Kadhia ya Sakaya na bao la kujifunga la CUF


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 29 June 2011

Printer-friendly version

MAGDALENA Sakaya, mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chama cha Wananchi (CUF) na viongozi wengine wa juu wa chama hicho, walikaa rumande ya polisi kwa muda wa siku mbili.

Alikaa pia gerezani kwa takribani siku 10. Wenzake wengine ni Doyo Hassan na Amiri Kilungi. Wakiwa polisi vigogo hao wa CUF waliwekwa katika selo moja wote bila kujali jinsia zao. Huko alikunywa, kula na kujisaidia ndani ya chumba hicho kidogo kisichokuwa na choo.

Wakati hayo yakifanyika, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad yuko serikalini visiwani Zanzibar. Huko anashika wadhifa wa makamu wa kwanza wa rais. Anakula kuku kwa mrija!

Huko hayuko pekee. Karibu viongozi wote wa CUF visiwani Zanzibar wana madaraka makubwa serikalini. Baadhi yao ni mawaziri na manaibu wao na wengine wanasubiri siku yao ifike wapate fursa kama za wenzao hao.

Askari waliokuwa wakiwatesa akina Sakaya, wanalipwa na kutumwa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Chama hicho ndicho kinachounda serikali ya umoja wa kitaifa na CUF visiwani humo.

Hata kama mwafaka huo wa visiwani hauna nguvu Tanzania Bara, ningetarajia walau kuwepo kwa kuheshimiana miongoni mwa viongozi wa vyama hivyo viwili.

Hatua ya serikali kumlaza chumba kimoja Sakaya na vijana wa kiume, haionyeshi kuheshimiana kulikotarajiwa.

Wiki chache zilizopita, nilimuuliza kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa CUF kuhusu nini hasa chama hicho kimepata upande wa Bara mara baada ya mwafaka wa Zanzibar. Jibu lake lilikuwa fupi, “Nothing” (Hamna kitu).

Lakini viongozi na wanachama wa CUF upande wa Zanzibar wanasema mwafaka umesaidia kupatikana amani na utulivu visiwani humo.

Sababu inayotolewa na CUF ndiyo hiyohiyo iliyotolewa na Morgan Tsvangirai kuhalalisha hatua yake ya kuingia katika serikali ya pamoja na hasimu wake mkuu kisiasa, Rais Robert Mugabe.

Leo hii, umaarufu wa kisiasa wa Tsvangirai na chama chake cha MDC umepungua kiasi kwamba kimegawanyika katika mapande mawili makubwa. Hivi sasa kuna MDC ya Tsvangirai na ile ya Arthur Mutambara.

Umaarufu wa kisiasa wa Tsvangirai umeshuka kiasi kwamba sasa nafasi yake kama kiongozi wa chama hicho inaviziwa na Tendayi Biti.

Mugabe anaendelea na madaraka yake. Upinzani unakufa taratibu kwa migogoro ya ndani kwa ndani. Wale ambao wamewekwa karibu na Mugabe hawataki kutoka kurejea ndani ya chama ili kukipa uhai. Wameonja tamu na hawataki tena chungu.

Wakati akina Maalim Seif, Juma Duni Haji na Abubakary Khamis Bakari wakila kuku kwa mrija, wenzao akina Sakaya na Kilungi walikuwa wamelala katika selo ya polisi na kupata mlo wao juu ya vinyesi na mikojo.

Hicho ni chama kimoja cha siasa. Wabunge wake na viongozi wake wanakamatwa. Lakini kwa upande wa pili, viongozi wake wakuu na wawakilishi wake wanakula “bata.”

Katika harakati zozote za kisiasa, hakuna chama ambacho kinajengwa wakati kuna makundi mawili ya watu ndani ya chama.

Fidel Castro na Ernesto Che Guevarra, walimpindua Dikteta Fulgencio Batista kwa sababu, pamoja na mambo mengine, walikula, kunywa na kulala pale walipokuwa wakilala wafuasi wao. Walikuwa nao pamoja karibu katika kila kitu.

Kama ilivyo kwa Tsvangirai, Maalim Seif hawezi tena kuzungumzia kwa ukali shida ya maji zinazowakabili wananchi wa Zanzibar. Hawezi kuzungumzia matatizo ya umeme, mfumuko wa bei wala ukosefu wa ajira. Naye ni sehemu ya matatizo yaliyopo.

CUF ingeendelea kuwa imara kama Seif na wenzake wangekubali kukaa pembeni. Hata kama hali ya kisiasa ingechafuka Zanzibar, wakulaumiwa wasingekuwa CUF. Ni CCM na serikali yao.

Serikali ya mseto ikifanya vizuri, CCM itachukua sifa na kama ikifanya vibaya, CUF itajitoa wapi wakati ni sehemu ya serikali hiyo na ina wawakilishi karibu kila sehemu?

0718 81 48 75
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: