Kama mnajua, epusheni balaa


editor's picture

Na editor - Imechapwa 07 September 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

WIKI iliyopita Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alionya kwamba kuwepo kwa viongozi wengi wasio waadilifu, wenye uchu wa mali na wanaojilimbikizia mali nchini kunahatarisha amani na utulivu.

Akizungumza katika sherehe za kusimikwa kwa askofu wa pili wa Kanisa Anglikana, Dayosisi ya Tanga mjini Korogwe mwishoni mwa wiki, Pinda alisema kuwa hali hiyo inatokana na wananchi kuchoshwa na maisha ya umaskini.

Hofu ya Waziri mkuu inatokana na ukweli kwamba wakati kuna Watanzania wanaishi chini ya dola moja, wapo viongozi wanaoponda raha kwa kutumia fedha na raslimali za umma. Mbaya zaidi wapo hata viongozi wa chama tawala, CCM waliofikia hatua ya kuuza hata nyara za taifa kwa maslahi binafsi.

Hofu hii imeoneshwa pia na wabunge wetu. Wakati wa mkutano wa nne wa Bunge la Bajeti kila mbunge aliyepata nafasi ya kuchangia makadirio ya matumizi ya fedha Wizara ya Ardhi na Makazi, na hata Maliasili na Utalii alisema ikiwa migogoro iliyopo haitashughulikiwa haraka amani inaweza kutoweka.

Baadhi ya wabunge, tena kutoka CCM walitahadharisha kuwa serikali inaatamia bomu la wakati kwa kushindwa kutolea ufumbuzi matatizo mengi hasa ya ardhi.

Kuna mbunge alizungumzia namna wapigakura wake katika wilaya ya Ludewa wanavyohangaika kwa usafiri wa Ziwa Nyasa.

Kuna mbunge, alitiwa mahabusu kwa sababu tu ni wa upinzani na alikuwa akitetea wapigakura wake. Mbunge huyo akaeleza namna wafanyakazi wa Maliasili na Utalii walivyochoma nyuma na mazao za wakazi wilayani Urambo kwa madai eti wako kwenye hifadhi.

Wapo wabunge walioilalamikia serikali kwa kushindwa kutatua migogoro kama vile ya wafugaji na wakulima au ya wanavijiji na wawekezaji.

Dalili za kutoweka amani zimejionesha kwa mapigano kati ya wakulima na wafugaji, wawekezaji na wanakijiji, wawekezaji katika machimbo ya madini na wachimbaji wadogo wadogo.

Wakati wabunge wakililia maisha bora ya Watanzania  zimepatikana taarifa kwamba baadhi ya viongozi wa chama na serikali wanaishi kwa ufisadi, rushwa na kuuza mashirika ya umma huku fedha wakiweka katika akaunti zao, wakitoa vibali vya kuiba na kuuza nyara na wakiingia mikataba ya kujineemesha.

Tunashukuru kwamba Waziri mkuu ameyaona haya sasa wafanyie kazi kuepusha balaa, vurugu, machafuko na vita ya wenyewe kwa wenyewe.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: