Kanisa lamweka pabaya Kikwete


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 01 September 2009

Printer-friendly version

UHUSIANO kati ya serikali na kanisa umeingia doa na unaweza kuvunjika. Kanisa limekataa amri za serikali. Katika hali isiyo ya kawaida, kanisa limeieleza serikali kuwa haliwezi kutafuta ushauri kwake kila linapotaka kuwasiliana na waamini wake.

Msimamo wa kanisa uliwekwa wazi na Askofu Mkuu wa Jimbo la Dar es Salaam, Polycarp Kadinali Pengo, mjini Mwanza wiki iliyopita, kwenye mazishi ya Mhashamu Askofu Anthony Mayala.

Pengo alichukua fursa ya mazishi kujibu Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyoagiza kanisa kufanya ushauri na serikali kabla ya kuandika nyaraka zao.

Hali hiyo inafuatia kanisa Katoliki kutoa waraka maalum unaotoa elimu ya uraia kushirikisha wananchi katika mjadala na mchakato wa uchaguzi ili kupata “viongozi bora” katika chaguzi zijazo.

Katika kikao chake wiki tatu zilizopita mjini Dodoma, NEC iliwataka viongozi wa dini kushauriana na serikali kabla ya kutoa nyaraka kwa waumini wao, jambo ambalo limefanya Pengo ang’ake.

Pengo, katika tamko linalotajwa kuwa kali kuliko aliyowahi kutoa kwa serikali, alisema hatua ya NEC inalenga kuyavua makanisa uwezo wa kusimamia mamlaka ya Mungu.

Alisema kanisa litaendelea kutoa nyaraka zake bila kushirikisha serikali, kwani kuruhusu hilo kutakuwa kushindwa kufanya kazi ya Mungu.

Hotuba ya Pengo iliwakandamiza Rais Jakaya Kikwete, rais mstaafu Benjamin Mkapa na viongozi wengine wa CCM na serikali ambao hawakuwa na muda kujibu.

Akitumia staili ya kuongea ya Mac Anthony katika kitabu cha Shakespeare cha Kaizari, Pengo alisema, “Ndugu zangu nimekuja kumzika Askofu. Sikuja kuleta mambo ya ugomvi…”

Alisema anaipenda Tanzania na anapenda iendelee kuwa mahali pa utulivu. “Kama nilivyosema, sikutaka kumchokoza mtu yeyote, ila najiuliza maswali, tena najiuliza kwa dhati kabisa, tunakoelekea siko,” alisema.

“Tuacheni maaskofu kama mlivyo mruhusu Anthony Mayala kufanya kazi yake, akiangaliwa na Mwenyezi Mungu. Na wale waliofanya kazi pamoja naye waendelee kufanya hivyo,” alisema Pengo.

Akijibu moja kwa moja kauli ya NEC kuwa wawe wanawasiliana na serikali kabla ya kuandika nyaraka, Pengo alisema, “Msiwafundishe maaskofu kuandika barua za kichungaji. Msiwafundishe. Mwenyenzi (Mungu) ndiye anayewaongoza.”

Alisema watumishi wa Mungu “Wanatenda kwa dhamiri kutoka ndani. Vinginevyo ni hatari, tutachanganyikiwa.”

Katika sauti ya upole Pengo alisema, “Ikiwa maaskofu lazima waiconsult political system (washauriane kwanza na mfumo wa kisiasa) ili waandike barua zao za kichungaji, (basi) mababa askofu acheni; msiandike barua yoyote; msiandike kuliko kuandika kitu kutoka kwa wale wanaotaka kutupa ushauri.”

Pengo alisema kuwasikiliza wanasiasa kabla ya kutenda kazi za Mungu ni namna moja ya kugeuza mamlaka ya chama au serikali kuwa mamlaka ya Kimungu.

Alisema maaskofu wanapoandika barua za kichungaji wanafanya hivyo ili watekeleze Neno la Mungu.

“Sasa usiwaambie acha muongee kwanza na sisi, tuone jinsi ya kuandika. Ni kitu cha hatari kabisa hicho,” alisema Pengo huku akishuhudiwa na mamia waliokuwa kwenye mazishi hayo.

Kadinali Pengo alisema amri ya wanasiasa kwa maaskofu inafanana na njia walizotumia wakomunisti wa Poland, lakini walishindwa pale “walipojaribu kuziba milango ya uchapishaji.”

“Poland walishindwa kuzima imani ya Mungu. Walitafuta mbinu ya kwamba mnapo mhubiri huyo Mungu hakikisheni mnamhubiri kulingana na system (mfumo) ya kwetu,” alieleza Pengo.

Alisema watawala Poland waliagiza kwamba “nyinyi maaskofu, mkiandika barua za kichungaji, hakikisheni hazipingani na ukomonisti. Kwa hiyo, tutazichuja barua zenu; tutawaelekeza mfanye vipi; mtakuwa mkimtaja Mungu, lakini Mungu asiyepingana na sisi,” alisema Pengo.

Kardinali alisema “Sasa Tanzania ya leo tuko mbali na hilo…Najiuliza, tena najiuliza kwa dhati kabisa, tunakoelekea ni wapi?

“Ukianza kuwaambia maaskofu, msiandike barua mpaka tupatane jinsi ya kuandika, tutafika wapi? Na kwanini tufikie hatua kama hiyo,” aliuliza Pengo.

Kuhusu upigaji vita ufisadi, Pengo alisema kuwa mchango wowote sharti utoke moyoni, kwani maneno matupu hayasaidii; badala yake yanaongeza hasira na yanajenga chuki.

Alisema kwa kuwa kauli dhidi ya ufisadi hazitoki moyoni, bora kuacha kupiga makelele yasiyojenga. Ni vema kunyamaza tu, kuliko kupiga kelele juu ya ufisadi kwa sababu umekosa nafasi ya kuwa fisadi.

“Nyamaza unatuongezea hasira, unajenga chuki katikati ya watu. Kama na wewe unataka kuwa fisadi basi fanya kwa siri. Unataka utufunike kwa maneno mazuri ya kuzuia ufisadi, kumbe na wewe chini chini ni fisadi. Wewe ni mbaya kuliko mashetani,” alisema.

Kardinali alisema, “Kelele zote hizi dhidi ya mafisadi zingekuwa zinatoka moyoni mwetu, tusigekuwa na mafisadi…Kila mmoja anapiga kelele juu ya mafisadi. Polisi anapiga kelele, mwanasheria anapiga kelele, maaskofu wanapiga kelele…

“Hakuna sababu ya kutiana hasira. Lazima kila mmoja atambue anachangia kiasi gani katika kuzuia au kuendeleza mambo haya…Maneno matupu hayatusaidii. Kila mmoja achangie katika wema au ubaya wa ufisadi,” alisema.

Akiwageukiwa wanasiasa, Kardinali alisema yamesemwa mengi juu ya mafisadi na maovu mengine.

Aliuliza, “Haya yanatoka moyoni au tunawaonea wivu wale waliofanikiwa kuwa mafisadi, kwa kuwa wamechukua vyote; sisi hatuna kitu cha kufanyia ufisadi, ndiyo maana tunapiga kelele?”

Kanisa Katoliki limekuwa na uhusiano mzuri na serikali kwa muda mrefu sasa lakini kauli za NEC na ile ya kanisa ikikataa kuagizwa la kufanya, zimeleta ufa katika mahusiano yao.

Ni mahusiano haya ambayo yanatajwa na “Muongozo wa Shura ya Maimamu” uliotolewa wiki iliyopita mjini Dar es Salaam kwamba umekuwa ukinufaisha wakristo kuliko waislamu.

Shura inakariri kile ilichoita “Mkataba wa Maridhiano” kati ya serikali na Jumuiya la Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Mkataba huu unatajwa kuhusisha “kuendeleza sekta ya huduma ya jamii kwa lengo la kupata fedha, kuratibu, kuwezesha, kuborosha na kukarabati huduma hizi kwa ajili ya manufaa ya Watanzania.”
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa CCT, Mchungaji Leonard Mtaika, makubaliano hayo ya 21 Februari 1992, yalishaisha na yalikuwa yamelenga serikali kuhakikishia asasi za kidini kuwa haitataifisha miundombinu ya afya, elimu na ustawi wa jamii inayoendeshwa na madhehebu hayo.

“Lakini sijui unazungumzia makubaliano yapi. Unayo hapo?” aliuliza Mchungaji Mtaika na kuongeza, “isije kuwa ni tofauti na ulichosema, kwani wengi wamechukua nakala na wanazitumia vibaya.”

Kwa mujibu wa kile kinachoitwa mkataba wa maridhiano, ambacho kinasambawa jijini Dar es Salaam, hati ya maridhianao inaonyesha ilisainiwa na Edward Lowassa kwa niaba ya serikali, wakati huo akiwa Waziri wa Nchi ofisi ya waziri Mkuu.

Nakala hiyo inaonyesha kuwa iliandaliwa na Profesa Dk. C.R. Mahalu, wakati huo akiwa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Malumbano ya sasa katai ya NEC na kanisa yanatokana na msimamo wa mbunge wa kuteuliwa Kingunge Ngombale-Mwiru aliyetaka viongozi wa kanisa “wauondoe waraka wao.”

Taarifa za ndani ya NEC zinasema ni Ngombale-Mwiru aliyekomalia waraka hadi likatolewa azimio la kutaka viongozi wa dini kukutana na viongozi wakuu wa nchi ili kujadili yaliyojitokeza baada ya Waraka.

Haijafahamika iwapo NEC itajadili “Muongozo wa Shura ya Maimamu” na kuagiza viongozi wa Kiislamu kuufuta au kukutana na viongozi wakuu wa serikali ili kuujadili.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: