Kampeni ya vurugumechi haina nafasi


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 08 September 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

KIPINDI cha vurugumechi kimewadia. Zanzibar wakati wa uchaguzi huwa na mambo mengi. Mengi kwelikweli kiasi cha baadhi yake kusababisha kuwachanganya wananchi.

Ingawa mchakato wa uchaguzi mkuu wa 2010 ulianza muda mrefu uliopita, hususan Julai mwaka jana pale Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilipoanza uandikishaji watu kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) la Zanzibar , kipindi hasa chenye mambo huwa kinachoingia sasa.

Keshokutwa Ijumaa, tarehe 10 Septemba, ndiyo siku ya kwanza ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi huo ambazo zitakamilika 30 Oktoba, siku ya mkesha wa upigaji kura utakaokuwa tarehe 31 Oktoba.

Wakati kama huu wa kampeni kunakuwa na vurugumechi nyingi katika maeneo ya miji, vitongoji vyake pamoja na vijijini kote Unguja na Pemba . Vurugumechi huwakumba watu wazima kwa vijana, wakubwa kwa wadogo, wanawake kwa wanaume, wote huwa katika mashaka.

Katika kampeni za uchaguzi wa 2005, wafuasi wa vyama vikuu vya siasa Zanzibar , Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), mara kwa mara walishuhudiwa wakiwa kwenye mapambano. Wengi waliumizana.

Vijana wahuni waliokuwa wakifugwa na kulishwa usiku na mchana kwenye kambi maalum za CCM zilizokuwa zikifadhiliwa na viongozi waandamizi wakiwemo wagombea wake katika uchaguzi, walikuwa wakipita maeneo ya mji wa Zanzibar hasa waliyoamini yanakaliwa kama makazi au baraza za mazungumzo na wapenzi wa CUF, na kushambulia watu.

Ni mashambulizi ya kwelikweli kwani vijana hao ambao Zanzibar walipachikwa jina la Janjaweed – sawa na vijana waliofadhiliwa na serikali nchini Sudan kushambulia wananchi wenzao wa jimbo la Darfur, lililoko Sudan Kusini, walikuwa wakirandaranda na mapanga, visu na mapande ya nondo na kujeruhi watu na kuteketeza mali.

Lakini kama vile matukio hayo hayakutosha kuleta fadhaa katika jamii, ilitia simanzi kukuta matukio mengine yaliyochochewa na vyombo vya dola. Hivi vinajulikana namna vinavyoongozwa kwa utashi wa kisiasa wa viongozi wa serikalini na ndani ya chama tawala.

Mara kadhaa vijana wa Janjaweed walikuwa wakiendesha operesheni za hujuma dhidi ya raia na mali zao huku wakilindwa na polisi. Ulinzi pia ulikuwa ukitolewa na askari wa vikosi maalum vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Vikosi vya SMZ navyo vinabaki kwenye rekodi kwa kuhusika na matukio ya ghasia wakati wa uchaguzi. Vijana wake walikuwa wakisambazwa kwa magari ya wazi katika maeneo mbalimbali majimboni wakati wa uandikishaji, kampeni na upigaji kura. Yote hayo huzua tafrani dhidi ya wafuasi wa upinzani na wananchi mitaani katika maeneo ngome za upinzani.

Ni ada kwa yale majimbo ambayo viongozi wakuu wa chama tawala wanaamini yana ushindani mkali na huenda wakayapoteza, kuwekwa kambi za Janjaweed ambazo hutembelewa na viongozi wa chama.

Ndani ya kambi hizi ambamo maisha huwa magumu, ya kubahatisha na yakiandamana na vijana hao kufundishwa vitendo vya kiharamia dhidi ya raia wema, mnafahamika kwa vijana hao kujihusisha na ulewaji, ufuska kwani wasichana na wavulana huchanganywa bila ya kuwepo udhibiti wowote kimaadili.

Vijana hawa walitumwa kuvuruga mikutano ya kampeni ya CUF, chama pekee kinachotoa ushindani wa maana Zanzibar kwa CCM. Mara kadhaa watu walishuhudia vijana hao wakicheza gwaride au mpira kwenye viwanja ambavyo walijua kiratiba vingetumika siku hiyo kwa mikutano ya kampeni ya CUF. Mingi ya mikutano ilivurugwa kwa sababu ya fujo lililozuka walipokutana na wafuasi wa chama hicho.

Majukwaa hayakusalimika. Yalitumika kwa wagombea kutoa lugha chafu; kushutumiana na kutishana. Wafuasi wakibeba vijisanamu vilivyosukwa kukashifiana baina wagombea na viongozi wa vyama hivi vikuu.

Hata Tume ya Uchaguzi ilikuwa ikiingia kati kushutumu vyama vya upinzani kwa madai ya kusababisha vurugu katika kampeni. Mara kadhaa tume ikitoa shutuma hizo baada ya kupokea malalamiko ya CCM.

Kwa sababu ya mazingira ya vurugu, si ajabu vyama vya upinzani vikapinga matokeo ya uchaguzi ambayo tangu mwaka 1995 yamekuwa yakiwaelemea. Ni CCM tu wakitangazwa kushinda. Wakiibebesha tume lawama na shutuma kwamba imeshirikiana na dola kuchafua uchaguzi.

Zanzibar imepata sifa nyingi hadi nje ya Tanzania katika uchafuzi wa uchaguzi. Inajulikana kuwa nchi inayokabiliwa na matatizo makubwa wakati wa uchaguzi kiasi cha hata mauaji kutokea baada ya matokeo kutangazwa kama ilivyokuwa mwaka 2001.

Baada ya CUF kupinga matokeo ya kushindwa uchaguzi mkuu wa 2000, walipodai kuwa wameporwa ushindi wa mgombea wao, Seif Shariff Hamad, waliitisha maandamano ya kulalamikia matokeo hayo na kudai uchaguzi mpya ufanyike.

Serikali ilipinga maandamano hayo yaliyopangwa 27 Januari, kwa kuyaita ni “haramu” kisheria, na ilijiandaa kuyavunja kwa nguvu. Hatimaye mauaji yakaanza siku moja kabla, tarehe 26, Ijumaa ambayo polisi waliua watu wawili kwa risasi.

Mtu wa kwanza kuuawa alikuwa Imam wa Msikiti wa Ijumaa wa Mwembetanga, Ustadh Juma Khamis, ambaye alipigwa risasi kwenye paji la uso akiwa mlango mkuu wa msikiti akitoka nje baada ya sala.

Ninayarudia matukio haya kwa sababu ni muhimu kuyakumbusha yaliyopita kama onyo kwa kila mtu. Yanaweza kujirudia iwapo uvumilivu wa kisiasa utadhihakiwa.

Mabadiliko makubwa

Zanzibar imepiga hatua kubwa na ya kupigiwa mfano. Maridhiano ya viongozi wakuu wa CCM na CUF yameleta utulivu mkubwa tangu viongozi wakuu wa CCM, Rais Amani Abeid Karume, na CUF, Maalim Seif walipokutana na kukubaliana kufuta siasa chafu zilizojenga chuki na hasama.

Wazanzibari wamesahau siasa za uhasama na wamechagua siasa za maridhiano kama walivyoonyesha kwenye kura ya maoni iliyopigwa tarehe 31 Julai ambapo waliidhinisha mabadiliko ya utawala yakianzia na kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi.

Sasa kampeni zinapoanza wagombea saba waliopitishwa na Tume ya Uchaguzi kugombea kiti cha urais ndio hasa wenye jukumu la kuongoza jahazi la kampeni kwa kuonyesha ukomavu wa kisiasa na kuelekeza wafuasi wao kwenye njia sahihi ya maridhiano.

Inafurahisha wote saba wameahidi kufanya kampeni za kistaarabu. Hilo linabaki jambo la kusubiriwa; bali kabla ya kuona, niseme mgombea atakayechagua siasa za hasama katika kampeni ametangaza kukataa kura za Wazanzibari.

Wagombea na majina ya vyama vyao kwenye mabano ni: Said Soud Said (AFP), Ali Mohamed Shein (CCM), Seif Shariff Hamad (CUF), Khamis Ali Bakar (Jahazi Asilia), Haji Ambar Haji (NCCR-Mageuzi), Haji Khamis Haji (NRA) na Ali Juma Khatib (TADEA).

Wote waliidhinishwa baada ya kutimiza masharti ya kuteuliwa waliporudisha fomu za kuomba uteuzi likiwemo sharti la kila mgombea kuambatanisha malipo ya Sh. 2,000,000 taslim za dhamana pamoja na fomu zilizokamilika.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: