Kamati ya Bunge yalikoroga


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 04 July 2012

Printer-friendly version
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na  Usalama, Lowassa

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, inadaiwa “kukubaliana” na utawala wa Morocco juu ya kuinyima Sahara Magharibi uhuru kamili.

Katika safari ya kamati hiyo nchini humo, hivi karibuni, inadaiwa wajumbe wa kamati waliombwa na serikali ya Morocco kuipigia chapuo katika vikao vya Umoja wa Afrika (AU) ili Sahara isipate uhuru kamili.

Kamati hiyo yenye wajumbe 21, inaongozwa na Edward Lowassa na makamu mwenyekiti wake ni Mussa Zungu.

Kwa karibu miaka 40, wananchi wa Sahara wamekuwa wakidai kutohesabiwa kuwa sehemu ya Morocco iliyo chini ya utawala wa kifalme.

Sahara ilikuwa koloni la Hispania tangu mwishoni mwa karne ya 19 na imekuwa kwenye orodha ya Umoja wa Mataifa (UN) ya nchi ambazo hazijapata uhuru.

Mwaka 1965 baraza la UN lilipitisha azimio la kutaka Hispania iachie Sahara iwe huru. Mwaka 1966 UN ikapitisha azimio la kutaka kuwe na kura ya maoni kuhusu uhuru wake.

Lakini mwaka 1975 Hispania ilijiondoa katika utawala wa Sahara, ikiacha nchi hiyo chini ya utawala wa Morocco ambayo kwa miaka yote ilikuwa ikidai kuwa ni sehemu yake.

Tangu hapo, chama cha ukombozi wa Sahara cha Polisario, kimekuwa kikipigania uhuru wa nchi hiyo.

Taarifa zinasema kamati ya bunge iliombwa na serikali ya Morocco kushawishi serikali ya Tanzania na baadaye serikali kushawishi nchi za Kusini mwa Afrika na baadaye Umoja wa Afrika (AU) kukubaliana na Morocco kuwa Sahara ni sehemu yake.

Mwandishi alimtafuta Lowassa kuzungumzia suala hilo bila mafanikio. Simu yake ya kiganjani iliita bila kupokewa na hata ujumbe aliopelekewa haukujibiwa.

Miongoni mwa wajumbe wa kamati walioandamana na Lowassa ni Mohammed Sanya.

Sanya alipoulizwa juu kamati kukubaliana na Morocco alisema, “Ndugu yangu, katika hili unanionea bure tu. Mimi si msemaji wa kamati. Msemaji ni mwenyekiti mwenyewe Mhe. Lowassa (Edward).

“Maana mie nikisema inaweza ikatafasiriwa tofauti. Nami sitaki kwenda kinyume cha utaratibu. Haya uliyonihoji ni mambo mazito bwana…inabidi wewe umtafute mwenyekiti mwenyewe.”

Alipobanwa Sanya alisema, “…kwanza naomba nieleweke. Ni kweli tulikwenda Morocco na  ripoti ya huko nadhani haijakamilika. Ikikamilika haina shida wahusika watafahamishwa. Lakini zaidi anaweza kuzungumza mwenyekiti.”

Mjumbe mwingine wa kamati hiyo, Augustino Masele alipoulizwa juu ya makubaliano katika safari hiyo alisema, “Aah kaka, mimi sikwenda Morocco. Huko alikwenda mwenyekiti wa kamati, makamu wetu na wajumbe kadhaa. Mimi nilikwenda Ubelgiji; ya huko siyajui.”

Naye, Muhammed Seif Khatib alisema, “Kwa bahati mbaya mimi sikwenda huko. Mtafute Mhe. Lowassa, Mhe Zungu, Mhe. Shellukindo na Mhe. Rachel Mashishanga. Hao wanaweza kukujibu.”

Gazeti lilitaka kujua iwapo ni kweli kamati ya bunge ilikubaliana na Morocco juu ya kuinyima uhuru Sahara.

Taarifa nyingine zilizofikia gazeti hili zilisema kuna mjumbe aliyependekeza kuwa Morocco na Sahara zinaweza kukaa kama Tanganyika na Zanzibar.

Hata hivyo, msimamo huo waweza kuonekana wa kipuuzi kwa kuwa mazingira ya Morocco na Sahara ni ya kikoloni; wakati mazingira ya hapa ni ya nchi mbili huru zilizofanya makubaliano.

Tangu enzi za utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, Tanzania imekuwa na msimamo wa kuona Sahara Magharibi ikiwa nchi huru.

Msimamo huo ameushikilia Dk. Salim Ahmed Salim akiwa katibu mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) na baadaye AU.

Rais wa Sahara, Mohammed Abdelaziz alifanya ziara ya siku mbili na kupokewa na mwenyeji wake Rais Jakaya Kikwete. Walifanya mazungumzo na mwenyeji wake na usiku alihudhuria dhifa ya kitaifa.

Taarifa zinaeleza kuwa rais alitaka kujua msimamo wa Tanzania kuhusu Sahara na iwapo ulishabadilika.

Rais Kikwete alimwambia kuwa Tanzania haitayumba katika msimamo wake wa kuunga mkono juhudi za uhuru wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Saharawi.

MwanaHALISI lilimtafuta Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano Kimataifa, Benard Membe ambaye naye ilielezwa kuwa hivi karibuni alikuwa Morocco.

Membe alikataa katakata kujadili mambo yanayohusu kamati ya bunge, akisema “…muwaulize wanaohusika. Mimi kweli nilikuwa Morocco lakini kwa shughuli maalum zilizonipeleka.”

Akiongea kwa simu kutoka Johannesburg,  Afrika Kusini, juzi Jumatatu ambako anahudhuria mkutano wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Membe alisema kikao hicho kinahusu pia suala la Sahara.

Alisema nchi 11 za Sadc zinaunga mkono uhuru wa Sahara, na kuongeza kuwa hata Zambia, ambayo mwaka jana ilitiliana saini na Morocco kupinga uhuru huo, imekubali kubadili msimamo wake.

“Kesho (Jumanne) nitafanya wasilisho maalum juu ya msimamo mpya wa Zambia na hivyo, msimamo chanya wa nchi zote za Sadc katika kuunga mkono uhuru wa Sahara,” ameeleza Membe.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: