Karume ametia aibu Zanzibar


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 05 January 2011

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

NILIPOSIKIA Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idi anaapa kwamba serikali mpya haitakubali ufisadi wa ardhi vyovyote vile, nilijua safari ngumu imeanza.

Ni safari ngumu na sina shaka italazimu Balozi Seif mwenyewe, Rais aliyemteua, Dk. Ali Mohamed Shein na waziri anayehusika na usimamizi wa raslimali ya ardhi, Ali Juma Shamhuna, wafunge mikanda.

Bali itakuwa safari ngumu kwa jumla maana ni lazima baraza zima la mawaziri liamue kwani watalaumiwa na wale watakaoguswa na “operesheni futa ufisadi wa ardhi.”

Niliposikia baadaye kuwa baadhi ya viongozi waandamizi wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wametakiwa kusalimisha hati za kumiliki ardhi kifisadi, nikajua kweli hakuna kisichowezekana.

Kufikia leo, taarifa zisizokanushika zinasema serikali imeshafuta zaidi ya hati 20 za kumiliki viwanja kwenye maeneo ambayo kwa asili yake ni ya wazi – ambazo ilizitoa huko nyuma.

Raslimali ya ardhi imekuwa matatizoni sana katika kipindi cha miaka 20 sasa kote Unguja na Pemba. Kumekuwa na malalamiko mengi ya makundi na watu binafsi kudai wameporwa ardhi.

Lakini katika kipindi cha miaka 10 kilichoishia Oktoba mwaka jana, malalamiko hayo yalizidi. Uporaji ulisikika kila mahali na viongozi wa juu wakitajwa kuhusika.

Tukio la wazi likahusisha vigogo waliovamia shamba la mzee Abdalla Shariff wa Shakani, nje ya mjini Zanzibar. Na licha ya mzee huyo kushinda kesi hadi mahakama ya rufani, hajarudishiwa ardhi aliyoporwa.

Mawaziri, makatibu wakuu na wabunge walihusishwa. Ni wao walifanikiwa kutumia madaraka kushawishi serikali ikatae haki na mpaka leo mwenye haki, Mzee Shariff, akifungwa mdomo.

Mara kadhaa polisi wa kutuliza ghasia walipelekwa kukaza hukumu lakini walirudi bila ya kutekeleza walichotakiwa; na sababu ikawa, “Pale kuna watu wamebeba mawe na bakora wametuzuia.”

Aibu ilioje, polisi kuzuiwa kufanya kazi halali na wanawake na watoto wadogo waliobeba bakora!

Tukio lililotokea wiki iliyopita linathibitisha ukubwa wa tatizo la ufisadi wa ardhi Zanzibar. Kule kuhusisha viongozi wa ngazi za juu wa utawala kumeshtua.

Katikati ya mgogoro wa ardhi ya Kanisa la Anglikana unaohusisha eneo la asili la kanisa hilo kijijini Mbweni Mfuuni, nje ya mji, ni familia ya Mzee Abeid Amani Karume, kiongozi mtukuka aliyeuawa kwa risasi 7 Aprili 1972.

Mkuu wa familia sasa ni Amani Abeid Karume, rais mstaafu wa Zanzibar aliyeongoza kwa miaka kumi serikali ya awamu ya sita – 2000/2010.

Bila ya kutarajia, mstaafu Karume amembeba mwanawe wa kike, Fatma Amani Abeid Karume, akisema anamiliki kihalali kiwanja kilichopo eneo la Kanisa, Mbweni Mfuuni.

Anasema Fatma anazo nyaraka halali. Kupitia picha za televisheni nikashuhudia Karume akiinua nyaraka na kuzionyesha kwa waandishi “mahsusi” walioitwa na familia hiyo ili kupaisha sauti yao.

Sikuwepo. Kwa bahati mbaya pia, waandishi ninaowaamini kikazi hawakuitwa. Sijapata simu ya Fatma, wala ya rais mstaafu Karume.

Ningeuliza, “Bibi Fatma umepata lini hati ya kumiliki kiwanja hapa?” Ningetaka kunukuu kumbukumbu za hati hiyo ikiwemo tarehe iliyotolewa, nani aliidhinisha na ilitolewa kwa maombi gani?

Vyanzo vyangu vinanieleza kumbe Fatma amepata hati mwaka 2009 – mwaka juzi. Hati ilitolewa baada ya shinikizo nyingi na maofisa wa Idara ya Ardhi na Usajili walikimbizana kila mmoja akiogopa kujiingiza. Wanasema ulikuwa “mtego mbaya.”

Ni kama vile siku walipotakiwa kupima eneo la Kibweni, mita chache kutoka nyumba ya mkereketwa mkuu wa CCM, mfanyabiashara Mohamed Raza Dharamsi na pembeni mwa Ikulu ndogo ya Kibweni. Walitakiwa kupima kwa nguvu.

Lakini kiwanja kinachobishaniwa Mbweni ni cha Kanisa la Anglikana, lenye eneo kubwa tangu karne ya 18. Tukumbuke Waanglikana ndio wakristo wa kwanza kuhamia Zanzibar. Walinunua maeneo Unguja na Pemba; hili la Mbweni ni eneo mojawapo.

Kwa sababu za kibinafsi zaidi kuliko haki, hawajapewa hatimiliki licha ya kuhangaikia kwa muda mrefu hasa baada ya kuona hatari ya wajanja kutwaa maeneo yao.

Mpaka leo wanalalamika hawajalipwa fidia kwa serikali kuchukua eneo lao Madungu, Chake Chake, Pemba palipojengwa Posta wala yalipo Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba - Wete.

Hawajatimiziwa ahadi ya wizara inayohusika na raslimali ya ardhi kuwa itatoa hati hizo. Wizara ilishindwa kutoa hati mpaka uporaji umefanyika.

Anaposimama baba hadharani kutetea mwana eti “anamiliki kihalali kiwanja” katika eneo la Kanisa, wakati eneo la mzee Karume – ambalo lenyewe lilitokana na kumegwa eneo la Kanisa – limo ndani ya ukuta uliojengwa kwa fedha nyingi, inasikitisha.

Ukweli ni kwamba kiwanja anachodai Fatma ni chake kipo nje ya ukuta wa eneo kubwa la familia yao. Wala Kanisa halina mgogoro wowote na anayeitwa mwekezaji wa hoteli pembeni na karibu na ufukwe.

Kama Fatma hana nyaraka za kuuziwa kiwanja na Kanisa, aseme amepataje uhalali huo. Isije ikawa alipata katika ule mtindo wa chukua chako mapema ulioshamiri kipindi cha miaka 20 nyuma.

Wakubwa na rafiki zao “walichukua, wakaweka waa” kwa kila walichokitaka, siyo utawala tu wakati wa uchaguzi. Nani mwenye ubavu wa kulalamika wakati ule? Yalimkuta kijana wa Kipilipilini Chwaka alipolalamika kuporwa ardhi ya kurithi na kutumiwa kujengea kituo cha petroli cha Gapco, alionyeshwa moto.

Amefunguliwa kesi ya jinai na jamhuri, na mwandishi aliyemsaidia kuchapisha malalamiko yake, Mwinyi Sadallah, akajumuishwa. Eti wachochezi. Hatimaye mpaka leo ukiingia mwaka wa tatu ushahidi tu haujamalizika.

Haya ni matukio yanayokera maana yanadhoofisha utawala bora katika nchi yenye watu wastaarabu.

Sasa hii inayomhusu rais mstaafu Karume ni kashfa nzito. Inaashiria mwanzo wa kufumuka mambo mengi kwa sababu ipo kesi mahakamani inamhusu mjomba wa Fatma, Mansour Yusuf Himid.

Mansour alikuwa waziri kwa miaka kumi ya utawala wa Amani Karume. Sasa ni Waziri wa Kilimo na Maliasili. Ni mmoja wa walioshindwa kesi na Mzee Shariff kule Shakani.

Anatajwa katika kesi nyingine iliyopo Mahakama ya Ardhi akidaiwa kutwaa ardhi visivyo. Uamuzi wa kesi hii ukitolewa, ukweli utajulikana.

Mtoto wa rais mstaafu Karume anatajwa kumiliki kwa hila eneo kubwa la ardhi kijijini Muyuni, Wilaya ya Kusini Unguja, ambako wenyeji wakitumia kwa shughuli za kilimo.

Walilalamika lakini walinyamazishwa kwa mbinu za kidola. Wamenyamaza sawa, lakini hawajaridhika maana wangali wanadai ni haki yao, hawakushirikishwa na wamezuiwa kutumia eneo la asili kwa shughuli zao.

Nahisi itakuwa shida. Mkoa wa Kusini na Kaskazini Unguja kuna malalamiko kwa familia hii kuhusu ardhi. Kuna malalamiko kisiwani Pemba kuhusu hayohayo. Mtandao wa WikiLeaks umeyaona. Mimi si mtabiri, lakini naona mengi yatafumuka.

0
No votes yet