Kagoda yamwakia Kikwete


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 15 September 2009

Printer-friendly version
Wahisani washinikiza ukaguzi
Misaada ya wafadhili yakatwa
Rais Jakaya Kikwete

SERIKALI imesalimu amri. Imerudisha nchini maodita wa Deloitte & Touche kutoka Afrika Kusini kufanya tena ukaguzi ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), MwanaHALISI limegundua.

Taarifa zinasema kurejeshwa kwa maodita hao wa kimataifa kumetokana na shinikizo la nchi wahisani wanaotaka serikali kufikisha mahakamani watuhumiwa wote, akiwamo mtuhimiwa mkuu, kampuni ya Kagoda Agriculture Limited.

Serikali imelazimika kukubali kurudisha nchini maodita hao kama moja ya masharti ya kupata misaada.

Tayari kampuni ya Deloitte & Touche imeanza kufanya ukaguzi katika baadhi ya akaunti ndani ya BoT.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya gazeti hili, miongoni mwa akaunti ambayo itakaguliwa ni Na. 99915091 01 ambayo ilitumiwa na Kagoda kukwapua mabilioni ya shilingi za umma.

Kampuni ya Deloitte & Touche ndiyo yenye taarifa nyingi na za kuaminika juu ya Kagoda.

Kumekuwa na taarifa zisizothibitishwa kwamba maodita hao, kutoka Afrika Kusini, ndio waliondoka na faili la Kagoda baada ya kutokea kutoelewana kati yake na serikali.

"Serikali imeamua kurudisha hawa Deloitte & Touche kwa sababu mbili kubwa. Kwanza, shinikizo kutoka kwa wahisani na pili, serikali kujua kuwa maodita hao ndio waliondoka na faili orijino (halisi) la Kagoda," ameeleza mtoa taarifa hizi.

Amesema, "Serikali imeamua kuwarudisha ili ukweli uweze kujulikana."

Kurejeshwa nchini kwa maodita hao kunaelezwa kuwa kunaweza kuathiri uhusiano kati ya rais Kikwete na baadhi ya marafiki zake ambao wamekuwa wakitajwa kuhusika na Kagoda.

Kwa mfano kumekuwa na madai kuwa Kagoda inamilikiwa na mfanyabiashara na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz. Mbunge huyo amekuwa akikana madai hayo hadharani.

Hata hivyo, Alhamisi iliyopita wakati Kikwete akijibu maswali ya 'moja kwa moja' ya wananchi alisema, "katika vita dhidi ya ufisadi sina rafiki wala ndugu."

Rais alikuwa akijibu swali la msikilizaji mmoja aliyetaka kujua kwa nini serikali imeshindwa kuchukulia hatua watuhumiwa wakuu wa Kagoda na kampuni tata ya Richmond Development Company (LLC).

Mwanzoni mwa mwezi Septemba 2006 serikali iliwapa maodita kazi ya kuhakiki hesabu za BoT kwa mwaka wa fedha 2004/2005.

Hata hivyo, kabla ya kazi hiyo kukamilika, zogo kubwa lilizuka kati ya maodita na BoT na hatimaye serikali ikavunja mkataba wake na maodita hao, mwezi mmoja baada ya kusainiwa.

Taarifa kutoka ndani ya BoT zinasema kufukuzwa kwa maodita hao kulitokana na uchunguzi walioufanya katika faili la Kagoda ambalo lilikuwa limehifadhiwa kwa siri na gavana wa benki wakati huo, Dk. Daudi Ballali.

Afisa mmoja wa BoT, jina tunalo, ndiye anayetuhumiwa kukabidhi faili la Kagoda kwa maodita.

Baada ya maodita kutoridhishwa na nyaraka zilizotumiwa na Kagoda kuchukulia dola za Kimarekani 40 milioni, Septemba 2006, waliandika barua kwa gavana Ballali wakitaka maelezo ya jinsi fedha hizo zilivyolipwa.

Imeelezwa kwamba Ballali hakujibu barua hiyo, badala yake alilishusha zigo hilo kwa Zakia Meghji aliyekuwa waziri wa fedha.

Taarifa zinasema Megji, kwa shinikizo la kigogo mmoja, aliandika barua kwa maodita akisema fedha za Kagoda zilitumika kwa "shughuli za usalama wa taifa."

Hata hivyo, 16 Septemba 2006, Meghji aliandika barua nyingine akikana ile ya awali. Safari hii akiwa kama aliyetoka usingizini, Meghji alisema alipotoshwa na gavana Ballali.

Kuondoka kwa Deloitte & Touche kulitia doa serikali na hivyo ikalazimika kuita kampuni ya Ernst & Young ili kumaliza kazi iliyokuwa imeanzwa na kampuni hiyo ya Afrika Kusini.

Katika ukaguzi wao, Ernst & Young waligundua kuwa Kagoda ilikwapua kwa mpigo dola 30.8 milioni na kuzitawanya katika mabenki saba kwa mkupuo nchi mzima.

