Kabila amuangikia Kikwete


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 26 October 2011

Printer-friendly version
Rais Kabila na Rais Kikwete

BALOZI wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) ameshindwa kuthibitisha iwapo nchi yake imeomba majeshi kutoka Tanzania.

Katika mahojiano na MwanaHALISI, Balozi Alfany Mpango alisema juzi Jumatatu, jijini Dar es Salaam, “Habari hizo sijui mimi.”

Mpango ambaye anaongea Kiswahili katika lafudhi ya Kikongomani alimwambia mwandishi wa habari hizi, kwa sauti ya upole, kwamba yeye hajui lolote juu ya serikali yake kuomba msaada wa majeshi kutoka Tanzania.

Gazeti la lOeil du Patriote (Jicho la Mzalendo) ambalo hutolewa mjini Paris, Ufaransa, limedai kwamba katika kukabiliana na tishio la kung’olewa madarakani, Rais Joseph Kabila ameomba majeshi kutoka Tanzania na Korea Kaskazini ili kumlinda.

Kwa mujibu wa gazeti hilo la kila wiki, toleo la wiki ya pili ya mwezi huu, tayari askari wa Tanzania wameingia mjini Kinshasa kuimarisha ulinzi wa Rais Kabila na kwamba “wataingia uwanja wa mapambano pale mambo yatakapomwendea kombo.”

Lakini ofisa wa ngazi ya juu katika wizara ya mambo ya nje ameliambia gazeti hili jana kuwa hana taarifa kuhusu suala hilo.

Alipong’ang’aniwa alisema, “Mh, taarifa hizi kwa kweli sizijui. Nitakuwa kikaoni si muda mrefu. Nitauliza wenzangu…Nitakujulisha.” Hakupatikana hata alipoitwa tena na tena.

Taarifa zilizoenea katika nchi za Maziwa Makuu kuhusu hali kuelekea uchaguzi nchini DRC, zinasema “Kabila maji ya shingo.”

Mwezi ujao, Kongo-DRC inafanya uchaguzi mkuu wa pili tangu Rais Kabila amrithi baba yake, Laurent Kabila, aliyeuawa kwa kupigwa risasi na mmoja wa walioitwa “dogodogo” wa jeshi lake.

Jeshi la Kabila lililouondoa utawala wa Mobutu, lilikuwa na askari wa umri mdogo walioitwa “dogodogo.”

Naye Kanali Kapambala Mgawe wa makao makuu ya jeshi ambaye gazeti liliambiwa ni msemaji wa jeshi, amesema suala hilo “litakuwa ngazi ya kitaifa.”

Mwandishi: Ngazi ya kitaifa ndio wapi? Au kwa Waziri wa Ulinzi?

Kanali: Huko ni kwa rais.

Mwandishi: Lakini inaweza kuwa maombi yameanzia kwenu au angalau mnajua jambo hili?

Kanali: Vyovyote vile lakini kama nilivyokwambia, hilo litakuwa ngazi ya kitaifa. Hayawezi kuja kwetu. Ndio hivyo ndugu yangu. Asante.

Gazeti lilishindwa kumpata waziri wa ulinzi, Dk. Hussein Mwinyi. Simu yake imekuwa ikisema hapatikani.

Mwandishi wa rais, Salva Rweyemamu hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hili. Simu yake iliita bila kupokelewa. Hata ujumbe ambao ulipelekwa kwa njia ya simu ya mkononi (sms) haukujibiwa.

Taarifa kutoka Kinshasa zimeeleza kuwa Kabila ameanza kubadilisha marafiki baada ya maswahiba wake wa miaka mingi, Marekani na baadhi ya nchi za Jumuiya ya Ulaya, kumshinikiza kuhakikisha uchaguzi mkuu nchini mwake unakuwa huru na wa haki.

Marekani na Ulaya wanasema, hawako tayari kushiriki kwenye kuhujumu demokrasia ya Kongo; bali wako tayari kuunga mkono uamuzi wa raia wa nchi hiyo.

Haijafahamika mara moja kilichosababisha nchi hizo rafiki wa karibu wa Rais Kabila kubadilisha msimamo.

Wachambuzi wa mambo wanasema, Marekani na Jumuiya ya Ulaya wamesukumwa na upepo wa mageuzi katika nchi za Mashariki ya Kati.

Hata hivyo, duru za kisiasa nchini DRC zinasema tofauti na uchaguzi wa mwaka 2006, wapinzani wa Rais Kabila, ni makini sana uchaguzi huu.

Duru zinataja chama cha Union Democatie Populaire et Sociale (UDPS) na washirika wake, kuwa tayari wamejipanga kuhakikisha Kabila harejei madarakani katika uchaguzi huo.

Kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja katika kipindi ambacho baadhi ya wananchi wa Kongo-DRC wanahoji uraia wa Rais Kabila.

Kiongozi huyo aliyeingia madarakani mwaka 1998 baada ya kifo cha Laurent Kabila, si Mkongomani bali ni raia wa Rwanda wa kabila la Kitusi – kwa baba na mama.

Baba mzazi wa Joseph Kabila anaitwa Adrien Christofer Kanambe. Mama yake halisi anaitwa Macelina.

Adrien Christofer Kanambe alikuwa na mke aitwaye Macelina Kanambe, mama yake mzazi Joseph “Kabila.”

Uchunguzi unaonyesha kuwa Laurent Kabila na mkewe Sifa Mahanya ni wazazi wa “kuokoteza” wa Rais Joseph Kabila.

Gazeti la Jicho la Mzalendo limesema pia kuwa tayari askari wa Korea Kaskazini wametua mjini Kinshasa ili kutoa mafunzo maalum ya kutumia silaha, zikiwamo zile zilizoko nje na mikataba ya kimataifa.

Gazeti linadai serikali ya Rais Kabila imeagiza shehena ya silaha kutoka Korea Kaskazini. Baadhi yake, limesema zimehifadhiwa kwenye kambi mpya ya kijeshi ya Kingakati.

0
Your rating: None Average: 5 (3 votes)