Kampeni bado Zanzibar, halahala CCM


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 25 August 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

DAKTARI Ali Mohamed Shein aliposema atafanya kampeni za kistaarabu na kiungwana, nilijua dhamira njema ya kujenga siasa za maridhiano Zanzibar inaendelezwa.

Nilijua sababu za Dk. Shein kutoa tamko lile na hasa kwa pale alipopatumia kulitoa. Ilikuwa ni mara tu baada ya kutangazwa rasmi ni mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi wa Rais wa Zanzibar.

Nilijua Dk. Shein anakubali mabadiliko. Anataka mabadiliko yasimame imara. Anataka wanachama wa CCM wasahau siasa za chuki na wakubali siasa za maridhiano.

Dk. Shein anajua fika CCM ndiyo chama kinachoshika dola. Kwa kushika kwake dola, na katika mazingira ya kiulinzi ya Tanzania, ndicho chenye nafasi ya wafuasi wake kuanza fujo.

Dk. Shein anajua fika katika uchaguzi uliofanyika Zanzibar tangu mwaka 1995, wafuasi wa CCM ndio waliokuwa mstari wa mbele katika kupiga wafuasi wa vyama vya upinzani.

Isitoshe, Dk. Shein anajua fika tangu mfumo wa vyama vingi urudishwe nchini kwa sheria ya bunge ya mwaka 1992, madhara makubwa ya siasa chafu yamewakumba zaidi wanaopendelea upinzani.

Wanafalsafa wanaamini kuwa popote pale wafuasi wa chama kinachoshika dola ndio wanaofurtu ada kwa ukorofi. Na huwa wanaotoroka mkono wa sheria kila wanapoendesha siasa za vurugu.

Hawa ni wafuasi wa chama kilicho madarakani. Chama ambacho kwa kawaida ya siasa za kidhalimu za Afrika na kwingineko ambako demokrasia haijastawi barabara, kustawi kwake kunategemea sana utawala.

Mara nyingi mfuasi wa chama cha upinzani, na hasa kile ambacho huonekana tishio kwa watawala – kuweza kuwadondosha kutoka madarakani – anapotoa kauli ya kutisha, huwa anajaribu tu kujitetea.

Kwamba yeye, huyu mfuasi wa upinzani, anatafuta namna ya kujikusuru/kujifariji lakini anajua wazi amezidiwa ubavu na mfuasi wa chama tawala. Mwenzake ana mgongo wa kuegemea.

Chama dola kinategemea nguvu ya wafuasi wake. Lakini kinategemea nguvu ya vyombo vya dola: Jeshi, Polisi, Magereza, Mgambo, Usalama wa Taifa. Hivi ni vyombo muhimu kiulinzi na kihifadhi kwa chama dola.

Tumepata kusikia kauli kalikali zikitolewa na viongozi wa CCM lakini hakuna aliyewahi kushikwa na kushitakiwa mahakamani kwa uchochezi au uvunjifu wa amani. Hakuna aliyefikishwa hata kituo cha polisi kwa kauli kama hizi.

Hakuna mfuasi wa chama dola aliyehujumiwa mali zake wakati au baada ya uchaguzi mkuu nchini. Lakini matukio ya kuteketeza kwa moto mali za wafuasi wa upinzani ni jambo la kawaida.

Ile tu mfanyabiashara kuhisiwa anafadhili shughuli za upinzani, “kosa la jinai.”

Hakuna kiongozi wa chama dola CCM aliyewahi kuvunjwa mkono kama alivyowahi kuvunjwa Profesa Ibrahim Lipumba, 26 Januari 2001, siku ya mkesha wa maandamano yaliyoandaliwa na CUF – 27 Januari.

Hakuna kiongozi wa CCM aliyewahi kukamatwa akasingiziwa uhaini kama walivyofanyiwa viongozi na wanachama 18 wa chama cha Profesa Lipumba, mwaka 1997.

Alisikika kiongozi wa ngazi ya juu Zanzibar akitahadharisha kwamba “silaha zilizotumika kufanikisha mapinduzi ya 1964 zingalipo zinaweza tu kunolewa (zikatumika tena).”

Haya yalisemwa juu ya jukwaa la kampeni ya uchaguzi mkuu uliopita. Ilikuwa ni kitisho dhidi ya demokrasia, lakini alikitoa mkubwa. Alikitoa kiongozi anayelindwa na mabunduki na minjemba yenye misuli iliyokomaa. Nani amshike? Mawe!

Hivi ndivyo chama dola kinavyokuwa na kukua. Ukuaji na uimarikaji wa chama dola unafanikiwa kwa nguvu za vyombo vya dola na serikali iliyopo madarakani.

Haya Dk. Shein anayajua vizuri. Anajua namna wafuasi wa upinzani wanavyoatilika na kudhalilika kila unapofika uchaguzi.

Anajua namna wanawake ambao ni wake wa wafuasi wa upinzani wanavyobakwa na vijana wa Janjaweed – vijana watoto wa familia fukara na ambao hawana elimu wala ajira Zanzibar – na askari wasiokuwa na nidhamu.

Dk. Shein anajua namna askari wa aina hii ambao hapana shaka waliidhinishwa kuwafanyia raia uhuni – hawakudhibitiwa vyovyote vile – walivyopita majumbani mwa wafuasi wa upinzani Unguja na Pemba na kudhalilisha watu.

Lazima anajua namna Janjaweed walivyokuwa wanashinda mitaani Nyarugusu, Magogoni, Kinuni, Mombasa, Mbuyu Mnene, Welezo, Mtopepo, Mtoni, Kihinani na maeneo mengine, na kupiga watu wazima. Anajua.

Anajua vijana hawa walivyokuwa wakiiba vitu vya wananchi vikiwemo vya thamani kama mikufu na bangili za dhahabu hadi wakatoka majumbani na masufuria yaliyokuwa na chakula. Anajua hili hasa lilitokea Chake Chake, Piki na Wete. Anajua.

Basi aliposema ataendesha kampeni za kistaarabu wakati wa uchaguzi huu, nilifurahi. Nikaona kwa hakika ule ukungu uliokuwa umetanda kwenye mawingu ya kisiasa Zanzibar, unaelekea kutoweka na nafasi yake kutanda mawingu meupe yanayong’aa. Ishara ya amani kamili.

Sasa kampeni rasmi za uchaguzi unaosimamiwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) – ambao ni wa kuchagua Rais wa Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani wa Zanzibar – hazijaanza.

Lakini Dk. Shein anapita akifanya mikutano na wafuasi wa chama chake. Wenyewe CCM wanaiita mikutano ya kujenga chama. Vyovyote iwavyo, mantiki ya mikutano hii itaeleweka iwapo haitakuwa inatangazwa. Ibaki tu midomoni mwa CCM wenyewe.

Mikutano inayofanyika nje ya kampeni halafu ikawa na nasaha kwa wanachama na kwa kuwa inahutubiwa na mgombea wa urais, inachukuliwa ni kampeni tu.

Baadhi ya matamshi ya Dk. Shein katika mikutano hii yanatonesha vidonda, yanarudisha watu nyuma. Si matamshi yanayolenga kuwaelekeza wana-CCM kuamini katika siasa za maridhiano. Siamini.

Dk. Shein anaposema CCM lazima ishinde uchaguzi maana amani na mapinduzi ya Zanzibar yanategemea tu CCM na CCM ndio chama chenye uwezo wa kulinda umoja na mshikamano wa Wazanzibari, mbona ni kampeni, tena mbaya?

Ni kampeni mbaya dhidi maridhiano. Ni upanga juu ya demokrasia na utawala wa sheria. Inakera. Haya ni matamshi ya kuwaambiwa wana-CCM wahakikishe wanachukua kila hatua kuhakikisha chama chao kinashinda uchaguzi wa 31 Oktoba.

Mimi hakika najenga mashaka kwa matamshi kama haya. Najiuliza hivi ni kweli Dk. Shein anaamini hasa Zanzibar bila ya CCM haindesheki?

Au kwamba mlinzi wa mapinduzi na umoja wa Wazanzibari ni CCM tu? Mbona kimekuwepo na watu wanabakwa na askari wa dola wakati wa uchaguzi? Askari gani alishitakiwa?

Si sahihi kwa kiongozi wa ngazi ya juu kama Dk. Shein kutoa matamshi haya wakati huu chama chake kina jukumu zito la kuivusha nchi kwenye bandari salama.

Wanasiasa wangesubiri kipindi cha kampeni kianze ndipo viongozi wa vyama wapande majukwaani. Wakitaka hapo hata wakinengua jukwaani itakuwa sawa tu.

Mikutano ya ndani kipindi hiki cha kabla ya kampeni Zanzibar, isitangazwe na vyombo vya habari. Nahofu itabomoba msingi wa siasa mpya za maridhiano.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: