanaeleza uzuri upi ambao watu hawajui?

Kila waendako wanaambulia patupu. Jimbo la Tanzania analoomba kutetea nalo linaelekea kuangukia upinzani.

Mtendaji mkuu wa CCM, Yussuf Makamba ni kiongozi mwingine anayemsababishia Kikwete balaa majmboni.

Mwaka juzi, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ilivunja nyumba za wakazi eneo la Tabata Dampo jijini Dar es Salaam ili kumpisha mwekezaji. Mabuldoza yalifanya kazi hiyo usiku na mchana, wananchi wakabaki nje na bila chakula.

Makamba katika kuzima soo, akakimbia haraka dukani akanunua chakula cha kuku na kukipeleka kwa watu hao waliobomolewa nyumba zao. Kumbe zilikuwa pumba za kuku.

Vyombo vya habari vilipoandika kwamba Makamba amewapa watu chakula cha kuku aling’aka. Maskini alipofuatilia ikaonekana kweli, akaomba radhi.

Kwa serikali hii ya CCM, hakuna cha bahati mbaya, kila jambo linafanywa kwa makusudi—kwao wananchi ni kama kuku—ndiyo maana wanatoa maamuzi pumba, majibu pumba, kauli pumba, ahadi pumba.

Siku zinazidi kuyoyoma Salma, Ridhiwani hawajazima moto aliowasha Kikwete. Kiwewe.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: