Kapteni Komba, epusha fedheha hii


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 18 April 2012

Printer-friendly version
Uchambuzi

KAPTENI John Komba hajachelewa. Anaweza kuepusha fedheha ambayo uongozi wa shule zake unataka kumtwisha.

Angalia hili. Wiki iliyopita nilikutana na walimu watano Mwenge, Dar es Salaam. Nyuso zao zimekunjamana. Wanabubujika maneno – kati ya lawama na laana.

Angekuwa msanii wa nyimbo za asili – Saida Karoli – angeimba: Baliho mbalila, baliho mbaborooga – hawa hapa wanalia, hawa hapa wanapiga yowe.

Kisa? Uongozi wa shule ambako wamekuwa wanafundisha, ama umeshindwa au umekataa kuwalipa mishahara yao.

Hizi ni shule za mbunge wa Mbinga Magharibi, msanii mashuhuri na maarufu wa tungo nyingi – hasa nyimbo – za wasifu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Anayekataa au kupuuza kulipa walimu, anasogeza tope karibu na jina la Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM. Kwa lugha sahihi na nyepesi, anataka kumchafulia kazi, jina, umaarufu na biashara ya kuendesha shule.

Komba ni “mwenyekiti” wa Sekondari za Bakili Muluzi (Usajili Na. S. 1373); Shule ya Msingi ya Colleta Memorial (Usajili Na. DS.02/7/044) na Shule ya Awali ya Colleta (Usajili Na. DS.02/7/E.A044).

Walimu wanasema mishahara wanayodai ni ile ya mwaka 2008 kwa miezi sita – Juni hadi Novemba; mwaka 2009 kwa miezi minne – Septemba hadi Desemba; na 2010 kwa Machi na  Mei hadi Novemba.

Kwa mujibu wa walimu niliokutana nao, kuna walimu wapatao 50 ambao wanazidai shule lakini “tumekuwa tukipigwa danadana.”

“Kuna wakati unadai na kulia na hatimaye kuomba na kuambulia Sh. 5,000 au 10,000 au 30,000. Unazichukua tu na kuibua matumaini mapya ya kulipwa. Lakini matumaini hayo yanapotea kadri miezi inavyopita bila malipo…” ameeleza mmoja wa walimu.

Ofisa mmoja katika utawala wa shule za Komba amenukuliwa akikiri shule kudaiwa na kwamba “kiasi chenyewe ni kidogo…ni kama Sh. 30 milioni tu.”

Swali: Kama ni kidogo kwa nini hawalipwi?

Jibu: Nadhani wanajipanga.

Swali: Wanajipanga kwa miaka mitano?

Jibu: Hilo sasa waulize wenyewe…

Swali: Kwani shule hazina wanafunzi na wanafunzi hawalipi karo?

Jibu: Hata hilo waulize wakubwa.

Swali: Lakini shule iliishawahi kufanya matembezi ya hisani kutunisha mfuko wake; ikitarajia kukusanya kati ya Sh. 90 milioni na 150 milioni. Kiasi gani kilikusanywa?

Jibu: Ni kweli matembezi yalifanywa; lakini sijui walikuwa wanatarajia kupata kiasi gani na walipata nini.

Kwa upande wao, walimu wanasema wanafikiria kuchukua hatua “imara zaidi katika kudai haki yetu.”

Mmoja wa walimu ambaye alionekana kuwa msemaji wa wale niliokutana nao anasema, “tunafikiria la kufanya.”

Swali: Kwa nini hamwendi mahakamani?

Jibu: Tuna uwezo wa kwenda mahakamani, lakini bado tunaona umuhimu wa kujadiliana.

Swali: Lakini imepita miaka mingi. Mtaendelea kujadiliana, kujadiliana tu?

Jibu: Hakika kila kitu kina mwisho.

Swali: Sasa mbona mnatembea pamoja kama Wachina wakati wa kujenga reli ya Tazara?

Jibu: Imetokea tu tukakutana

Swali: Nimeelezwa kuwa mmekwenda Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC). Ni kweli?

Jibu: Hiyo ni katika kuendeleza majadiliano

Swali: Mmepata ushauri gani huko?

Jibu: Bado tunaendelea kufanya mawasiliano.

Bali mmoja wa wanasheria wa LHRC amekiri kufahamu malalamiko ya walimu. Alisema mwishoni mwa wiki iliyopita, “Tunatafuta jinsi ya kuwasaidia kukutana na mwajiri wao na kumaliza tatizo hili; ikiwezekana, nje ya mahakama.”

Mwanasheria alikiri pia kukutana na mkurugenzi wa shule za Komba aliyesema anaitwa Salome A. Komba ambaye aliahidi kufika ofisi za LHRC juzi Jumatatu akiwa na mwanasheria wake ili “kujaribu kutatua tatizo hili.”

Imefahamika kuwa Salome A. Komba ni mke wa John Komba.

Mwanasheria amesema hata hivyo, amewasiliana kwa njia ya simu ya mkononi na Kapteni John Komba (Mb) moja kwa moja kutoka Dodoma.

“Amenieleza kwamba atakuwa Dar es Salaam, Ijumaa hii, ili kujadili nasi na kutafuta uwezekano wa kumaliza madai ya walimu,” amesema mwanasheria.

Baadhi ya walimu wenye “mgogoro” na shule za Komba wamedai kuwa wameambiwa na mkurugenzi Salome A. Komba kuwa hivi sasa hakuna fedha; na kwamba uongozi wa shule una mipango ya kuuza shule hizo.

“Kuna wakati tumeambiwa kuwa tusubiri na kwamba shule zitakapouzwa ndipo zitapatikana fedha za kutulipa,” ameeleza mmoja wa walimu.

Bado haijafahamika shule zitauzwa lini, kwa nani na kwa kiasi gani.

“Lakini sisi walimu hatuna hisa katika miliki ya shule hizo,” ameeleza mwalimu na kuongeza, “wenye hisa ndio wanaweza kusubiri mauzo. Sisi ‘vibarua’ tunapaswa kupewa chetu tukaenda tutakako.”

Katika mazingira ya kutatanisha, hivi karibuni utawala wa shule umetoa taarifa ifuatayo:

“Tunapenda kuwatangazia kwamba mmiliki wa Bakili Muluzi Sekondari na Shule ya Colleta na Shule ya Awali Colleta ni EDUCATE GIRLS NGO.

Mwenyekiti ni Capt. John D. Komba; Katibu/Manager ni Mrs. Salome A. Komba kwa mujibu wa sheria ya wizara ya Elimu na mafunzo ya Ufundi Sura 353…”

Tangazo hili lisilo na tarehe, limesambazwa tu na halina maelezo ya nyongeza iwapo tayari shule zimeuzwa kwa “Educate Girls NGO.”

Hata hivyo walimu wanasema tangazo hilo haliwahusu. “…sisi tunajua aliyetupa kazi. Ni vizuri tu kwamba bado yumo katika hiki ambacho kinaonekana kuwa mfumo mpya. Ni watu walewale,” ameeleza mmoja wa walimu.

Bado haijafahamika walimu watalipwa lini. Ndani ya serikali na hata nje, mwalimu anaendelea kunyanyasika.

Huyu hajalipwa posho ya usafiri; yule hajalipwa nyongeza ya mshahara. Huyu hajalipwa makato yaliyofanywa bila idhini yake; yule hajalipwa mshahara wa kwanza kwa madai kompyuta haijatambua jina lake.

Lakini katika hili la shule za Muluzi na Colleta, kila mmoja anaweza kutarajia Kapteni John D. Komba (Mb) kulitatua haraka ili kuondoa fedheha inayomnyemelea.

O713 614872
0
No votes yet