Kamanda Kova na igizo tata


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version
Wazo Mbadala
Kamanda  wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova

WEZI wana mbinu moja kubwa. Katika maandalizi yao ya kuiba huwa wanabeba mifupa ya kuku kwa ajili ya kuwarushia mbwa.

Basi, wakifika mahali walipopanga kuiba au kupora, wakikurupushwa na mbwa baada kufanikisha wizi au kabla ya kuiba, humwaga mifupa ili wabaki wanatafuna wakati wao wanatokomea.

Tukio la wizi likifanyika mchana, wezi hurusha fedha – nyekundunyekundu tupu – ili vijana wanaowakimbiza wachelewe wakigombania kuokota noti hizo, huku wezi wakitoweka.

Mbinu hizo zimemvutia saaaaaana Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akaamua kuzitengenezea igizo fupi la kilaghai la Mtuhumiwa wa Kumteka na Kumtesa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka.

Kova akatafuta wahusika wawili wakuu – mchungaji kiongozi, Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la Kawe, na mlokole feki raia wa Kenya Joshua Gitu Mhindi (31).

Kova akajiridhisha na wahusika hao na kisa chenyewe, akazima taa ofisini, akacheza igizo lake akafurahia – akamwona kifikra Gwajima akimwombea Mhindi atubu dhambi.

Haraka Kova akawaita waandishi wa habari kichwani akiamini igizo hilo lenye utata, litafifisha udadisi wa Watanzania juu ya ushiriki wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika tukio la kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka.

Kamera zilipojaa ofisini kwake, huku akipigwa picha kila upande ili lisikike kila neno analotamka, akabwaga mifupa ya kuku wake eti we’ ve got him yaani wamemnasa.

Waandishi wa habari wakamhoji, “Nani?” Kova akafuta miwani yake, akasetaseta, akasimama wima akaeleza eti polisi wamemtia mbaroni aliyeshiriki kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka, akamtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Joshua Gitu Mhindi (31) raia wa Kenya.

Kova alidai kwamba Mhindi alinaswa kanisani hapo alipokuwa anatubu. Tangu Ijumaa Kova alipolisingizia kanisa, Watanzania wamekataa kula mifupa au kuamini igizo hilo.

Kwa bahati mbaya, hata Gwajima amekana kushiriki katika igizo hilo. Amesema hakumpokea mtu yeyote wala kumshuhudia akieleza yooooote ya moyoni wakati wa toba na ushuhuda.

Sasa Kova amepata wapi habari hizi? Amezusha siyo? Uzushi huu wa Kamanda Kova unachochea madai na kelele za wanasiasa, wanaharakati na wananchi kwa ujumla kwamba inahitajika TUME HURU kuchunguza sakata hili.

Uzushi huu wa Kova ni kielelezo kwamba Jeshi la Polisi halina nia njema ya kuchunguza ukweli wa tukio hilo. Vilevile ni kielelezo kuwa limeishiwa mbinu siyo za kuchunguza tu, bali hata za kudanganya.

Kova amechelewa kurusha mifupa yake na hawezi kutuondoa katika imani kwamba SERIKALI ya CCM imehusika.

Kova anapoibuka na mbinu za kitoto katika sakata hili zito ajue hatudanganyiki ng’o. Badala ya kudanganya eti aliyemtesa Dk. Ulimboka ameokoka Serikali ijitakase, ikiri, iokoke.

Jambo zuri ni kwamba hata huyo mlokole feki wa Kova anadai wako 12 na walitumwa na ofisa wa serikali; na katika ushuhuda wake wa awali katika hospitali ya taifa ya Muhimbili kitengo cha mifupa MOI, Dk. Ulimboka mwenyewe alisema aliyetengeneza mpango wa kutekwa kwake na hatimaye kuteswa ni ofisa wa ikulu.

Kova atutegulie kitendawili hiki. Mlokole feki anadai walifadhiliwa na ofisa wa serikali, Dk. Ulimboka anadai ni ofisa anayemjua vema kutoka ikulu; Dk. Deo Michael ambaye ni rafiki yake Dk. Ulimboka anamtaja kwa jina ofisa huyo kutoka ikulu kuwa ni Abeid.

Mchungaji amemwambia Kova aache maigizo serikali iunde tume huru kuondoa utata.

0658 383 979
0
Your rating: None Average: 4.3 (4 votes)