Kamati Maalum UVCCM: Itashughulikia uhai au msiba?


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 23 March 2011

Printer-friendly version

BARAZA Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM), limeunda kile kinachoitwa, “Kamati maalumu ya kujivua gamba,” ili kushughulikia uhai wa umoja huo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, ni Hussein Bashe, mjumbe wa baraza kupitia mkoa wa Tabora.

Wengine wanaounda kamati hiyo, ni mwenyeviti wa umoja huo mkoani Dodoma, Anthony Mavunde, mwenyekiti wa UV-CCM mkoani Tanga, Rogers Shemwelekwa na mwenyekiti wa UV-CCM mkoani Iringa, Fadhili Ngajilo.

Wengine ni Riziki Pemba, Daudi Ismail, Ashura Seng’ondo na Zuberi Bundara.

Pamoja na mambo mengine, “kamati ya kujivua gamba” imepanga kukutana na watu mbalimbali ili kupata maoni yao juu ya namna gani jumuiya hiyo inaweza kurudisha heshima yake iliyokuwa nayo huko nyuma. Kazi ya kamati hii inatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutangazwa, Bashe alisema kamati yake itakutana na makundi mbalimbali likiwamo Jukwaa la Wahariri wa vyombo vya habari.

Hata hivyo, hatua ya UV-CCM kuunda kamati ya kushughulikia uhai wake katika kipindi hiki ambacho chama kimegeuka kuwa genge la watu wachache, ni sawa na mwanadada kumeza vidonge vya mpango wa uzazi wakati mimba imeishatungwa na tayari mtoto anakaribia kuzaliwa.

Kwa hali ilivyo ndani ya chama hiki na jumuia zake, huwezi kukiokoa kwa kuunda kamati za kushutikiza. Kunahitajika mkakati madhubuti unaoweza kukiokoa chama hiki kutoka hapa kilipo sasa.

CCM tayari kimepoteza mwelekeo wake kitambo kilichopita, kutokana na hatua yake ya kukumbatia mtindo unaowanyanganya wanachama mamlaka ya chama chao na kukibakiza kuwa chama cha viongozi.

Mtindo huu ukarithiwa na jumuia zote na kuenea katika matawi yote ya CCM nchini. UV-CCM yenyewe ndiyo iliyoanza kutumika kama chombo cha kutelekeza maadili mema ya chama pale ilipojipa udalali wa kugawa rushwa katika uchaguzi na kuchafua wagombea wasiokuwa na fedha za kuwahonga wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi kumalizika. 

Walipomaliza kazi hiyo ndani ya chama, wakatumia mtindo huohuo ndani ya jumuia yao wenyewe. Tangu enzi za awamu ya uongozi wa Emmanuel Nchimbi, uongozi wa jumuia ya vijana unakuwa ni ama wa kununuliwa kwa fedha, vyeo au hata kwa ngono.

Haishangazi mpaka leo, viongozi wakuu wote wa jumuia hii wana kambi zao mfukoni na wanapigana kufa na kupona kuzitetea katika vikao.

Kwa mfano, unapomteua Bashe kuwa mwenyekiti wa kamati ya “kujivua gamba” unategemea nini?

Kwanza, Bashe ni mwajiriwa wa New Habari Corporation Limited, kampuni inayomilikiwa na Rostam Aziz, mbunge wa Igunga na mfanyabiashara ambaye amekuwa mwiba kwa CCM na serikali yake.

Bashe hawezi kukubaliana na hoja itakayotolewa na wanachama wenzake wanaotaka Rostam Aziz aenguliwe kutoka kwenye chama hata kama ataona wazi kuwa hiyo ndiyo njia sahihi ya kukiokoa chama hicho.

Hili linathibitishwa hata na kauli zake ndani ya mkutano wa baraza la vijana uliomchagua yeye kuwa mwenyekiti wa kamati.

Kila sekunde aliyoipata kuzungumza, Bashe aliitumia kumtetea Edward Lowassa –  aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond na swahiba wake Rostam Aziz, na kushambulia aliyekuwa spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta na mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba tata wa Richmond, Dk. Harrison Mwakyembe.

Pili, ni Bashe huyuhuyu ambaye CCM ilimwengua katika kinyanganyiro cha kugombea ubunge katika jimbo la Nzega kwa madai kuwa si raia wa Tanzania, bali wa Somalia. Ni huyu ambaye chama kimemkabidhi jukumu hilo kubwa.

Katika hali ya kushangaza, wajumbe akiwamo katibu mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba walinyamazia msimamo wa chama na kauli ya Katibu Mwenezi John Chiligati aliyetoa taarifa mbele ya vyombo vya habari, na akaungwa mkono na mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete pale Mnazi mmoja alipodai uraia wa Bashe una utata.

Baada ya siku chache waziri mwenye dhamana ya masuala ya uraia, wakati huo, Laurence Masha akasema uraia wa Bashe hauna utata. Kilichofuata ni Bashe kugoma kumnadi mgombea wa CCM Nzega na vigogo wa CCM wakaandamana kumbembeleza.

Hata kama amesamehe, majeraha hayajapona na hawezi kamwe kuaminika anapotoa hukumu zake katika kutafuta mustakabali wa CCM na jumuia zake.

Machoni pa wengi, Bashe ni tarishi wa kundi la mafisadi. Hata “kuzushiwa” utata wa uraia ulikuwa ni mzengwe wa kumkomoa katika minyukano kati ya mafisadi, mafisadi-kati, na wapambanaji wa ufisadi ndani ya CCM.

Habari zilizoenea sasa ndani ya jumuia hiyo na chama chenyewe ni kuwa tatizo linaloonekana kuwa kubwa eti ni tabia ya viongozi kuongea hadharani masuala ya chama. Lakini wakati mwenyekiti wa chama amekuwa akilalamika kuwa vikao havifanyiki kama katiba inavyoagiza.

Kutokana na hali hiyo, kamati ya Bashe bila shaka itakuja na mapendekezo yaleyale ambayo yanadaiwa kuwa yanapigiwa chapuo na watuhumiwa wakuu wa ufisadi.

Kwanza, kamati ya Bashe itakuja na mapendekezo ya kutenganisha kofia mbili za uongozi – mwenyekiti wa chama na rais wa Jamhuri. Huu ndiyo mradi ambao Lowassa anautaka utekelezwe katika harakati zake za kuelekea ikulu mwaka 2015.

Pili, kamati ya Bashe itataka mawaziri wote serikalini wasiwe wajumbe wa Halmashauri Kuu ya taifa (NEC). Hoja inayojengwa katika hili, ni hatua ya mawaziri kuwa wajumbe wa NEC kumechangia kudhoofisha chama hicho kwa kuwa NEC sasa haiwezi kuita mawaziri na kuwakemea pale wanapotenda kinyume na maagizo ya chama.

Tatu, kamati ya Bashe itakuja na mapendekezo ya kufukuzwa kwa Kamati ya Utekelezaji ya UV-CCM, kwa hoja kwamba kamati hiyo ndiyo chanzo kikuu cha chama kuvurugwa. Itaeleza jinsi ilivyoshindwa kuitisha mikutano ya baraza kuu katika kipindi muhimu cha kampeni.

Hoja hii, ni lazima itaingizwa katika taarifa ya kamati ya Bashe kwa kuwa, hata kabla ya kwenda Dodoma, hoja kubwa iliyokuwa imejadiliwa ni kufukuzwa kwa kamati ya utekelezaji.

Hoja ya kufukuzwa kwa kamati ya utekelezaji ilikosa nguvu Dodoma kwa kuwa mmoja wa walengwa wakuu wa kufukuzwa, Benno Malissa alionekana tayari amejisalimisha kwa kambi ya Lowassa.

Wala hakuna anayetarajia kuwa kamati ya Bashe itakuja na pendekezo la kunusuru chama kwa kuagiza NEC kuwaondoa katika nafasi za uongozi, Lowassa, Rostam na Andrew Chenge ambao tuhuma dhidi yao zinakielemea chama.

0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: