Kamati Kuu ina busara kuliko wabunge wa CCM


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 10 August 2011

Printer-friendly version
Kamati Kuu ya CCM

MWALIMU Julius Nyerere aliwashangaa wananchi, baadhi yao wanachama wa CCM waliosema 1+1=3. Hesabu hiyo ilihusu muundo wa muungano.

Hakuielewa hesabu hiyo kwamba ukiunganisha serikali ya Tanganyika na ile ya Zanzibar unapata serikali tatu badala ya mbili. Alihoji, “1+1=2 hii 3 inatoka wapi?”

Kwa nujibu wa sera ya CCM, muungano wa Tanzania ni wa serikali mbili – Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ). Mwalimu Nyerere alitetea sera hii akipinga vikali waliotaka serikali tatu yaani ya Tanganyika, SMZ na Serikali ya Muungano.

Mpaka sasa katika suala hili na hata mjadala kuhusu uundaji wa Katiba mpya ya Jamhuri, umejikita katika hesabu ya 1+1=2 au 1+1=3 na wachache wasiokubalika sana 1+1=1 yaani ibaki serikali moja tu ya muungano.

Angekuwa hai leo, Mwalimu Nyerere angeshangaa vijana aliowaachia madaraka wakihangaika kujua kama 10 – 4 =14 au ni 6.

Kwamba baada ya serikali kupunguza ushuru wa mafuta kwa lengo la kupunguza bei, imepanda badala yake na serikali imekaa kimya.

Alipokuwa anawasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2011/2012 bungeni Juni 8, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo alisema serikali itapunguza ushuru katika bidhaa za mafuta ya petroli ili bei vituoni ipungue, na pia itapandisha ushuru wa mafuta ya taa ili kuzuia uchakachuaji.

Uchakachuaji kwa mafuta ni mtindo wa kuyachanganya mafuta ya taa na yale ya petroli kama mbinu ya kukwepa ushuru.

Wabunge wenye muono wa mbali, hasa wapinzani waliotumwa na wapigakura kwenda kuwatetea bungeni, walipinga mipango ya serikali kupandisha bei ya mafuta ya taa wakisema kufanya hivyo ni kuumiza wananchi maskini.

Serikali kiziwi ya CCM na wabunge wake wanaojiita “mawaziri tarajiwa” wakakejeli utetezi huo. Wabunge wa CCM ambao wengi wao hutwanga usingizi hadi kukoroma walishangilia kupitishwa bajeti iliyolenga kumwongezea mzigo mwananchi maskini.

Wabunge waliokejeli hoja za upinzani ni pamoja na Mwigullu Nchemba anayewakilisha jimbo la uchaguzi la Iramba Magharibi. Huyu kwa bahati pia ndiye Katibu wa Idara ya Uchumi na Fedha wa CCM.

Mwigullu aliponda bajeti mbadala ya kambi ya upinzani iliyopinga upandishaji ushuru wa mafuta ya taaa, huku akitetea kila kilichopendekezwa na serikali.

Tatizo la wana-CCM ni kufuata falsafa ya enzi za vita baridi kwamba “adui yako hata akikwambia jambo jema usilikubali.” Hofu yao kubwa ilikuwa kwamba jambo hilo jema linaweza kuwa mtego.

Wakati wabunge wa CCM wanatetea kupanda bei ya mafuta ya taa, wakitumia falsafa hiyo, hadi Mei, mwaka huu, bei ya mafuta kwenye vituo vya nchini ilikuwa kati ya Sh. 1,900 na Sh. 2,300.

Alipofuatwa na waandishi wa habari aeleze sababu za kupanda kwa kasi kwa bei hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Haruna Masebu alisema kulitokana na kushuka kwa thamani ya shilingi ikilinganishwa na dola ya Marekani.

“Tatizo hili halipo kwetu kama mamlaka, ila linatokana na kushuka kwa shilingi yetu na kupanda kwa dola ya Marekani; na kazi yetu kubwa ni kuhakikisha tunatoa bei elekezi kila mara ili kuondoa usumbufu kwa wananchi hasa kuhusu bidhaa za mafuta,” alisema Masebu.

Kipindi hicho, dola moja ya Marekani ilikuwa sawa na Sh. 1,550.90. Leo dola ni takribani sawa na Sh. 1,600.

Juni 8, 2011, Ewura ikatoa bei elekezi kurasimisha bei iliyokuwa sokoni. Bei ya chini ya petroli kwa Dar es Salaam ikawa Sh. 2,015 na ukomo wa juu Sh. 2,016. Dizeli ilikuwa kati ya Sh. 2,005 na Sh. 2,155 wakati mafuta ya taa yalikuwa kati ya Sh. 1,558 na 1,674.

Karagwe ambako bei ndiyo ya juu zaidi nchini, viwango vilikuwa Sh. 2,246 – 2,415 (petroli); Sh. 2,236 – 2,404 (dizeli) na mafuta ya taa Sh. 1,789 – 1,923.

Ilipofika 28 Juni, Masebu alikutana na wadau wa mafuta jijini Dar es Salaam akawaambia kuanzia Julai mosi bei za petroli na dizeli zitashuka na mafuta ya taa itapanda.

Alisema bei ya dizeli itapungua kwa Sh. 215 kwa lita. Vilevile alisema mafuta ya taa yatapanda kwa Sh. 385 na kuanzia Agosti mosi, bei ya mafuta hayo itashuka zaidi ili kutoa nafuu kwa mtumiaji.

“Lengo la mkutano wa leo (Juni 28) ni kuwaeleza wadau wa mafuta kuhusu mambo yaliyotokea Dodoma, ambayo yamesababisha sisi Ewura kama wadhibiti, kuwatangazia kuwa kutokana na punguzo la kodi katika mafuta na nyongeza katika mafuta ya taa, bei mpya ya bidhaa hizo itaanza rasmi Julai mosi,” alisema Masebu.

Kilichokuwa kinasubiriwa ni kusainiwa kwa Sheria ya Fedha inayotambua makubaliano hayo yaliyopitishwa na Bunge. Pamoja na kupanda kwa bei ya mafuta ya taa Masebu alisema yatakuwa chini kwa Sh. 15 ya bei ya dizeli.

Kauli yake inatokana na kauli ya Waziri Mkulo aliyesema kuwa katika jitihada za serikali za kupunguza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi, imeamua kupunguza baadhi ya kodi za mafuta ili bei ya bidhaa hiyo ipungue.

Halafu Naibu wake, Pereira Ame Silima aliwasilisha bungeni muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2011, akisema Serikali imeongeza ushuru wa bidhaa kwa mafuta ya taa kutoka Sh. 52 hadi Sh. 400.30 pamoja na mambo mengine, lengo likiwa ni kudhibiti uchakachuaji wa mafuta nchini.

Kilichoshuhudiwa kuanzia Julai mosi baada ya kutiwa saini Muswada wa Fedha na kuwa sheria, ni kupanda kwa kasi bei ya bidhaa hiyo badala ya kushuka kama ilivyoelezwa na serikali.

Wananchi wakapiga kelele. Maskini wakalia na watetezi wa wananchi wakatoa angalizo. Si Ewura wala serikali iliyosikiliza vilio hivyo.

Wizara ya Nishati na Madini ambayo ingejitosa kueleza sababu zake, imegubikwa na kashfa ya watendaji wake kuhonga baadhi ya wabunge ili wapitishe bajeti mbovu.

Hapo ndipo Kamati Kuu (CC) ya CCM yenye wajumbe 30, wakiwemo marais wastaafu wenye busara, hekima na msimamo, ikarekebisha hesabu za serikali 10 – 4 =6 na siyo 14 yaani ukipunguza ushuru bei ya bidhaa lazima ishuke.

Kamati Kuu, chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete, aliyeridhia bajeti ya Mkulo, ikaeleza kutoridhishwa na sababu za kuongeza bei ya mafuta ya taa ili kupambana na uchakachuaji.

Hapo ndipo Ewura ikafufuka na kutangaza bei elekezi ikisema kiwango cha juu kwa petroli jijini Dar es Salaam ni Sh. 2,004; dizeli Sh. 1,911 na mafuta ya taa Sh. 1,905.

Mtiririko huu unaonyesha kama Ewura imepokea maelekezo kutoka CCM. Sasa kwanini ishindwe mwezi mzima ila iweze kupunguza baada ya tamko la CC?

Wajumbe 30 wa CC wana busara kuliko wabunge 250 wa CCM? Au Ewura imetumika kukidhi masuala ya kisiasa kuelekea ‘Iii-igu gugugugunga?’

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: