Kadhia ya Magdalena Sakaya


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 22 June 2011

Printer-friendly version
Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Tabora (CUF), Magdalena Sakaya

KUANZIA Mei 28 hadi Juni 7 mwaka huu, Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Tabora (CUF), Magdalena Sakaya, alishikiliwa katika mahabusu ya gereza la wanawake wilayani Urambo mkoani Tabora.

Katika mahojiano yake maalumu na gazeti hili mapema wiki hii, Sakaya anasema alichokishuhudia katika siku zake hizo kumi za mateso kimebadili kabisa maisha na mtazamo wake kuhusu vyombo vya dola na ufuatwaji wa misingi ya utawala bora, haki na sheria hapa nchini.

“Nimejionea mwenyewe hali ambazo wananchi walioko mahabusu na magerezani wanaishi. Wanaishi katika maeneo ambapo hata ng’ombe watapata taabu kuishi.

“Katika siku yangu ya kwanza (Mei 28) katika mahabusu ya Polisi, niliwekwa katika chumba kimoja na wanaume. Hakukuwapo na choo na watu walitakiwa kujisaidia kwenye mifuko, mbele za watu nikiwamo mimi.

“Chumba kizima kilikuwa na harufu. Hakuna magodoro na hivyo watu wanalala sakafuni. Inzi na wadudu wa aina zote wanazunguka tu katika vyumba. Na kumbuka maisha hayo anaishi mahabusu ambaye bado hata hajatiwa hatiani. Huu ni utawala wa kikatili sana,” anasema.

Sakaya na wenzake 10 walikamatwa Mei 28 mwaka huu kwa madai ya kuchochea vurugu wakati wa sakata la ukamatwaji wa mifugo ya wafugaji wa Urambo wanaodaiwa kufanya shughuli zao katika eneo la hifadhi ya taifa.

Tayari serikali imefungua kesi dhidi ya Sakaya na wenzake hao ambayo inaendelea katika Mahakama ya Wilaya ya Urambo wakidaiwa kusababisha mkusanyiko, kupiga polisi mawe, kutaka kunyang’anya silaha, kujeruhi polisi na kukataa kutoa taarifa polisi.

Katika jambo ambalo Magdalena hataweza kulisahau ni siku ambayo waliomba ruhusa kwa polisi awaruhusu waende kula nje ya mahabusu hayo na askari huyo akahoji kwa dharau; “Hivi hamjafa tu? Tunataka kwenda kuwazika.”

Mbunge huyo na wenzake walishindwa kula ndani ya mahabusu hiyo inayonuka kwa siku nzima ya kwanza na ingawa waliomba waruhusiwe kula nje ya mahabusu, walikataliwa.

“Sasa katika siku ya pili, tukiwa tumeishiwa nguvu kabisa mimi na wenzangu kwa sababu ya njaa na uchovu, tulimuomba askari aturuhusu tutoke nje ya mahabusu tule. Na ndipo akatujibu, ‘hamjafa tu? Tunataka kwenda kuwazika.’ Hebu fikiria mtu anatoa jibu kama hilo, je kuna utawala wa sheria hapo?” anahoji.

Akisimulia tukio la ukamatwaji wake jinsi lilivyokuwa, Sakaya anasema siku nne kabla ya kukamatwa, alipata taarifa wakati akihudhuria vikao vya kamati za bunge jijini Dar esSalaam kuwa mifugo mingi ya wananchi inakamatwa na serikali wilayani Urambo.

“Nikampigia simu Mkuu wa Wilaya ya Urambo (Anna Magova) na kumuuliza kulikoni? Yeye akaniambia hana taarifa kwa vile yuko Tabora Mjini kwenyewe vikao. Ila akaniambia atanipigia baadaye kunipa taarifa rasmi.

“Na kweli akanipigia simu baadaye na kunithibitishia kuwa ni kweli mifugo imekamatwa. Nikamwambia si tulikubaliana mwaka jana kuwa wafugaji wasisumbuliwe hadi suluhu ya kudumu itakapopatikana? Imekuaje tena? Mkuu wa Wilaya akaniambia nisimfundishe kazi kwani uamuzi umeshafikiwa. Ndiyo nikaamua kwenda mwenyewe.

“Nilipofika Urambo, mimi na ujumbe wangu kutoka makao makuu ya chama (CUF) na wilaya ya Urambo, tulikwenda moja kwa moja kwenye Kata ya Usinge ambapo wafugaji wengi walinyang’anywa mifugo yao.

“Wananchi waliposikia tumefika wakaja kutupa malalamiko yao na sisi tukawa na kazi kubwa ya kutuliza. Wakati tukiwatuliza, mara ikaja gari ya polisi ikiwa imejaa askari na polisi wakaniuliza kwa nini nafanya mkutano wa hadhara bila ya kibali?

“Nikawaambia sijaitisha mkutano wowote wa hadhara. Ni wananchi tu ndiyo walikuwa wananipa malalamiko yao. Ndiyo tukakubaliana kuwa niende kwenyen makao makuu ya Kata ili nizungumze na viongozi wa serikali ya kijiji, askari na wawakilishi wa wananchi kutafuta suluhu.

“Lakini huko kwenye ofisi ya kata ndipo mifugo yote iliyochukuliwa na serikali ilikuwa imewekwa. Kwa hiyo tulipofika tukaambiwa ofisi imefungwa. Wakati tukihojiana kwa nini ofisi ya serikali imefungwa, polisi wakaja tena, safari hii kwa shari.

“Wakatutaka tuondoke la sivyo watatupiga risasi. Nikasema kwa nini mnataka kutumia nguvu wakati sisi tunataka suluhisho la amani? Ikapigwa risasi ya kwanza ikapita mbali. Ikapigwa ya pili ikapita karibu yangu. Karibu sana na ndipo watu walipoanza kushtuka.

“Kesi niliyofunguliwa inaendelea. Lakini watu waliopigwa na polisi hadi kutaka kuzimia ndiyo haohao waliofunguliwa kesi ya kutaka kupiga polisi. Ukimuona huyo mtu anayeshitakiwa kwa kupiga polisi utaona huruma.

“Kuna mwenzetu mmoja alipigwa sana na polisi na akawa katika hali mbaya. Ni mwanaume lakini alilia mpaka na mimi nikaanza kutokwa na machozi. Tulipopelekwa polisi naye akapelekwa badala ya hospitali. Usiku mzima alikuwa akilia kwa maumivu. Lakini askari walikuwa wakimdhihaki. Leo kafunguliwa kesi ya kupiga polisi.

“Kichekesho kilikuwa kwenye dhamana. Nilinyimwa dhamana eti kwa sababu ningeachwa ningesababisha uvunjifu wa amani. Lakini makosa yote niliyoshitakiwa kwayo hayaangukii katika makosa ambayo mtu ananyimwa dhamana
 
“Hakimu akataka wadhamini wangu waje na hati za nyumba. Sasa kijijini kule Urambo utapata watu wangapi wenye nyumba zenye hati? Hata wakili wangu (Twaha Taslima) alijenga hoja kwa hakimu kuwa hata yeye hana hati ya nyumba yake iliyoko Dar.

“Na tangu lini watu wakatakiwa kutoa hati za nyumba wakati utaratibu ni kupata wadhamini na uthibitisho wa barua kutoka kwa wenyeviti wa vijiji. Zote hizo zilikuwa ni njama za kunikomoa mimi, wenzangu na CUF kwa ujumla. Nchi hii haina kabisa utawala bora,”anasema.

Sakaya anatoa wito kwa serikali kufanya maamuzi ya busara na mapema kwenye kutatua migogoro ya wananchi wanaoishi kwenye maeneo yanayopakana na hifadhi kwa vile yanaweza kuzua maafa makubwa katika siku za mbele.

Anasema tatizo la ardhi linazidi kuwa kubwa kila kukicha na kama serikali itaendelea kupuuzia tatizo hilo, ipo siku nchi itaingia katika maafa makubwa ya ardhi baina ya wananchi na serikali yao.

Mbunge huyo ametoa tuhuma kwa baadhi ya viongozi na wanasiasa wa Urambo kuwa wanatumia nafasi zao kuchukua fedha kutoka kwa wafugaji wakidai kuwa watawasaidia wasifukuzwe.

“Serikali na wanasiasa (akiwataja majina) wanafaidika na hali hii ya sasa. Wanatumia nafasi zao kuomba hongo kutoka kwa wafugaji. Huu ni unyanyasaji na ni lazima ukomeshwe. Serikali ni lazima ifanye maamuzi ya haraka, anasema.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: