Kama hatutaki kashfa, tujiandae


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 27 April 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

WIKI iliyopita, MwanaHALISI liliandika kuhusu mgogoro mkubwa uliopo nchini Ghana sasa ambapo mke wa rais mstaafu wa taifa hilo, Nana Konadu Agyemang, ametangaza kutaka kuwania urais.

Pamoja na mengi yaliyosemwa, Waghana wengi sasa wamebaini kuwa tatizo lao kubwa ni kuwa taifa lao halijajenga utaratibu mzuri wa kutengeneza watawala wajao wa taifa lao.

Matokeo yake ni kuwa kila mtu anadhani kuwa ana uwezo wa kuwa rais wa taifa lao. Hali kama hiyo inayoikumba Ghana hivi sasa, inaonekana ipo pia hapa nchini Tanzania.

Mtu yeyote mwenye uwezo wa kifedha, maarufu au mpenda sifa, anaweza tu kutumia nafasi yake kuwania nafasi yoyote ya uongozi anayoruhusiwa kuwania. Uwezo wake ni fedha na umaarufu alionao.

Na tatizo hili linaonekana limesambaa katika maeneo mengi barani Afrika. Na hii ni kwa sababu, viongozi wengi wa wakati wa uhuru wa bara la Afrika, hawakuwekeza kwenye kuandaa viongozi wapya, waliwekeza kidogo au waliwekeza vibaya.

Kwame Nkrumah, kwa mfano, anashutumiwa nchini Ghana kwa vile chuo cha mafunzo ya uongozi alichoanzisha nchini humo, kilifundisha zaidi itikadi za Nkrumah, mambo yake aliyoyafanya kwa ajili ya taifa lake na mambo ya chama cha Nkrumah cha CPP.

Kwa hiyo, ingawa alianzisha chuo, mafunzo hayakuwa sahihi. Haiwezekani chuo kikaanzishwa kwa ajili ya kumtukuza mtu au chama kimoja. Kwa mbali, nafikiri hili pia ndilo tatizo lililokikumba Chuo cha Kivukoni kilichoanzishwa na Mwalimu Nyerere.

Wengine kama akina Mobutu Sesseseko, hawakuwa na mpango wa kuandaa viongozi kwa vile walijua wao na familia zao watatawala maisha. Na siwalaumu wazee wetu hawa kwa vile wengi wao walilelewa katika mazingira kichifu kutoka katika makabila yao; ambako ukoo wa utawala ulikuwa mmoja tu.

Ndiyo maana, leo hii inaonekana nchi nyingi za Afrika zitapata shida mara baada ya viongozi waliopo sasa madarakani kuachia ngazi.

Nchini, Kenya, haijulikani nini kitafuata baada ya akina Raila Odinga, Uhuru Kenyatta na Kalonzo Musyoka kuamua kuachia ngazi. Na hata hao waliibuka tu kwa sababu ya mahusiano yao na familia zilizotawala nchi hiyo mara baada ya Uhuru.

Ukienda Uganda, wananchi hawajui nani atachukua nafasi ya Yoweri Museveni. Yapo maneno kuwa mwenyewe anamuandaa mwanaye wa kumzaa, Muhoozi Kainerugaba, kuchukua nafasi yake jambo ambalo walio wengi wanadhani si sahihi.

Lakini, kama nchi zenyewe hazijaweka taratibu za kuandaa viongozi wa baadaye, tunategemea nini kutoka mfumo huu wa siasa za soko huru?

Wapo wanaodhani kuwa mfumo kama wa China ambapo wananchi tayari wanajua nani watachukua madaraka mwakani, si mzuri kidemokrasia.

Lakini kuna mambo mawili makubwa ya kutazama. Moja ni kuwa kama siasa za nchi hazina ushindani mkubwa kama wa Marekani na Uingereza, ni muhimu kuweka utaratibu mzuri wa kupokezana madaraka ndani ya chama chenye nguvu.

Pili ni katika mazingira ambayo upinzani ni mkubwa. Hapa ni muhimu kuwa na taratibu, kanuni na sheria zitakazohakikisha kunakuwapo na usawa miongoni mwa wagombea.

Kwamba wakati Barack Obama, mtu mwenye uwezo wa wastani wa kifedha, anapoanza kampeni, apewe fursa sawa na mamilionea kama Hillary Clinton na John McCain.

Kunatakiwa pia kuwepo na Mahakama na Tume Huru za Uchaguzi zitakazohakikisha kuwa haki itatendeka. Katika mazingira ya Tanzania ya sasa; hili la pili hatujalifikia na hivyo kazi inakuwa kwa chama kilicho madarakani kuandaa viongozi wajao.

Ni chama ndicho kinachotakiwa kutambua vijana ambao wana uwezo mkubwa wa uongozi. Na hili linaweza kufanyika mitaani walipo wajumbe wa nyumba kumi na viongozi wa serikali za mitaa.

Linaweza pia kufanyika katika shule kuanzia za msingi hadi sekondari ambapo nadhani walimu wana nafasi kubwa ya kutoa maoni kuhusu vijana wanaowafundisha. Walimu hawa wanaweza kufanya kazi za chama.

Vijana hawa wanaweza pia kutafutwa kwenye vyuo vya elimu ya juu ambako nafikiri kuna wigo mpana zaidi wa kubaini viongozi.

Ukifuatilia historia za viongozi wengi waliopata mafanikio, utabaini kuwa walianza kuwa viongozi tangu wakiwa mashuleni au mitaani walikokuwa wakiishi.

Wakati nikikua katika maghorofa ya Shirika la Reli eneo la Polisi Ufundi jijini Dar es Salaam katika miaka ya 1980, mara zote wazee wetu walikuwa wakimchagua kijana mmoja aliyeitwa Charles (nimesahau jina lake la pili) kuwa kiongozi wao.

Nadhani alikuwa kijana kuliko wenzake waliomchagua lakini walikuwa wakimpa nafasi. Hakukuwa na rushwa yoyote aliyoitoa. Na alikuwa kiongozi mzuri na mtu mzuri pia.

Na wengi wa viongozi waliopo sasa, iwe Jakaya Kikwete, Yoweri Museveni, Barack Obama au Meles Zenawi, wengi walifanya kazi za kujitolea kwenye vyama au serikalini wangali vijana.

Hii maana yake ni kuwa vyama, hususani chama tawala, ni muhimu kikatoa nafasi kwa vijana hao wenye vipaji kufanya kazi za kujitolea na kuajiriwa ndani ya vyama au serikali.

Wakipata uzoefu wa kazi na huku wakipewa fursa mbalimbali za mafunzo, tutashangaa nchi yetu ikibarikiwa kuwa na rundo la viongozi waliotokana na watu, wenye vipaji na wanaojua wanachotakiwa kufanya.

Taifa letu, kwa hali iliyopo sasa, linaweza kujikuta siku likitawaliwa na muuza dawa za kulevya au kijana ambaye hajawahi hata kuwa katibu kata zaidi ya kuwa mtoto wa kigogo mmoja wa nchi yetu.

Na itakuwa aibu kiasi gani kwa nchi yetu wakati tutakaposikia rais wetu huyo akinyakuliwa na majeshi ya kigeni (kama ilivyokuwa kwa Jenerali Noriega wa Panama), ili akashitakiwe kwa makosa yake ughaibuni!

Na tukiwa na utaratibu mzuri, itapunguza vita ya kila mara ya kuwania madaraka miongoni mwa viongozi wetu. Tunajua sasa kuwa kutakuwa na uchaguzi mwaka 2015 wa kutafuta mrithi wa Kikwete.

Kama sote tungelijua nani anafuata, si ingepunguza vita hii iliyoanza sasa ambayo haitakwisha hadi kieleweke? Na tunajua tutakua tumeathirika kiasi gani kama taifa kufikia wakati huo?

0718 81 48 75
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: