Kama mv Bukoba, kama Spice Islander


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 14 September 2011

Printer-friendly version
Uchambuzi
Mv. Spice Islander

NI kilio kilekile. Maisha yameangamia. Yaliyoikumba mv Bukoba ndiyo yameikumba Spice Islander katika Bahari ya Hindi.

Kama kawaida, hakuna mwenye idadi kamili ya waliokuwa katika meli. Hakuna mwenye idadi kamili ya waliopona. Hakuna mwenye idadi kamili ya waliokufa. Hakuna mwenye idadi ya waliohai chini ya meli!

Hakuna kumbukumbu. Ni ulimwengu wa kubahatisha; wa kubabaisha na kujaza pengo pale muhusika anapokumbana na maswali. Taaluma ilikufa zamani. Kila mmoja anakwenda kwa mazoea tu.

Huwa ninakwenda Zanzibar na hata Pemba kwa meli. Watoto wadogo hawatozwi nauli kama wafanyavyo kwenye ndege. Tiketi huwa kwa wakubwa na hivyo vidogo hupakatwa.

Na udogo una maumbile yake. Kama mdogo kwa umri lakini umbo lako kubwa, watakutoza. Utaingia kwenye orodha. Kama mkubwa kidogo kwa umri lakini umri wako ni ule usio na shukrani, basi umepona. Hutozwi.

Watoto wangapi wadogo wa umri ambao walikuwa katika meli hii iliyoanzia Dar es Salaam? Wangapi waliingia kwenye bandari ya Zanzibar. Wangapi? Hutajua idadi yao.

Swali gumu ni hili: Hao ambao hujui idadi yao; ambao hawako kwenye orodha, wako wapi sasa? Jibu la haraka ni kwamba hawakuwepo wa aina hiyo.

Lakini ukitaka kuthibitisha kuwa walikuwemo, chukua kinda aliyesalimika; pata jina lake, nenda kwenye orodha ya waliokuwa melini. Jina lake halimo! Kama unabisha twende pamoja. Halimo!

Hao wote wameteketea. Kuna wanaoitwa “wajanja.” Wamedandia meli. Ama wamelipa kidogo au wamesamehewa kabisa. Wamo ndani ya meli, lakini hawako kwenye orodha. Wako wapi sasa? Huwezi kujua.

Kuna watoto wanakwenda shule. Umri mdogo wa miaka 15 au chini ya hapo. Yawezekana wamelipa nauli kamili inayotakiwa au wamesamehewa na mmoja wa wahusika.

Kama wana hadhi hiyo ya kusamehewa, basi hawawezi kuwa kwenye orodha. Hapa naongea na wasafirio kati ya Dar es Salaam, Zanzibar na Pemba – haya yapo au hayapo? Wako wapi watoto hao?

Sikiliza taarifa za serikali: Waliokufa ni 197. Waliookolewa ni 619. Hawa wanatoka kwenye orodha ipi? Ya wangapi? Ya wali? IPI? Waliobakia chini ni wangapi? Waliopotea – maana kuna uwezekano wa kupotea – ni wangapi?

Ni mambo mlegezo. Ni mazoea. Anayeuliza na anayeulizwa, wote ni sawa. Inafikia wakati watu makini wanauliza: Meli hii ni ya nani hasa? Siyo ya baadhi ya viongozi? Wanajenga shaka. Wana haki.

Katika hili la Spice Islander, ndio maana kuna ndimi nyingi. Taarifa za awali zilisema meli ina uwezo wa kubeba abiria 170 na mizigo. Taarifa za baadaye zikasema ni abiria 600.

Wenzangu hawajachimba – wale wanahabari. Nawaamini. Katika hili hakuna atakayekubali taarifa za juujuu. Ni uhai umepotea. Ni jukumu la wote kujua vipi na kwa nini.

Sasa watoto! Watoto! Taarifa kutoka Nungwi, eneo la ajali, zinasema wengi waliopoteza maisha ni watoto na vikongwe.

Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), juzi Jumatatu lilimuuliza waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan, juu ya mkasa huu na hasa vifo vya watoto.

Dunia nzima ilimsikia mbunge huyo wa Makunduchi akisema kuwa labda itungwe sheria ya kuweka idadi maalum ya watoto ambao kila mtu mzima atatakiwa kusafiri nao ili kukabiliana na vifo vya watoto wengi pale ajali ikitokea.

Huyo ni waziri. Hazungumzii chombo kipya cha usafiri. Hasema ukaguzi wa mara kwa mara wa vyombo vya majini. Hataji umuhimu wa kufuata taratibu, kanuni na sheria za kuendesha vyombo hivi.

Hatumsikii akijadili umuhimu wa maadili ya kazi. Hatusikii lolote juu ya serikali kuona umuhimu wa kuwa na usafiri imara; hata umuhimu wa serikali kuweka meli mpya, ya kisasa kwa walipakodi wa Pemba na Unguja.

Hiyo ni akili ya shuruti. Sheria! Pamoja na kwamba sheria ni muhimu, lakini huwa zina mahali zinasimama. Meli iliyoundwa Ugiriki mwaka 1967, hakika imezeeka.

Uzee huu hauendi kwa sheria za kubeba watoto; inakwenda kwa sheria za taaluma,  ukaguzi, matengenezo, usimamizi, taratibu za kuwa na orodha ya kila mtu anayeingia melini; ajira inayoeleweka na kulindwa.

Shuruti ya kuwa na idadi rasmi ya watoto watatu au wawili wa kusafiri nao, haina mantiki, kwani mzazi aweza kushindwa hata kujiokoa mwenyewe; wote wakafa maji au akafa yeye na wao wakabaki kwa muujiza.

Hilo nalo ni tatizo la fikra mlegezo. Hivi watawala hawaoni, hata kwa macho ya kawaida yasiyo ya kitaaluma, kuwa meli hiyo imezeeka?

Ni kama mv Victoria katika ziwa ambamo mv Bukoba ilizama na kuua zaidi ya watu 1,000. Hili mara lizimike hapa, mara pale! Mara limepelekwa matengenezo ya muda mrefu.

Nalo li-Victoria ni la miaka hiyohiyo ya 1960. Limechoka. Ama litakumbwa na yale ya mv Bukoba au ya Spice Islander. Sitabiri maafa, naagalia mbele kwa kuchambua matendo na nyakati. Tusubiri.

Kwa wanaojua Zanzibar ya Abeid Amani Karume, watakubaliana kuwa ingeendelea kuwa hivyo kiuchumi, meli zilizozeeka zisingekuwa baharini.

Ungemsikia akifoka, “Ebo! unaua watu na kuwavua kwa kokoro kwani wamekuwa dagaa? Leta meli mpya!” 
Angeshangaa kutu iliyozunguka “kiuno” cha Spice Islander. Angeuliza kama inabeba abiria 600, inakuwaje na maboya ya kuokoa 200 tu? Angesema, nami namkumbuka sana, “Ebo, hawa wengine 400 watajiokoaje?”

Ukora ungejulikana. Utapeli ungeanikwa. Wahusika wangetawanyika kabla ya kutawanywa; au kazi ingefanywa kwa ustadi.

Ingawa utawala wa mtu mmoja hauna nafasi tena, kwa kuwa leo tunataka mfumo wa uendeshaji; lakini kuwa na mwenye dira kunaokoa mengi kuliko kusema tuna mfumo lakini hauendi; au umeonza.

Roho za walioangamia majini Nungwi zilale mahali zinapostahili. Ndipo tuone wanasiasa wakiimba rambirambi na kujenga minara ya kumbukumbu isiyoleta mabadiliko. Tusubiri.

0713 614872, ndimara@yahoo.com, www.ndimara.blogspot.com
0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)