Kanisa kutikisa 2010


Aristariko Konga's picture

Na Aristariko Konga - Imechapwa 19 May 2009

Printer-friendly version
Lalenga kubadli mwelekeo wa siasa
Labaini kasoro katika utawala
Kadinali Pengo

KANISA Katoliki Tanzania limejipanga kuleta mabadiliko makubwa ya kiuongozi nchini, MwanaHALISI limebaini.

Tayari mpango wa kanisa umeanza na taarifa zinasema hatua ya utekelezaji iliyofikiwa hadi sasa ni ya kuridhisha.

Mchakato wa kanisa ulioanza Januari mwaka huu unalenga mafanikio ya kwanza yapatikane katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaofanyika mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwaka kesho.

Mpango wa kanisa umelenga kuamsha waumini na wananchi wote kwa ujumla ili washiriki katika kuleta mabadiliko makubwa ya uongozi wa nchi, kuanzia vitongoji, mitaa, vijiji hadi ngazi ya taifa.

Huu ni mpango shirikishi wa aina yake unaolenga kutoa elimu juu ya uongozi bora, viongozi bora na jinsi ya kuwapata wawakilishi sahihi wa wananchi.

Mchakato wa Kanisa ambao tayari umechapishwa katika vijitabu mbalimbali, unalenga upatikanaji viongozi bora mwaka kesho, lakini unafanya maandalizi ya uchaguzi wa 2015 kwa vile tathmini ya hatua ya kwanza inakamilika mwaka 2011.

MwanaHALISI imepata vitabu hivyo mahsusi kwa mpango huo ambavyo vimetolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), vyenye ratiba ya utekelezaji hadi 2011.

Ratiba ya mpango huu iliyobeba kichwa cha “Mpango wa Kichungaji Kuhamasisha Jamii Kuelekea Uchaguzi,” inaeleza pia kuwa “Mungu alimpa binadamu wajibu wa pekee, siyo tu mlinzi na mdhamini wa dunia…bali pia kuwa mshiriki katika kuumba na kutunza.”

Kanisa linasema kuwa katika miaka ya hivi karibuni limegundua matatizo mengi ya uongozi ambayo yanahitaji kujadiliwa na kutafutiwa tiba.

“Uongozi unahitaji watu wenye sifa ya huduma, wanaojali, waliowazi, wanaowajibika, wanyenyekevu, wenye hekima na upendo…Lakini uongozi kila mara unashawishika kutenda kinyume na hayo na kuwa na uchoyo na kutumia madaraka vibaya,” linaeleza kanisa.

Katika kukabiliana na hali hiyo, kanisa linasema, “Ni muhimu kuandaa viongozi, kushirikiana nao na kushikamana nao na kuwadhibiti kwa lengo la kuwasaidia kuwa jasiri walio waamnifu katika kazi zao.”

Kanisa linasema watu wanapaswa kuangalia namna wagombea wanavyoteuliwa na vyama vyao, na pia kutafuta njia na vyanzo vya fedha za vyama vya siasa na namna wanavyozitumia.

Lakini pia kanisa linawataka waumini wake kujadili mfumo wa uwakilishi wa uwiano na kuona kama unaweza kuwa bora kuliko ule wa sasa wa mgombea mwenye kura nyingi ndiye atangazwe mshindi.

“Kuna haja kubwa pia ya kuwasaidia watu kuijua Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni lazima katika mambo ya kijamii tuwahimize watu kueleza matatizo wanayokumbana nayo…na kuyatolea taarifa katika ngazi ya Parokia hadi jimbo au wilaya.

“Tuwasaidie kushiriki katika utawala tangu ngazi ya serikali za vijiji au mitaa hadi ngazi ya halmashauri ya wilaya na kutafuta taarifa, kisha kufuatilia nini watumishi wa umma wanafanya katika kuhudumia watu,” inasema taarifa ya kanisa.

Kanisa Katoliki limepanga kuunda timu kutoka Chama cha Wanataaluma Wakristo Tanzania (CPT) na wajumbe wa halmashauri, kutengeneza maswali maalum yanayoendana na mazingira husika ili watu wajadili na kutoa maoni.

“Hapa tusiwape nafasi wale ambao ni wagombea wa kisiasa kutawala mjadala,” kanisa limeonya.

Katika kijitabu kingine CPT wametoa “mada za kuongoza maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2010,” ambazo ni Uongozi Mintaarafu Ufunguo wa Mabadiliko nchini Tanzania, na Vipaumbele kwa Misingi ya Mafundisho ya Kanisa kuhusu Jamii.

Mada nyingine ni Mfumo wa Kisheria Tanzania: Mapengo na Changamoto zake, Haki za Binadamu katika Sera za Biashara na Fedha, Hifadhi ya Jamii, na Mtazamo wa Kimaadili katika Mfumo wa Siasa na Uchumi.

Katika mada ya Uongozi Mintaarafu, kanisa linasema viongozi ni lazima waaminike na wawajali watu, kwa kuwatendea haki na siyo kufukuzia mali na utajiri na kwamba fikra na taratibu mpya zinahitajika kuwezesha umma kushiriki katika kufanya maamuzi.

“Hatujajipanga kujiongoza, ila kwa ushawishi wa watu kukubali yale wataalam na viongozi wa kisiasa wanayoamini ni mazuri kwa ajili yao,” kanisa linaeleza.

Kama ratiba hiyo ya Kanisa Katoliki itatekelezwa kama ilivyopangwa, na wananchi wengi wakafikiwa na kupewa elimu hiyo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2010, basi kunaweza kutokea mabadiliko makubwa ya safu ya uongozi wa nchi mwaka ujao.

Mpango huu unadhihirisha kuwa kuna mambo ambayo yatakuwa yamewashtua maaskofu wa Kanisa Katoliki na hata viongozi wengine wa dini.

Mchakato huu unaweza kuleta mabadiliko ambayo pengine historia ya nchi hii haijawahi kushuhudia tangu uhuru, kama ratiba ya kanisa itafuatwa na kutekelezwa kikamilifu.

Ratiba inaonyesha ilianza kutekelezwa Januari mwaka huu kwa Baraza la Maaskofu (TEC) kufanya mkutano wa taifa wa kutengeneza programu na wahusika walikuwa wakurugenzi wa kichungaji na wajumbe wa Tume ya Haki na Amani.

Kazi ya kukamilisha programu katika mfumo wa vijitabu ilifanyika Februari na mpango wa kutuma mpango huo kwenye majimbo ulitekelezwa Machi, walengwa wakiwa maaskofu, wakurugenzi wa uchungaji, majimbo na viongozi wa Tume ya Haki na Amani wa majimbo.

Aprili mwaka huu kulikuwa na mikutano ya kila jimbo ya kuzindua programu, walengwa wakiwa mapadre, watawa, halmashauri na vyama vya kitume na taasisi. Walioanza ni mapadri na watawa, wakifuatiwa na walei.

Semina kwa ajili ya walei na vyama vya kitume katika ngazi ya parokia zilianza mwezi huu na zitaendelea hadi Juni. Walengwa ni halmashauri zinazojumuisha viongozi wa jumuiya ndogondogo, vyama na kamati katika ngazi hiyo.

Programu itafikishwa katika jumuiya ndogondogo kati ya Julai na Septemba na walengwa watakuwa waumini na wakazi. Wasimamizi wa kazi hiyo ni paroko na halmashauri ya parokia.

Oktoba hadi Desemba 2009 kutakuwa na mijadala na utekelezaji katika ngazi ya jumuiya ndogondogo na vyama vya kitume. Wasimamizi watakuwa paroko, kamati ya utendaji na viongozi wa jumuiya hizo.

Mkutano wa taifa wa tathmini ya kwanza ya uelimishaji wananchi utafanyika Januari 2010, miezi tisa kabla ya uchaguzi mkuu kwa kushirikisha wakurugenzi wa kichungaji na wajumbe wa Tume ya Haki na Amani.

Februari hadi Septemba 2010 kutakuwa na mwendelezo wa mijadala na utekelezaji, vinavyolenga waumini na wakazi katika majimbo, parokia, jumuiya ndogondogo na wananchi kwa ujumla.

Hatua hii ndiyo itaongoza hadi uchaguzi mkuu ifikapo Oktoba 2010. Mkutano wa taifa wa tathmini ya pili ya mpango huu utafanyika Januari 2011, ili kubainisha ajenda baada ya uchaguzi.

0
No votes yet