Kama serikali ni sikivu basi irekebishe Katiba


editor's picture

Na editor - Imechapwa 24 November 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KILA waziri anaposimama bungeni kujibu hoja au malalamiko ya wabunge kuhusu shida zinazowakabili wananchi wanaowawakilisha, husikika akisema, “serikali yenu hii ni sikivu sana hivyo itafuatilia kwa karibu kwa lengo la kupaa ufumbuzi”.

Hata viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nao huimba wimbo huo huo kuonyesha kwamba serikali inayoundwa na chama chao ni sikivu kwa mapendekezo ya wananchi kupitia wabunge.

Pamoja na kuimba wimbo huu katika kila kikao cha Bunge au katika majukwaa ya kisiasa, serikali imeziba masikio isisiki kilio cha muda mrefu cha wananchi wake juu ya haja ya kurekebisha Katiba na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Hata serikali za nchi rafiki kama Rais Barack Obama wa Marekani, alipoingia madarakani alisema Marekani ni ya Wamarekani wote.

Alisema yanahitajika mabadiliko na akasema katika uongozi wake atawasikiliza Wamarekani hasa pale wanapotofautiana naye.

Mfano huo unafaa kuigwa na serikali ya Rais Jakaya Kikwete, rais wa Watanzania wote, kwamba anapaswa kuwasikiliza pale anapotofautiana nao ili afanye marekebisho kwa masilahi ya Watanzania.

Mpaka sasa tunajua kimsimamo serikali inatofautiana na wananchi kuhusu suala la Katiba na uundwaji wa NEC.

Hivyo, huu ndio wakati wa kusikiliza mapendekezo ya wananchi yanayolenga kuboresha misingi ya utawala bora na demokrasia; serikali ikae ijadiliane na kufanya marekebisho.

Mapendekezo ya Watanzania yamewasilishwa kupitia ama vyama vya siasa au taasisi zisizo za kiserikali au watu binafsi, wasomi na wataalamu mbalimbali wakiwemo wana CCM wenyewe.

Kwa hiyo kama kweli serikali hii ina rais msikivu kama inavyodaiwa, hatuoni kwa sababu gani anakataa kufanya mabadiliko. Hatuoni kwa nini serikali inadai ni sikivu huku ikitia pamba isisikie kilio hiki.

Watanzania wanataka katiba mpya kwa sababu iliyopo ni ya zamani na haikidhi kamwe kwa wakati uliopo. Katiba iliyyopo ilitungwa mwaka 1977 enzi za mfumo wa chama kimoja, na imewekwa viraka vingi kwa utashi wa watawala badala ya wananchi wenyewe.

Watanzania wanataka katiba mpya kwa vile wamechoka kuendelea kutumia katiba inayokejeli utu na uhuru wao na inayowarudisha nyuma na kung’ang’aniza utawala mbaya. Ndiyo maana tunasema kama serikali ni sikivu
basi irekebishe Katiba.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: