Kagoda? Tufike tamati


editor's picture

Na editor - Imechapwa 26 May 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

WATANZANIA wakiulizwa wanachokitaka kuhusu ufisadi wa kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, tunaamini watasema kwa sauti kali, “kamata hao, shitaki hao sasa.”

Jibu hili litawaudhi wengi katika uongozi wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa sababu bado hawaoni kukamata wenye Kagoda na kuwashitaki kuwa ni jambo la maslahi kwao.

Lakini hata ukiuliza wananchi kwa kiasi gani hawapendi ahadi za serikali kuhusu kushughulikia Kagoda, jibu litakuja kwa kiwango hichohicho. Watasema, “Ahadi zimetutosha tunataka hatua.”

Hata hapo viongozi wa serikali hawatafurahi. Watakasirika na kukasirikia wananchi. Wanataka nini kumbe? Funika kombe mwanaharamu apite. Wanaficha wanachokijua.

Hili ndilo tatizo kubwa la serikali ya CCM na linaiangamiza kadri 2010 inavyokaribia. Pale penye ukweli na wao viongozi wakiufahamu ukweli wenyewe, hawana moyo wa kuachia ili wananchi nao waufahamu.

Kibano kinachoisibu Kagoda na wenyewe ni kikubwa kiasi cha mtu kushangaa ingekuwa serikali yetu ni  makini – ile ambayo wakuu wake wana dhamira ya kweli ya kupambana na ufisadi – tungekwishajua moja la maana.

Serikali imeshindwa kubana wenye Kagoda na sababu ni moja tu: Kagoda imepumbaza uongozi hadi kuwa wapowapo tu. Au, kama mkondo unavyoelekeza, Kagoda ni ya baadhi ya walioko madarakani.

Serikali inaimba vita dhidi ya ufisadi lakini inacheza ngoma ya kuenzi ufisadi. Vinginevyo ingekuwa imekamata wahusika. Inawajua.

Lakini kama viongozi hawataki kukamata wenye Kagoda kwa kuwa wanaamini hawajatenda kosa lolote, si wanyamaze basi? Kwanini wanatoa ahadi?

Watanzania wamechoka kusikia viongozi wa serikali na taasisi zake wakizungumzia uchunguzi wa Kagoda na ahadi za kutoa taarifa. Hizo ni ndoto milele.

Wanajua serikali yao imeshawaangusha katika hili. Wanajua viongozi wanapotamba kupambana na ufisadi, hawako hasa makini na ufisadi wenyewe.

Hawagusi kamwe mapapa wanaonenepeana kwa miradi mikubwa na mipango ya kuchota mabilioni ya shilingi. Hawa na wao ni chanda na pete. Wamejenga ubia zamani na umesaidia kufanikisha mambo yao kwa pamoja.

Kipi kipya anachoahidi Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) au Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), na mwingine yeyote serikalini ambacho hakijapatikana kuhusu Kagoda?

Uchunguzi gani usioisha? Wananchi wamechoka kusubiri, hasa pale ambako hakuna sababu za kusubiri.

Tu watu makini. Tunafikiri na kupima. Tunajua anayesema ukweli na anayedanganya. Bali tumefika tamati. Lisemwe lililopo ili tuanze ukurasa mpya.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: