Kama Ghana; kwa ari na nguvu zaidi


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 04 August 2010

Printer-friendly version

WAKATI nipo Ghana hivi karibuni, kuna siku nilipatwa na mshangao baada ya kukutana na wazungu wawili; mmoja mwanamke mwingine mwanamume, wakitembea kwa miguu eneo la Osu, katikati ya jiji la Accra, majira ya saa tano usiku.

Mimi na wenzangu kutoka Tanzania, Ghana na Liberia, tuliokuwa tukipata chakula saa hizo tulipatwa na mshangao kwa tukio hilo.

Osu ni eneo kama Kariakoo hivi ambapo kwa kawaida huwa na vitendo visivyofaa nyakati za usiku vikiwamo vile vya kuhatarisha usalama.

Baada ya kuulizauliza hapa na pale, ndipo nikapewa sababu iliyofanya wazungu wale watembee kwa miguu saa zile bila ya wasiwasi.

Sababu kubwa ilikuwa ni hali ya usalama na ukarimu miongoni mwa Waghana. Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol), Ghana ndiyo taifa salama zaidi barani Afrika.

Interpol katika ripoti yake ya karibuni zaidi imeonyesha kwamba matukio ya uhalifu nchini Ghana ni karibu nusu ya idadi ya matukio ya namna hiyo katika nchi za Afrika.

Usalama huu wa Ghana ndiyo unaowapa kiburi wageni kuzurura watakavyo ndani ya nchi hiyo na katika muda watakao.

Hali hii imeifanya Ghana kuwa miongoni mwa nchi za Afrika zinazoingiza fedha nyingi kutokana na utalii ingawa haina vivutio vingi kama vya kwetu.

Na kwa sababu ya ukosefu wa vivutio vya maana, ndiyo maana nchi hiyo imeamua kuwekeza sana kwenye utalii wa utamuduni, ikitumia sana tawala za kikabila ambazo zinaendelea hadi leo.

Kwa hiyo, Mmarekani anayekwenda Ghana leo, atarajie kuelezwa kuhusu historia ya kabila la Asante na namna watawala wake walivyopigana na ukoloni.

Wageni hao watanunua bidhaa za asili za Ghana, mavazi ya asili ya nchi hiyo na watajitahidi kula vyakula la jadi vya watu wa eneo walilotembelea. Hizo zote ni fedha.

Sisi tunaendelea kujisifia tu na Mlima Kilimanjaro, Zanzibar na Serengeti. Ingawa ni kweli kwamba hayo yote ni utajiri, tunapaswa pia kutumia utamaduni wetu.

Kwa mfano, wimbo wa vazi la taifa umeacha kuimbwa siku hizi. Wenzetu huku wana mavazi yao na wanafanya kila wawezalo kuyatangaza. Fursa ipo na tunatakiwa kuitumia.

Pia, Tanzania ina utajiri wa kiutamaduni ambao ungeweza pia kuuzwa. Wajerumani wangetaka sana kutembelea Isimani na kupata historia ya Chifu Mkwawa na Wahehe.

Waarabu wangetaka sana kutembelea Kilwa na Mikindani. Wengine wangetaka kufika hadi Tabora. Barabara hakuna lakini mbaya zaidi, inaonekana tumeanza kuutupa utajiri wetu wa utamaduni.

Wenzetu wanatengeneza mamilioni ya dola kwa kuuza nguo zao, historia yao na tamaduni zao. Hili tunaweza kabisa kuliiga.

Lakini kubwa zaidi linalozidi kuipa sifa Ghana nje ya Afrika ni ukarimu wa watu wake. Wananchi wa hapa naweza kuwalinganisha na Watanzania.

Ila, kwa sababu ya tawala za jadi kuendelea kuwa na nguvu, wananchi wa Ghana wameendelea kuwa na utaratibu wa jadi wa kiafrika kuwa wakarimu kwa wageni.

Familia za Ghana hugombana pale inapobainika mmoja wao hakumtendea vema mgeni yeyote, mweusi au mweupe, aliyewatembelea.

Kama ilivyokuwa kwa babu zetu, wananchi wa kawaida wa Ghana hujisikia fahari kumsaidia mgeni yeyote anayehitaji msaada kutoka kwake.

Kwa hiyo, mtalii atalipa gharama sawa ya teksi kama ambavyo angelipa raia wa nchi hiyo. Si kama nchi nyingi za Afrika, Tanzania ikiwamo, ambapo mtalii ‘anagongwa’ mpaka kichwa kinamuuma.

Binafsi ni muathirika wa ukarimu na uaminifu huu wa Waghana. Wiki iliyopita nilisahau mzigo wangu kwenye teksi iliyokuwa imenitoa mjini.

Vitu nilivyonunua vilikuwa na thamani kubwa. Hata hivyo, nusu saa baadaye, baada ya dereva yule kubaini kwamba ana mzigo usio wake, na tayari akifahamu kwamba mimi ni mgeni, alirudi hadi hotelini kwangu na kuuliza hadi kunipata na nikapata mzigo wangu.

Ukarimu unalipa. Hivi sasa, Ghana ndiyo nchi inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya raia wa kigeni kutoka Ulaya na Marekani wanaokwenda kufanya kazi za kujitolea nchini humo.

Wageni hao wanakwenda kufanya kazi kama manesi, walimu, mabibi afya, wakandarasi, madaktari na fani nyingine katika maeneo ya vijijini ambako huduma hizo zinahitajika sana.

Hawa wamesaidia sana katika kupunguza lile pengo baina ya mahitaji halisi ya huduma na idadi ya watoa huduma waliopo.

Matokeo yake, Ghana imekuwa miongoni mwa nchi za Afrika zenye idadi ndogo ya vifo vya akina mama wakati wa kujifungua na watoto walio chini ya miaka mitano.

Tanzania, ambayo wastani wa vifo vya akina mama wakati wa kujifungua inafikia 400 katika watu 100,000 ingeweza kufaidika sana na wafanyakazi wa kujitolea.

Wanachohitaji wafanyakazi hawa ni kuonyeshwa upendo na ukarimu na wananchi pamoja na serikali yao.

Hawawezi kwenda kuishi katika nchi ambayo kila huduma inapandishwa bei kwao eti kwa vile wana rangi tofauti na sisi.

Hawataki pia kwenda mahali ambapo hakuna tofauti sana na walikotoka. Eti mtu katoka London, New York au Berlin anakuja kujitolea Tanzania halafu anapelekwa Muhimbili na anapewa nyumba Upanga.

Hawa wakija, wanafurahi kama wanapelekwa Nanjilinji, Nkasi au Mpiga Miti. Huko ndiko wanakoweza kutoa msaada zaidi kwa nchi yetu. Lakini sasa tuwe tayari.

Hili la ukarimu ni jukumu letu sote na si la serikali pekee. Ni rahisi sana kwa jina la nchi nzima kuchafuliwa kwa tukio moja; tena la bahati mbaya dhidi ya raia mmoja wa kigeni.

Tayari watu wetu wanasifika kwa ukarimu lakini matukio ya karibuni yanaonyesha wananchi wameanza kuiacha pembeni sifa hii muhimu kwa nchi kama yetu.

Kwa mfano, wale wazungu raia wa Uholanzi waliokuja nchini na kunusurika katika ajali ya ndege iliyotaka kuligonga gari lao kule mkoani Tanga, waliondoka mara moja baada ya tukio hilo.

Kama walikuwa wameambiwa Tanzania ni nchi ya watu wakarimu, watakuwa wameshangazwa na watu waliokwenda kuwapora mabegi yao na fedha badala ya kuwaokoa katika hatari.

Hii si Tanzania tunayoitaka. Tukiwa wakarimu, tukawa wenye upendo na tukijali tamaduni zetu, tutafaidi kuliko tukitaka kwenda tunakoelekea sasa. Tubadilike.

0
No votes yet