Katita ukaguzi uliofanywa na Ernst & Young, zaidi ya Sh. 133 bilioni zilibainika kuwa zilikwapuliwa katika mazingira ya kutatanisha, Kagoda ikiwa miongoni mwa makampuni 22 yaliochotewa fedha za EPA.

Kuja kwa maodita kutaweza kusaidia kupatikana kwa kumbukumbu sahihi juu ya Kagoda.

Taarifa zinasema hata maofisa wa serikali, wakiwamo wale wa Kamati ya Rais Kikwete ya kuchunguza sakata la EPA, wameshindwa kuthibitisha rasmi tarehe ambayo mikataba ya makubaliano (Deed of Assignment) ilipokelewa BoT.

Utata mwingine ni kile kilichoelezwa kuwa ni kutengeneza taarifa za uongo au kuvuruga ushahidi wa maandishi. Baadhi ya maofisa wa BoT waliohojiwa wamedai kuwa walikuwa wakifuata maelekezo ya "wakubwa" zao.

Tayari kuna taarifa kwamba makachero wa Tanzania wamelazimika kwenda Ujerumani na Singapore kwa ajili ya kuchunguza baadhi ya kampuni zilizohusishwa na Kagoda, lakini kuingia kwa Deloitte & Touche kunasemekana kutarahisisha kazi.

Vyanzo ndani ya serikali, vinasema ulazima wa maofisa hao kwenda nje ya nchi umetokana na maelekezo ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ambaye alishauri maeneo ya kukamilishwa kabla wahusika kutajwa na kufikishwa mahakamani.

Uchunguzi umebaini kuwa kampuni mbili za Frankfurt, Ujerumani za Lindeteves J. Export BV na Hoechst, ndizo ambazo maelezo yake yameonyesha kuwepo kwa utata ambao unahitaji kutafutiwa maelezo ya ziada.

Wakati kampuni ya Lindeteves J Export BV inaonekana kwamba ni ya Ujerumani, taarifa zinaonyesha kwamba kampuni hiyo ipo nchini Singapore na si Ujerumani; na hakuna ushahidi wowote kuonyesha kwamba kampuni hiyo ina ofisi Frankfurt nchini Ujerumani.

Kwa upande wa kampuni ya Hoechst, imebainika kwamba ofisi za kampuni hiyo zimekosewa na kwamba iliungana na kampuni nyingine iitwayo Rhone Poulence tokea mwaka 1999 kabla hata ya Kagoda kudai kuingia mkataba nayo.

Hadi sasa wahusika wa kampuni ya Kagoda ambao ndiyo chanzo halisi cha kuibuka kwa sakata la wizi wa fedha za EPA, wamebaki kwenye minong'ono tu.

Mbali na Rostam, wakili wa mahakama kuu, Bhyidinka Michael Sanze anawataja baadhi ya watu wanaohusika katika mradi wa Kagoda kuwa ni pamoja na Benjamin Mkapa, Daud Ballali na Meregesi.

Mikataba ya ununuzi wa madeni kwa makampuni 12 ilisainiwa katika kasi ya kufumba na kufumbua, katika kipindi kifupi cha 25 – 10 Septemba 2005 na 5 Novemba 2005.

Imefahamika kuwa nyaraka zote zilisainiwa na wakili mmoja tu, Bhyidinka Michael Sanze wa Malegesi Law Chambers ya Dar es Salaam, na kati ya hizo, mikataba minne ilisainiwa 18 Oktoba 2005 na mitano ilisainiwa siku moja baadaye, 19 Oktoba 2005.

"Haiingii akilini kuona wawakilishi wa makampuni yote haya ya kigeni walivyoweza kusafiri kwa wakati mmoja kuja nchini wakitofautiana kwa saa chache," ameeleza wakili mmoja wa kujitegemea.

Hatua ya kurejesha maodita wa Deloitte & Touche nchini imechangiwa, kwa kiasi kikubwa na serikali kukosa kiasi cha dola 312 milioni (zaidi ya Sh. 400 bilioni) kutoka Benki ya Dunia (WB).

Serikali ilitarajiwa kupata mkopo nafuu wa dola 2,157 milioni kati ya mwaka 2008 na 2011. Badala yake sasa fedha hizo zimepungua hadi dola 1,845 milioni.

Kwa mujibu wa WB, hadhi ya Tanzania imeshuka kufuatana na vigezo vya utawala bora.

Ofisa wa WB aliyetajwa kuwa miongoni mwa walioshiriki kuweka vigezo hivyo, Paolo Zacchia, amenukuliwa akisema, kashfa za wizi wa fedha – ikiwemo ya Kagoda, ndizo zimeleta mgogoro kwa Tanzania.

Tanzania imeshuka kutoka nafasi ya 10 katika ripoti ya WB ya mwaka 2007, hadi nafasi ya 16 kwa ripoti ya mwaka 2008.

Vigezo ambavyo Tanzania imeonyesha kushuka sana ni pamoja na uwazi, uwajibikaji na mapambano dhidi ya rushwa.

Nchi zote zinazopokea mikopo kutoka WB zimekuwa zikipimwa kwa vigezo 17 vikiwamo vinavyohusu matumizi, usimamizi na udhibiti wa fedha na rasilimali katika sekta za umma.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: