Kandoro na hadithi ya sungura


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 09 May 2012

Printer-friendly version

KWA waliosoma katika shule za msingi za Tanzania kabla na mwanzoni mwa miaka ya 1990, bila shaka wanakumbuka hadithi ya “sungura mjanja na sizitaki mbichi hizi.”

Hadithi hii iliandikwa kwa mtindo ya shairi, katika kitabu cha Kiswahili darasa la tatu. Hapa nitakumbusha walau beti mbili za kwanza, kulingana na nafasi.

Hadithi inayokuja, ni ya sungura sikia
Hadithi uliyoingoja, leo ninakuletea
Alitoka siku moja, njaa aliposikia
Njaa aliposikia, sungura nakuambia.

Siku hiyo akaenda, porini kutembelea
Akayaona matunda, mtini yameenea
Sungura akayapenda, mtini akasogea
Mtini akasogea, sungura nakuambia.

Hadithi hii inasimulia kisa cha sungura aliyekuwa na njaa, akiwa na nia na ari ya kuruka kuchuma ndizi iliyoiva mtini bila mafanikio. Alitumia ujanja na nguvu zake zote kufikia ndizi zile, lakini hakuambulia kitu.

Baada ya kuruka mara kadhaa bila mafanikio, sungura alichoka na kukata tamaa.  Kwenye beti za mwisho za shairi hilo, sungura alibadili kauli na kuzibeza ndizi hizo, “ eti sizitaki mbichi hizi”.

Kisa hiki hakina tofauti sana na tukio la sasa la Mkuu wa Wilaya (DC) ya Mbozi, Gabriel Kimolo aliyeamua kuachia ngazi kwenye nafasi hiyo.

Amesema hawezi kuendelea kutumika katika serikali ambayo kuna watendaji wasio waadilifu lakini hawachukuliwi hatua. Pia amezungumzia hatua ya serikali kuruhusu kampuni moja kununua kahawa mbichi kwa mazingira yasiyo na maslahi kwa wakulima.

“Tangu 2010 Novemba baada ya uchaguzi mkuu, mkataba wangu wa kipindi cha 2006-2010 kiliisha rasmi. Tangu wakati huo nilitarajia uteuzi mwingine wa kipindi cha 2011-2015 kama ilivyo kwenye sheria ya mkataba wa uteuzi wangu; sasa ni kipindi cha mwaka mmoja na miezi sita, kipindi hiki ni kirefu sana na kimeathiri katika utendaji wangu wa wilaya kama mkuu wa wilaya na familia yangu kwa ujumla,” alisema DC huyo aliyetarajia kukabidhi ofisi jana kwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbozi.

Katika utamaduni ambao haukuzoeleka hapa nchini, Kimolo aliandika barua ya kujiuzulu kwa Rais Jakaya Kikwete aliyemteua na kuiwasilisha kwa Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mbeya, Abbas Kandoro, akieleza bayana sababu za kujiuzulu kwake.

Kimolo, bila shaka akijua mapema mambo ambayo yangetokea baada ya kujitoa ndani ya serikali, aliamua kujitokeza kwa waandishi wa habari na kuweka wazi sababu zake za kujiuzulu.

Lakini kinyume cha matarajio ya wengi, Kandoro ambaye hahusiki na uteuzi wa wakuu wa wilaya ameibuka kumjibu, na mbaya zaidi kusoma barua ya DC kujiuzulu ambayo haikuelekezwa kwake.

Kandoro badala ya kujibu hoja na  tuhuma za ufisadi alizoibua DC Kimolo ndani ya serikali, yeye amemrukia DC huyo kuwa anataka kujisafisha na kujikosha.

Amesema kuwa Kimolo amefikia hatua baada ya kubaini kuwa hatakuwamo katika uteuzi wa mpya wa wakuu wa wilaya unaotarajiwa kufanyika karibuni.

Kabla ya kujizulu kwake, DC Kimolo alikuwa “mtu safi, mwenzetu, tunayeshirikiana naye,” lakini baada ya kujiondoa serikalini na kurusha tuhuma nzito, amebadilika na kuwa, “siyo mwenzetu, anajikosha na hayumo kwenye orodha ya wakuu wapya wa wilaya”. Sizitaki mbichi hizi.

Ni jambo la kushangaza kuona mtu anaomba kujiuzulu kwa rais, lakini Kandoro anakuja hadharani na kusoma barua yake kwa waandishi wa habari na mbaya zaidi anaongeza “ya kwake” ambayo hayamo kwenye barua hizo.

Kandoro amekaririwa na vyombo vya habari akisema, “Sasa nataka niwaambie jambo ambalo (Kimolo) hakutaka kuwaambia wala kuandika kwenye hii barua yake, ni kwamba Machi 23, mwaka huu, Kimolo alipewa barua kuwa hatakuwepo katika orodha ya wakuu wa wilaya inayotarajiwa kutangazwa hivi karibuni.”

Kwa kauli hii Kandoro anashangaza kweli kweli. Kwanza anatunga sababu za DC Kimolo kujiuzulu, maana hizi zake hazimo kwenye barua wala DC mwenyewe hakuzieleza kwa waandishi wa habari.

Pili, anataka umma uamini kwamba yeye anajua nani yuko kwenye orodha ya wakuu wa wilaya na nani hayumo. Kama ni kweli, itabidi tujiulize, Kandoro ana ubia gani na Raia Kikwete?

Yaani Rais Kikwete amemtuma Kandoro kumjibu mteule wake kwa njia ya mipasho isiyokuwa na tija, kama ambayo tumezoea kuisikia kwenye vyama vya siasa!

Kwenye vyama ni kawaida kusikia, mtu anayehamia chama kingine anavyosemwa na kurushiwa madongo kana kwamba hawajawahi kuwa mwanachama au kiongozi muhimu kwenye chama anachohama.

Utasikia mara “ooh, huyu ni gamba, mara ameondoka na pesa za chama, mara tulikuwa tumeshamfukuza, mara amenusa kwamba hatakiwi akaamua kuondoka mapema” na maneno mengine kedekede.

Lakini pia, kauli hii ya Kandoro inatoa ujumbe mahususi kwa umma, kwamba uteuzi wa Rais Kikwete unavuja mapema na kuwafikia wananchi kabla ya muda wake.

Cha ajabu zaidi, ni pale Kandoro anaposema Kimolo amepewa barua ikimweleza kuwa hatakuwamo kwenye orodha ya wakuu wa wilaya. Yale yale, sizitaki mbichi hizi.

Yaani Rais Kikwete siku hizi amefikia hatua ya kuwaeleza wateule wake mapema kuwa hawatakumwo kwenye uteuzi unaofuata?  Na anawaeleza kwa barua na kuwafahamisha wateule wengine walioko juu yao? Ina maana wakuu wa wilaya wote nchini hivi sasa wanajua kama watakuwamo kwenye uteuzi mpya au la?

Kulikuwa na haja gani DC kuandikiwa barua kuelezwa hatakuwamo kwenye uteuzi badala ya Rais Kikwete kumfukuza kazi kwa makosa aliyonayo kama yapo?

Hii, kama ni kweli, tumefika hatua mbaya, na pia ni hatari kwa nchi yetu. Je, hii haitakuwa fursa ya wateule hao wa rais kutumia vibaya ofisi zao baada ya kubaini kuwa hawana chao tena?

Kama utaratibu huu ungekuwapo, kwa nini rais amefikia hatua ya kupangua baraza zima la mawaziri wiki iliyopita, badala ya kuwaandikia barua mawaziri wasiostahili kuwajulisha mapema ili nao wajiondokee kama DC Kimolo?

Kwa ujumla kitendo alichofanya Kandoro, ingawa yeye anadhani kinaihami serikali, ni kibaya. Kinaweza kuzuia uhuru wa viongozi kuwajibika kwa kujiuzulu pale wanapoona hawana msaada au wanakwamishwa kiutendaji ndani ya serikali na mashirika ya umma.

Nikiamini kwamba Kandoro ameteleza na kudandia shughuli ambayo si yake, bado natega masikio kusikia kauli ya Rais Kikwete juu ya uamuzi wa DC Kimoro na sababu zake za kujiuzulu, huku nikilinganisha na sababu alizoeleza Kandoro akitaka umma uziamini bila kujali kwamba zinaidhalilisha serikali.

0
No votes yet