Kama na yeye hajui, nani atajua?


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 09 February 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

IMERIPOTIWA kwamba Rais Jayaka Kikwete amesema naye hajui ni nani wamiliki wa kampuni ya Dowans. Kikwete hakusema tu kuwa haijui, lakini alisema jambo jingine linalotatiza wengi.

Alisema, “Sina uhusiano wowote wa kimaslahi, kwa namna yoyote ile na kampuni ya Dowans; siwajui, sijawahi kukutana nao na hawana ya sababu kukutana na mimi kwa sababu hawanihitaji.” 

Kauli hii na nyingine imenifanya nijiulize maswali kadhaa: Kwanza, sitaki kushuku kuwa Rais Kikwete hakusema kweli, hivyo ninakubali kabisa kuwa rais hawajui na hajawahi kukutana na Dowans na wala wao hawakuwa na sababu ya kukutana naye.

Kwa maneno mengine, Rais Kikwete hawajui wamiliki wake, hajui wahusika wake au maafisa wake na kuwa hajafanya jitihada yoyote ya kuwajua – ndio maana hawajui.

Sasa swali kubwa ambalo limenikabili ni kwamba ni kwa nini hawajui? Yaani, kwa nini rais wa Jamhuri aliyeapishwa kulinda na kutetea utawala wa sheria, hajachukua muda kutaka kujua ni kina nani walio nyuma ya kampuni inayotaka kufua nishati nchini?

Kwanini katika wingu lote la tuhuma za ufisadi kuanzia wakati wa Richmond hadi kurithishana mkataba kinyemela, rais wa jamhuri hajakaa chini kutaka kujua ni nani walio nyuma ya kampuni ya Dowans?

Lakini katika kujiuliza swali hilo kubwa nikajikuta nakaribisha maswali mengine. Moja kwa mfano, ni kweli kwamba rais Kikwete hajali kuwa ni kampuni gani inajiingiza katika sekta ya nishati nchini – moja ya sekta nyeti kiusalama na kiuchumi katika taifa?

Je, kama kampuni hiyo ni genge la wahalifu kutoka kundi la mafia kutoka Italia au Urusi ambao wamefanya  uhalifu na njama ya kuingia kwa mradi wa kuzalisha nishati, rais Kikwete yeye hajali?

Itakuwaje kama ni genge la mafia wa Kitanzania ambao wakitumia uzoefu na mahusiano yao na wanasiasa na wafanyabiashara ndani na nje waliweza kujiingiza kwenye mradi huo na kuwapiga kumbo watu wengine?

Pili, Rais Kikwete hajashtushwa na uanzishaji wa makampuni feki ndani na nje ya nchi ambayo yamejiingiza kwenye biashara mbalimbali kwa kuhusiana na watendaji serikalini na hadi bungeni?

Mathalani miradi ya kampuni ya kitapeli ya Deep Green Finance Limited, Tangold Limited na Meremeta – makampuni ambayo yaliundwa maalum kuchota maliasili ya taifa na mengine kuchota fedha za umma ndani ya Benki Kuu (BoT) na serikalini na baadaye yakatoweka kama ukungu.

Je, rais Kikwete hajafikiria kuwa Dowans ni mojawapo ya makampuni ya aina hiyo? Hivi, kwa mfano, serikali ikilipa hizo Sh. 94 bilioni (baada ya kushindwa kutafuta mbinu za kuzuia malipo) halafu kampuni ya Dowans Tanzania Limited ikaamua kufunga shughuli zake na kutoweka, kama ilivyofanya Deep Green Finance, Rais Kikwete anaweza kusema “imetokea kwa bahati mbaya?” Au atakuja kusema “sikujua?” 

Kampuni ya Deep Green Finance ilipokea zaidi ya Sh.100 bilioni ndani ya mwezi mmmoja na kisha kuhamisha fedha hizo kwenda akaunti nyingine na kisha kampuni hiyo ikaamua kujifilisi na kufunga biashara zake.

Licha ya viongozi wa upinzani wakiongozwa na katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibord Slaa kuhoji uhalali wa kampuni hiyo, hadi leo takribani miaka mitano, serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya rais Kikwete haijawa na ujasiri wa kuwaambia wananchi kwanini kampuni hiyo ipokea fedha hizo.

Na akiulizwa leo, nani walikuwa hasa wamiliki wa Deep Green, jibu lake naweza kulikisia. Atasema hajafanya jitihada ya kujua yaliyotokea. Ninawahakikishia chini ya nyota za mbingu, Dowans wakilipwa watatokomea kama Deep Green Finance na hakuna atakayekuwa na ujasiri wa kukiri kilichotokea.

Nikajiuliza swali jingine kuwa ni kwanini Rais Kikwete hataki na hajajaribu kujua wamilimi wa kampuni ya Dowans au undani wake wa kampuni hiyo?

Kwamba wakati wananchi wanalalamika toka mwanzo, tangu mchakato unaanza wa kurithishana mkataba kinyume cha sheria rais Kikwete anasema hakujaribu kujua nani wako nyuma ya Dowans!

Kwenye maelezo yake, Jumamosi iliyopita, rais alitudokeza alichokifanya kuhusiana na kuzuia malipo ya Richmond (japo hakutaka kujua ni kina nani). Lakini hajatuambia alifanya nini kuzuia kampuni ya Dowans isirithishwe mkataba nyuma ya mgongo wa TANESCO kama ilivyofanyika?

Rais Kikwete amesema kuwa hawajui wamiliki wa Dowans na hajawahi kukutana na wao hawana sababu ya kukutana na yeye. Hivi, amewahi kujaribu kumwita Rostam Aziz na kumuuliza “eeh bwana hivi hawa Dowans uliowaleta humu nchini ni kina nani hasa? Hivi hili ni swali gumu kwa rais kuuliza?

Jambo la mwisho ambalo nimebakia kushangaa ni kuwa Rais Kikwete kama baadhi ya viongozi wa CCM na serikali, wanafikiri tunamatatizo na malipo ya Dowans kwa sababu ya “kiasi” chake.

Kwamba tunatatizwa na malipo ya bilioni 94! Kwamba hizo ni “fedha nyingi sana.” Si kweli. Hatuna tatizo na Dowans kulipwa Sh. 94 bilioni, ama Sh. 200 bilioni. Tatizo ni uhalali wa malipo yenyewe. Hata kama watalipwa Sh. 10 bilioni, bado tutapinga malipo hayo.

Inakuwaje majenereta yenye kugharimu chini dola 60 milioni yaje kutugharimu mwisho wa siku zaidi ya bilioni 200 halafu bado majenereta yenyewe siyo ya kwetu?

Lakini zaidi ni kuwa ilikuwaje kampuni ivunje sheria katika kupeana mkataba na Richmond bila kuitaarifu TANESCO na sisi katika utimamu wetu tukubali ati kwa vile wametupatia umeme (ambao tulilipia) basi tuwalipe tu yaishe?

Kuna imani ambayo inataka kujengwa kuwa Dowans hawajalipwa hela yoyote na kuwa wameshinda “kesi” na sasa tuwalipe kwani tusipowalipa tumewadhulumu.

Wanachofanya ni kutaka tujisikie “vibaya” kwamba tukipinga malipo ya Dowan,s basi tunawaonea hao Dowans “kwa sababu tumetumia umeme wao”.

Nashangazwa na fikra za namna hiyo. Tunachohoji ni mkataba wenyewe kutokuwa halali; siyo sababu zilizotolewa na TANESCO kule ICC kwamba siyo halali kwa kuwa Richmond ni kampuni hewa. La hasha!

Si halali kwa kuwa kitendo cha Richmond kuwarithisha Dowans mkataba bila kupata idhini ya kimaandishi kutoka TANESCO ilikuwa ni kosa ambalo lilifanya mkataba uliorithiwa usiwe halali.

Uhalali wa mkataba haukuwa katika kutoa huduma, bali ni uhalali wa yule anayetoa huduma. Hivi kampuni inaweza kuja na kujiunganisha umeme kwenye gridi bila kuwa na mkataba, halafu ikatudai na sisi tukakubali kulipa kwa sababu ati tumetumia “umeme wao?”

Hata hawa viongozi waliojitokeza na kusema malipo hayaepukiki, kwa sababu ni sheria. Je, hiyo sheria inafuatwa katika kulipa Dowans tu, au na wengine?

Kwanini tunang’ang’ania sheria inayowafaa wao, lakini hatutaki kutumia sheria kutufaa sisi?

Inafahamika kwamba kisheria, mwanasheria mkuu anaweza kuingilia kesi yoyote katika Jamhuri ya Muungano endapo ataiona kwa kufanya hivyo itakuwa ni kwa maslahi ya taifa.

Naomba nitoe changamoto; kama kweli Kikwete naye hataki Dowans walipwe, basi mwanasheria mkuu wa serikali ajiunge kwenye kesi ya wanaharakati kutoa nguvu zaidi na atoe msaada wote wa kisheria.

Vinginevyo, kila mmoja atasema “hatujui kama rais alituambia ukweli wote;” kama yeye hajui anayotakiwa kujua, basi hakuna anaweza kujua.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: