Kamanda wa polisi huyu si wa Tanzania


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 30 May 2012

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki
Kamishna Msaidizi Mwandamizi  wa Polisi, (SACP), Simon Siro

MKUU wa Operesheni Maalum za Jeshi la Polisi Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, (SACP), Simon Siro, labda si Mtanzania. Nina maana anaweza kuwa raia wa kigeni. Nitaeleza.

Kwa vitendo vyake na kwa kauli zake, SACP Siro si raia kabisa au kwa maneno mengine si polisi wa Tanzania. Haiwezekani askari Polisi Mtanzania tena mwenye cheo kikubwa kama cha Kamishna akaliaibisha na kulidhalilisha Jeshi la Polisi kwa namna alivyofanya Kamanda Siro.

Akiwa mji mdogo wa Ikwiriri wilayani Rufiji katika mkoa wa Pwani, wiki iliyopita, Kamanda Siro, alifanya yale ambayo askari Mtanzania aliyehitimu ukuruta katika chuo maarufu cha Polisi Moshi (CCP) hawezi kuyafanya wala kufikiria kuyafanya.

Nimesoma kwenye vyombo vya habari na kushuhudia Kamanda Siro akisema kwamba askari wa Kituo cha Ikwiriri walikosea na kwamba ndio chanzo cha vurugu zilizohusisha mapigano ya wakulima na wafugaji!

Gazeti moja liliandika: “Lakini hali hiyo tete ilibadilika ghafla jana (Jumanne wiki iliyopita) wakati Mkuu wa Operesheni Maalumu za Jeshi la Polisi nchini, Simon Siro, alipotumia busara na kuingilia kati siyo tu kwa kuamuru kuachiwa kwa watuhumiwa hao, bali pia kuwalaumu polisi na kusema wao ndio wamekuwa chanzo cha tatizo kutokana na kuwapendelea wafugaji. Hatua hiyo ndiyo iliyorejesha amani na utulivu katika eneo hilo.”

Hapa nilipo nahema kwa hasira. Kamanda anayeongoza kikosi cha Polisi wa Fanya Fujo Uone (FFU), anawagwaya wakulima? Kamanda mkubwa wa Polisi anawanyenyekea wakulima badala ya kuwapiga mikanda, kuwakanyaga mateke ili wakome kulalama na wawaogope Polisi!

Kamanda gani huyu? Ama kweli Jeshi la Polisi nalo limeingiliwa. Nchi yetu sasa ipo hoi bin taaban. Tunakotoka, tunakokwenda, hatukujui, tunakwenda hobelahobela tu.

Zamani watu walisema uandishi wa habari umeingiliwa na makanjanja; wahandisi nao wameingiliwa na sasa wanajenga barabara inabomoka kesho yake; wanasiasa wameingiliwa sasa hawajui kudanganya ndiyo maana wanafukuzwa kazi kwa wizi; wao wanadai wameonewa na kuandaa maandamano ya kuwapokea.

Hata mashushushu nao wameingiliwa, tofauti na zamani. Waliopo sasa hawajifichi; hebu fikiria shushushu wa chama fulani anapomwalika Mwenyekiti wa chama kingine kuja kuwa mpambe wake atakapoomba urais kupitia chama chake! Si kila mtu atamgundua kuwa ni shushushu aliyetumwa kukiangamiza chama hiki?

Na tuache haya ya kuingiliwa kwa sababu hata mameya nao wameingiliwa na sasa wanafikiri kwa namna tofauti sana kwa kutumia kiungo nyeti anachokifahamu mwenzao wa Jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi, peke yake.

Turudi kwa Kamanda Siro, polisi mwoga anayetofautiana na makamanda wenzake na askari wenzake. Tabia ya Kamanda Siro itafanya raia wasiwaogope polisi tena na hii ni hatari sana kwa jeshi letu la Polisi.

Sisi Watanzania tumezoea na tunawapenda polisi na makamanda wa Polisi katili, wanaopiga raia ili kuwanyoosha waweze kutawalika vema. Tunataka makamanda wa polisi kama Venance Tossi aliyewanyoosha watuhumiwa wa ujangili.

Tumezoea makamanda wa Polisi kama Michael Kamhanda wa Mkoa wa Ruvuma, aliyewakomesha wakazi wa Songea wakakoma kabisa hadi leo hatusikii maandamano wala mikutano ya kupinga mauaji ya kishenzi mkoani humo.

Tunataka Polisi kama Kamanda Andengenye wa Arusha na IGP Said Mwema wenye intelijensia kali na uwezo wa kupiga marufuku maandamano na kutawanya mikutano ya wabishi wanaotumia kisingizio cha siasa za upinzani.

Hatujamsahau kiboko ya njia, Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Kamishna Paul Chagonja. Huyu ndiye aliyetumwa na IGP Mwema kuongoza maofisa kutoka Makao Makuu ya Polisi kwenda Songea kufanya uchunguzi wa ghasia hizo.

Tunataka makamanda kama Chagonja aliyeshirikiana vema na wenzake wakawatwanga wakazi wa Nyamongo, wakaua sita au saba hivi na walipoendelea kuleta vurugu wakipewa kichwa na CHADEMA wakatupa maiti barabarani na kuyatelekeza huko. Tarime na Nyamongo wakanyooka hadi leo.

Viongozi kadhaa wa CHADEMA wakiwamo wabunge Esther Matiko na Tundu Lissu, walipoleta za kuleta, nao wakaswekwa ndani na kufunguliwa mashitaka na hadi leo kesi ipo mahakamani. Yes, tunataka makamanda wa Polisi kama hawa.

Yeye Kamanda Siro analeta lele mama? Hakuna kukamata wala kusweka ndani? Eti leo anasamehe na kuamuru wakulima 53 wakorofi wa Ikwiriri waliokamatwa kwa kudiriki kupiga wafugaji wa Kimasai na Kisukuma. Wakulima watawapa Polisi nini hadi wanasikilizwa na Kamanda Siro?

Wafugaji wanawanunulia askari wa Polisi saa, simu, redio, televisheni, nyama kilo mbilimbili, maziwa kwa bili chupa moja kila askari na hivyo watoto wa askari hawapati kwashiorkor na hata nauli wafugaji wanawalipia askari kwenda Utete na Dar es Salaam! Leo watu wanaobughudhi wafugaji wanaachiwa?

Hapana, huu si utamaduni wetu Watanzania. Kamanda Siro achunguzwe uraia wake isije ikawa ni Mrundi, Mkongo, Mmalawi, Mzambia au Mnyarwanda.

Haiwezekani Kamanda wa Polisi wa Tanzania aliyeiva hasa mafunzo ya ukakamavu, aonyeshe ulegelege kama huyu Kamanda Siro.

Kule kwetu nilikozaliwa, polisi hasa tunawafahamu. Kwa upande wa Kenya wanaitwa “machoni’ au kwa jina lao maarufu la GSU au General Service Unit.

Hawa ndio wanaokaribia kulingana na askari wa kwetu FFU – Fanya Fujo Uone. Hawa FFU kule kwetu tunawaita “motoroisi” nasikia Kingereza chake ni Motorized Police.

Kwetu hatujui FFU bali tunajua “motoroisi” ambao wakiingia kijijini au kufika kwako, hutasikia wanapiga hodi, bali utasikia mbwa akilia kapigwa teke, kuku wanaruka na kilio juu, paka na mbuzi hata kondoo wakikanyagwa mabuti na kupigwa mikanda. Hao ndio askari wanaoogopwa Ukuryani.

Mliona askari wale waliokuwa wakipiga raia Zanzibar hadi wakaua zaidi ya 20 na wengine wanasema waliouawa ni karibu 100. Wale askari waliokuwa wanapiga raia na wakimkosa wanakanyaga baiskeli yake! Hamkuona kwenye video? Wale ndio askari wetu Tanzania. Siro siye.

Hivi Kamanda Siro anayefyata mkia kwa Wandengereko atafanya kazi mkoani Mara kweli? Mie napendekeza avuliwe madaraka maana ameonyesha udhaifu mkubwa. Hatutaki askari narenare katika kipindi hiki cha mabadiliko makubwa huku raia wakikiasi chama tawala.

Sasa raia wanaikimbia CCM na Polisi nao, tena Kamanda mkubwa anatetemeka na kuonyesha woga kwenye eneo la tukio na anarudi nyuma eti anawalaumu Polisi wake kuwa ndio chanzo cha vurugu? Kamanda gani huyu, haraka fukuzilia mbali kabla mambo hayajaharibika.

Bila hivyo Polisi watakosa heshima.

0
No votes yet