Kama JK, kama Prof. Mbwette


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 21 March 2012

Printer-friendly version

WASAIDIZI wa Rais Jakaya Kikwete sasa wameanza kuiga utendaji wake katika kuongoza asasi za umma, MwanaHALISI limegundua.

Profesa Tolly Mbwette, makamu mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), ameiga mtindo wa Rais Kikwete wa “kusamehe wezi.”

Aliliambia gazeti hili kuwa katika chuo hicho kumetokea wizi wa mamilioni ya shilingi na amechukua hatua mbalimbali za kushughulikia tatizo hilo.

Alipoulizwa ni hatua gani amechukua, Prof. Mbwette alisema, ametumia staili ya Rais Kikwete ya “kuingia mkataba na watuhumiwa.”

“Tuliingia mkataba ikiwa ni utaratibu wa kawaida kama ambavyo Rais Jakaya Kikwete alifanya kwa baadhi ya watuhumiwa wa fedha za EPA (Akaunti ya Madeni ya Nje),” alisema.

“Sijafanya kosa hapa. Wewe si unajua kuwa hata rais wetu aliagiza waliochota fedha kutoka akaunti ya EPA wazirudishe la sivyo watashitakiwa?” alihoji kwa sauti ya kujiamini.

Kilichofuatia hatua hiyo, zimeeleza taarifa ndani ya chuo, ni menejimenti ya chuo kuandaa mkataba wa maelewano na watuhumiwa waliokiri kukwapua fedha hizo.

Taarifa hizi zimethibitishwa na Profesa Mbwette mwenyewe alipohojiwa na MwanaHALISI wiki iliyopita, kuhusu hatua aliyochukua kuhusiana na walioiba fedha OUT.

Mwaka 2008, Rais Kikwete alitangaza hadharani kuwa wafanyabiashara wote waliothibitika na, au kukiri kukwapua fedha kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wazirejeshe.

Rais alitoa miezi mitatu kwa wafanyabiashara wezi kurejesha fedha hizo, vinginevyo angelekeza wafikishwe mahakamani kwa mashitaka ya ufisadi.

Hata hivyo, tangu hapo, mpaka sasa, serikali haijatoa orodha yoyote ya waliorejesha fedha na nani hawakurejesha na wepi walitakiwa kushitakiwa mahakamani.

Gazeti hili ndilo liliripoti, kwa mara ya kwanza, wizi wa Sh. 800 milioni ndani ya OUT. Kwa mujibu wa taarifa za awali, Sh. 500 milioni kati ya fedha hizo, zimeibwa idara ya malipo ya mishahara iliyokuwa ikiongozwa na Egnelus Mlekaria.

Fedha nyingine zaidi ya Sh. 300 milioni, zimeelezwa kupotea mikononi mwa mtumishi aitwaye James Rweikiza, aliyekuwa mhasibu na mkuu wa kitego cha mikopo ya wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho.

Ripoti hiyo ilimsukuma Prof. Mbwette kuitisha mkutano wa waandishi wa habaria ambapo alikiri “upotevu wa fedha.”

Alieleza kuwa wapo watuhumiwa wamekabidhiwa kwa jeshi la polisi kwa uchunguzi na hatua zaidi za kisheria. Alimtaja Mlekaria kuwa alipewa nafasi ya kurejesha fedha alizotuhumiwa kuiba.

Kwa hatua hiyo, Prof. Mbwette anasema, ni vema jamii, hususani vyombo vya habari, “vikapongeza juhudi za chuo za kizalendo kufikisha suala hili kwenye vyombo vya dola ikilinganishwa na asasi nyingine ambazo hukaa kimya katika wizi wa fedha za umma.”

“Sisi ni mashujaa,” alijigamba Prof. Mbwette mithili ya mwanasiasa na kuongeza, “Kwa sasa uchunguzi unaendelea kuwabaini watuhumiwa wengine walioshirikiana na watuhumiwa hawa (Mlekaria na Rweikiza).”

Amesema watuhumiwa wengine bado wanachunguzwa ndani ya chuo na benki ambazo alidai zimetumika kusababisha wizi huu. Hakutaja benki zinazohusika.

Taarifa za uhakika ambazo gazeti hili limezipata jijini Dar es Salaam, zinasema wizi katika idara ya mishahara OUT ni wa zaidi ya miaka mitano, wakati ule wa mikopo umefanyika ndani ya “miaka ya karibuni.”

Uchunguzi umebaini kuwa Mlekaria anadaiwa kuchota fedha kupitia mishahara ya wafanyakazi hewa, baadhi yao wakiwa wamekwishahama au kufariki dunia.

Gazeti hili limethibitisha kuwa hadi sasa, Mlekaria hakutimiza “maelewano” ya kurejesha fedha. Hali hii, inatajwa kuwa ndio imechochea suala lake lifikishwe Polisi.

Hata hivyo, yapo malalamiko kuwa kesi hizo zinacheleweshwa makusudi kama mkakati wa kuwezesha suala hilo kumalizwa kienyeji.

Kesi inayomhusu Rweikiza ipo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: