Kanumba, Kanumba


Elius Kambili's picture

Na Elius Kambili - Imechapwa 11 April 2012

Printer-friendly version

MSANII wa filamu Afrika Mashariki na Kati, Steven Charles Kanumba ameacha pengo kubwa katika tasnia ya filamu nchini.

Ni kweli, wapo wasanii wanaoweza kuvaa viatu vyake ipasavyo, lakini itachukua muda kufikia viwango vya Kanumba aliyezaliwa 8 Januari 1984 na kuaga alfajiri ya 7 Aprili 2012.

Nyota ya Kanumba ilianza kung’ara mwanzoni mwa miaka ya 2000 baada ya kujiunga na kundi la Sanaa za Maonyesho la Kaole ambalo lilikuwa linarusha tamthiliya zake kupitia runinga ya ITV. Alianza kujihusisha na sanaa tangu miaka ya 1990.

Kanumba alizikwa jana katika makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam na mazishi yake kuhudhuriwa na umati mkubwa wa wakazi wa Dar es Salaam, mikoa ya jirani, mkoa wa Shinyanga ambako alizaliwa na mkoa wa Kagera ambako ndiko anatoka mama yake.

Alfajiri ya 7 Aprili, jiji la Dar es Salaam liligubikwa na taarifa za kifo cha Kanumba, huku Elizabeth Michael (Lulu) akitajwa kuhusika na kifo hicho.

Kuhusishwa kwa Lulu kunatokana na maelezo ya mdogo wa marehemu aitwaye Seth Bosco aliyotoa polisi.

Kanumba hakuacha taarifa yoyote; hivyo bado haijafahamika nani atarithi mali zake kwa kuwa alikuwa hajaoa wala kuwa na mtoto anayefahamika kwa ndugu zake.

Alimiliki magari, Landcruiser V8, Lexus, Toyota Hiace na Toyota GX 110. Pia alikuwa anamiliki kampuni  ya filamu iitwayo, Kanumba The Great Production.

Hakuna taarifa sahihi za kiasi cha fedha alichokuwa anamiliki, lakini alikuwa na uwezo wa kutoa filamu moja kila mwezi ambapo alikuwa anapata Sh. 20 milioni kutoka kwa wasambazaji.

Kanumba atakumbukwa zaidi kwa kuigiza na kutayarisha filamu zilizokuwa na mguso wa moja kwa moja kwa jamii na kutoa mafunzo. 

Miongoni mwa filamu alizocheza Kanumba na kumpa umaarufu ni  Dar To Lagos, She is My Sister, Uncle JJ, Oprah, Tufani, Johari, Gharika, Baragumu na Sikitiko Langu.

Nyingine ni Dangerous Desire, Cross My Sin, Village Pastor, Family Tears, Devil Kingdom, Kijiji cha Tambua Haki na nyingine.

Hapa chini ni miongoni mwa filamu za Kanumba zilizoweza kufikisha ujumbe moja kwa moja kwa jamii na kuelezea mambo yanayotokea kila siku katika jamii ya Tanzania.

Devil Kingdom

Aliigiza filamu hii mwaka jana akiwa na msanii Ramsey Nouah wa Nigeria. Humo aliigiza namna watu wanaojifanya watumishi wa Mungu wanavyohusika na vitendo vya kishirikina.

Filamu hii inaonyesha jinsi mchungaji alivyotumia nguvu za giza kujaza waumini kanisani na kutenda miujiza kwa nguvu za giza lakini mdomoni mwake akisikika akimuomba Mungu.

 Kijiji cha Tambua Haki

Filamu nzima inaeleza jinsi wananchi wanavyonyimwa haki zao kutoka kwa mamlaka husika.

Kanumba aliigiza kama askari wa mgambo katika kijiji; lakini alijikuta akitofautiana na watendaji wenzake kutokana na msimamo wake wa kutotaka kupora haki za wananchi.

Uncle JJ

Katika filamu hii, Kanumba anakutana na mikasa mbalimbali kutoka kwa watoto wa dada yake alioamua kuishi nao, lakini anapata changamoto zaidi kutokana na kutothamini mchango wa mwanamke katika jamii.

Kanumba anaamua kumpeleka shule mtoto wa kiume na kumwacha yule wa kike huku akisisitiza kwamba, hakuna ulazima wa kumpa elimu mtoto wa kike. Filamu hii imetoa funzo kwa jamii kuwa, wanawake wana haki sawa na wanaume.

Kanumba alisoma shule ya msingi Bugoyi, Shinyanga. Alikwenda shule ya sekondari     Mwadui na baadaye seminari ya Kikristo, Dar es Salaam kabla ya kuingia sekondari ya Jitegemee kwa kidato cha tano na sita.

0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)