Kampeni bila Janjaweed, bila vituko


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 22 September 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

HALI ya utulivu na amani inayozidi kusawiri Zanzibar katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu, inazidi kuthibitisha kumbe hakuna lisilowezekana pale utawala unapoamua.

Imekuwa imani ya wanafalsafa wengi duniani kwamba siku zote viongozi waliopo madarakani ndio wenye fursa zaidi ya kuvuruga uchaguzi kuliko ilivyo kwa wanasiasa wanaohangaikia kuyadhibiti madaraka.

Wanasema chama kinachoamuru vyombo vya dola aghalabu ndicho huingia na kudhibiti mfumo wa uchaguzi ikiwemo kuziingilia tume zinazosimamia sheria ya uchaguzi.

Kwa mfano, ni vigumu kuamini chama cha upinzani ambacho hakimiliki wala kukaribia fursa ya kudhibiti vyombo vya kimamlaka vya kuweza kutumika kuelekeza hatua zinazolenga kukidhi maslahi yao – kinaweza kupandikiza wapiga kura vituoni na kuwatumia kujiongezea idadi ya kura.

Ni vigumu kwa sababu mawakala wa chama kinachoongoza dola wanaposhiriki mipango ya kuvuruga uchaguzi, hupewa ulinzi kamili na vyombo vya dola. Ndio kusema mipango mingine ya kuvuruga uchaguzi, hufanyika mchana kweupe huku wananchi wakiona. Wataisimamishaje bila dola?

Hii hufanyika kutokana na ukweli kuwa mipango yao hiyo imeidhinishwa kikamilifu na viongozi wa dola kwa kutambua kuwa ikitekelezwa vizuri, itakidhi maslahi yao ya kisiasa.

Kwa mfano, tume za uchaguzi za nchi za Afrika ambazo bado dola zake hazijakubali sawasawa demokrasia ya kweli kustawi, ni rahisi kuruhusu mbinu za watawala ili kubaki madarakani kwa kupindisha sheria za uchaguzi.

Mwaka 1995 ulipofanyika uchaguzi mkuu wa kwanza baada ya mfumo wa vyama vingi kurudishwa mwaka 1992, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilisingizia hujuma pale watendaji wake waliposhindwa kufikisha vifaa vya uchaguzi majimbo ya Mkoa wa Dar es Salaam yaliyo pua na mdomo na ghala la kuhifadhia vifaa hivyo.

Kama tukio lile halikuwa funzo lolote kwa serikali, staili ileile ya uvurugaji uchaguzi ilishuhudiwa Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2000.

Katika hali iliyomshtua kila binadamu anayefikiri vizuri, vifaa vilicheleweshwa kwenye vituo vya majimbo ambayo kuyajumuisha yote ukubwa wake, hayatimii masafa ya kilomita 30 kutoka kusini kwenda kaskazini.

Ubaya huzaa ubaya. Ufumbuzi wa uvurugaji huo, na wenyewe ukawa ni uvurugaji mpya. Askari wa ulinzi na usalama walitumwa kuvamia vituo vya uchaguzi, wakapora masanduku ya kura na kutoweka nayo kusikojulikana.

Baada ya kadhia hiyo, hatimaye, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilitangaza kile ilichoita “marudio ya uchaguzi” siku tano baadaye. Masikini tume, haikupata funzo lolote pale wenzao NEC walipotumika kuvuruga. Nao wakabariki ushetani.

Hapana shaka watawala waliokuwa zaidi wakihifadhi maslahi ya chama chao kuliko ya nchi au kufikiria hadhi ya taifa mbele ya ulimwengu, walijua uamuzi wa kurudiwa kwa uchaguzi kwenye majimbo 17 ya Mkoa wa Mjini Magharibi, usingefurahisha chama kikuu cha upinzani – Chama cha Wananchi (CUF) – na pengine kingesusia uchaguzi.

Ndivyo ilivyotokea. CUF ikatangaza kutoshiriki “marudio ya uchaguzi.” Ikahimiza watu wake wasitoke majumbani tarehe 5 Novemba 2000 kwa ajili ya kupiga kura. Kweli hawakutoka.

Matokeo yake, CCM iliyokwishajipanga upya, ikapata ushindi wa asilimia 67 usio jasho. Watawala hawakuishia hapo, walituma wanausalama kusaka fomu zote za matokeo zilizotoka vituoni ambazo zilikuwa zinaisuta CCM.

Mawalaka wa uchaguzi wa vyama vya upinzani, hususan wa CUF, waliandamwa hadi kuhatarishwa maisha ili wazikabidhi fomu zile. Nia ilikuwa kuhifadhi nyuso za wakubwa dhidi ya aibu ya mwaka kwani ingethibitika walivuruga kwa makusudi uchaguzi baada ya kuona walishapoteza.

Lakini, mipango yoyote ile ya uvurugaji wa uchaguzi inakuwa haitekelezeki iwapo viongozi hao waliopo madarakani wamebadilika na kuheshimu maslahi ya nchi. Wameamua kusema “uvurugaji uchaguzi basi.”

Ina maana wamejenga msimamo. Wanataka kujiandikia historia mpya ya kuendesha uchaguzi safi na unaoweza kuiletea nchi heshima mbele ya macho ya raia zake; bali pia macho ya walimwengu wengine.

Ndivyo inavyoonekana kutokea Zanzibar.

Wiki ya kwanza ya kampeni imepita bila ya kuguswa mtu. Ukipita kwenye baraza za wananchi mjadala mkubwa unaosikia ni mabadiliko ya uendeshaji wa kampeni ya uchaguzi kwa kuwa kuna utulivu wa hali ya juu.

Ni hali tofauti na mazoea. Inashangaza kila mtu. Inashangaza watazamaji wa uchaguzi ambao baadhi yao walishuhudia uchaguzi wa 2000 na 2005 Zanzibar. Rafiki mmoja mtazamaji ameniambia, “Ninachokiona leo sikiamini.”

Mwanaharakati huyu analinganisha idadi ya majeruhi aliokwenda kuwakagua hospitali ya Al Rahma katika siku tatu tu za kwanza za kampeni mwaka 2005. Safari hii hajaitwa kufanya hivyo. Akafanye nini wakati hakuna mikwaju?

Katika uchaguzi wa 2000 na 2005 watawala waliamini katika fujo ili kutimiza dhamira zao mbaya za kuvuruga uchaguzi na hatimaye kujibakisha madarakani.

Ndio hali halisi. Maridhiano ya kisiasa yaliyojengwa na Rais Amani Abeid Karume wa CCM na Seif Shariff Hamad wa CUF, yangali yamesimama barabara.

Bado rais mwenyewe anakumbuka, na zaidi “anathamini” ahadi yake kwa watu na dunia kwamba uchaguzi huu utakuwa huru na wa haki ili maridhiano yake na Maalim Seif yawe na maana.

Amerudia kauli yake ya Zanzibar kupata uchaguzi safi utakaoiletea nchi heshima juzi tu alipokuwa akimtambulisha Dk. Ali Mohamed Shein, mgombea wa chama chake anayewania kumrithi Ikulu, kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni yake.

Rais Karume alisema, “safari hii tutafanya uchaguzi wa kihistoria Zanzibar na kuwa mfano wa kuigwa na nchi nyingi Afrika.”

Mara mbili ameshuhudiwa akiinua juu kadi ya mpiga kura huku akitamka kuwa “safari hii hakuna uwezekano wa mtu kupiga kura zaidi ya mara moja.” Ana maana mtu mmoja kura moja tu.

Zanzibar ilishazoea mtu mmoja kupiga kura atakazo kwa kuwa afanyacho kina maslahi na watawala. Hakipingiki. Baada ya uchaguzi tangu 2000, unamkuta mtu anasema hadharani, “nilipiga kura 20 peke yangu.”

Mambo mawili: kampeni imeanza kiungwana; na hakuna Janjaweed, maarufu kwa kutembea na mapande ya nondo na kuyatumia kupiga wananchi wanaoaminika hawatachagua CCM. Je hii itaendelea?

0
No votes yet