Jussa anaimba kibao cha CCM


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 22 February 2012

Printer-friendly version

BAADHI ya watu katika jamii hupenda sana kujiweka karibu au kujinasibisha na mafanikio ya watu wengine; vijana hudai kujipa ‘ujiko’.

Utasikia, “wakati tunasoma mshambuliaji YY alikuwa hapiti kwangu, mimi nilikuwa beki matata bwana,” au utasikia, “tasnifu ya waziri XX niliitengeneza mimi.” Katika kundi hili wapo wanafiki, waongo na wambea kwa ajili ya kufurahisha baraza.

Halafu wapo wachonganishi na wazushi ambao, kwa kila jambo wanaloshindwa husingizia wengine ili waonewe huruma.

Utasikia, “Aah KK ndiye kanisababishia haya” au “Si unajua bosi wetu ni mwislamu (au mkristo) hivyo hataki wakristo (au waislamu).”

Katika kundi hili yumo Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) upande wa Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu.

Jussa ameingiza fitina za dini na ubaguzi ambao Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetumia tangu ulipoanza mfumo wa vyama vingi.

Amesema eti sababu zilizochangia CUF ishindwe katika uchaguzi mdogo wa Uzini ni uwepo wa wakristo wengi na watu wengi wa kutoka Tanzania Bara.

Jussa anasema kikwazo kwa CUF ni ukristo na ubara. Je, hicho ndicho kilichangia ilishindwa vibaya Tanzania Bara, isipokuwa majimbo mawili? Hivi ni kweli walioipa ushindi CCM ni wakristo kutoka bara? Je, ni kweli waislamu ni wale tu walioipigia CUF?

Kiongozi wa ngazi ya juu kama Jussa anapotoa kauli kama hiyo, huo huweza kuwa msimamo wa CUF; na kwa vile kauli yake haijakanushwa popote, bila shaka ametumwa awasilishe ujumbe huo. Ujumbe umefika.

Hivi karibuni, Jussa alituma ujumbe mwingine mkali wa CUF kuhusu Bara na Muungano pale Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka alipowasilisha kwenye Umoja wa Mataifa maombi ya kuongezewa mpaka baharini – km 241.5.

Jussa alimshambulia Prof. Tibaijuka, kama mtu binafsi akionyesha hofu kwamba ikiwa mpango wa Zanzibar kujiondoa kwenye Muungano huu wa sasa utafanikiwa, mipaka hiyo mipya itazua mgogoro kati yao na taifa jipya la Bara.

Kwa hiyo, Bara ni tishio kwa mustakbali wa Zanzibar na unapokuja kuonekana sasa ushawishi wa CHADEMA unaongezeka, wanaona wakristo na wabara ni tishio jingine kwa CUF baada ya CCM.

Jussa anajua siasa chafu za CCM. Katika uchaguzi wa mwaka 1995 CCM waliimba kwa nguvu kwamba vyama vingi vitasababisha vita kama Rwanda ambako takriban watu 800,000 walikufa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1994.

CCM ilikuwa inadai kirefu cha CUF ni Chuki, Udini na Fitina. Wakaimba udini kwa CUF na wakaimbisha watu waone ukabila katika NCCR-Mageuzi. CCM imetumia silaha hizo katika kila uchaguzi na kwa bahati mbaya CUF haikutoa utetezi mwafaka.

Hata katika uchaguzi uliopita CCM ilitumia kete hiyo; katika baadhi ya maeneo wamelaani udini (ukristo) na maeneo mengine udini (uislamu). CCM imechanganya watu wakachanganyikiwa.

Baada ya CUF kukubali ndoa na CCM kuunda Serikali ya Mapinduzi (SMZ) inayoendeshwa kwa mfumo wa Umoja wa Kitaifa, Jussa amejifunza kuimba wimbo wa udini na ubaguzi.

Anawaweka wapi wakristo wanachama wake? Anawapa ujumbe gani? Jussa anapouchukia ukristo na wakristo ana uhakika chama chake kinaweza kutwaa madaraka ya nchi bila watu wa dini zote? Uzini ina wakristo wengi kuliko waislamu au ndiyo mfa maji haachi kutapatapa?

0658 383 979
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: