Karume ampiku Kikwete


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 03 February 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

RAIS Amani Abeid Karume amepanda chati kisiasa hata kumzidi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

Ushahidi ni kitendo cha Rais Karume kufanikiwa kujenga maridhiano kati ya chama chake cha CCM na hasimu wake mkuu kuhusiana na mustakabali wa siasa za Zanzibar.

Mafanikio ya Karume yamekuja haraka kuliko ahadi za Kikwete zilizochukua zaidi ya miaka minne bila kuonyesha mwelekeo wa kumaliza “mpasuko Zanzibar.”

Uamuzi wa Karume wa kukubali kukutana na mshindani wake mkuu katika kugombea urais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, umemjengea heshima, siyo tu mbele ya wananchi Zanzibar na Watanzania, bali pia kwa jumuiya ya kimataifa ambayo imekuwa ikimbana Kikwete  na kutaka amalize matatizo ya Zanzibar.

Rais Karume amekutana mara mbili na Maalim Seif, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) na mgombea urais wa Zanzibar 1995, 2000 na 2005, na kukubaliana kuacha “siasa za chuki.”

Badala yake, wanasiasa hao wameahidi kushirikiana na kujenga maelewano yatakayosaidia kuharakisha maendeleo ya Zanzibar.

Maendeleo Zanzibar yamedumaa kutokana na CUF kukataa kushirikiana na serikali kwa msimamo kuwa CCM imekuwa ikikipora chama hicho ushindi katika kila uchaguzi mkuu tangu mwaka 1995.

Tarehe 30 Desemba 2005, Rais Kikwete alipohutubia bunge lililoundwa baada ya uchaguzi uliomuingiza madarakani, aliahidi kuhakikisha anatafuta ufumbuzi wa kudumu kwa alichokiita “Mpasuko wa Zanzibar.”

Mazungumzo yalianzishwa kati ya CCM na CUF na baada ya miezi 14 walifikia muafaka na ikawa ni juu ya vikao vya juu vya vyama hivyo kuuidhinisha ili utiwe saini na hatimaye utaratibu wa utekelezaji wake uanze.

Hata hivyo, huku akijua fika kwamba ndani ya chama chake kuna viongozi wasiotaka mabadiliko, Rais Kikwete aliridhia misimamo ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) hasa watokao Zanzibar na kuibua jambo jipya ambalo CCM haikuwahi kuliwasilisha katika vikao vya mazungumzo na CUF..

NEC iliyokutana siku mbili – tarehe 2-3 Machi 2008 kijijini Butiama, Musoma mkoani Mara, ilitoa tamko kuwa muafaka uliopatikana lazima upelekwe kwa wananchi ili wauhalalishe kwa njia ya “kura ya maoni” kwa kuwa utekelezaji wake utabadilisha mfumo mzima wa utawala wa nchi.

CUF ilikataa pendekezo hilo kwa kusema lilikuwa ni jambo jipya lililoibuliwa kwa makusudi ili kukwamisha utaratibu wa utiaji saini muafaka huo.

Lakini baada ya kazi kubwa iliyofanywa na kada wa CCM na muasisi wa Afro-Shirazi Party (ASP), Hassan Nassor Moyo, akishirikiana na mtu wa karibu na Maalim Seif, Ismail Jussa Ladhu, Karume alitumia vizuri fursa iliyotokea na kuwezesha kupatikana maelewano.

Kwanza, alimkaribisha Maalim Seif na kukutana mara mbili ikulu mjini Zanzibar kwa vikao vya faragha. Mkutano wa kwanza ulifanyika 5 Novemba 2009.

Huu ulitoka na taarifa fupi kwamba wamekubali kuacha siasa za uhasama na kujenga maelewano.

Walikutana tena ikulu baada ya mwezi mmoja hivi na kukamilisha majadiliano yao yaliyozaa mpango wa siri ambao hatimaye umewezesha kuandaliwa kwa hoja binafsi na kuwasilishwa mbele ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Mpango wao ulipiga hatua kubwa wiki iliyopita pale Baraza lilipokubali, kwa kauli moja, hoja binafsi ya mjumbe kutoka CUF, Abubakar Khamis Bakary na kupitisha azimio lililokuwa na marekebisho kidogo.

Katika hoja yake, Abubakar ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani barazani, alipendekeza uchaguzi mkuu wa Zanzibar uliotazamiwa kufanyika Oktoba mwaka huu uahirishwe ili kwanza iundwe serikali ya umoja wa kitaifa ya mpito itakayofanya kazi ya kutengeneza ushindani linganifu wa kisiasa utakaowezesha kufanywa uchaguzi huru, wa haki na uwazi.

Mapendekezo yaliyomo katika azimio hilo ndiyo yaleyale ambayo Rais Kikwete alishindwa kuyafikisha mwisho baada ya “kutishwa” na wahafidhina waliodai kuwa akiyaridhia, itakuwa ameruhusu kutokomezwa kwa Mapinduzi ya Zanzibar.

Ni katika vikao vya juu vya CCM Butiama, wasaidizi wa Rais Kikwete, wakiwemo Katibu Mkuu, Yusuf Makamba, Kingunge Ngombale-Mwiru na Ali Ameir Mohamed waliokuwa wanakamati ya mazungumzo na ile ya CUF, walimshinikiza akubali “kuchomekwa” matakwa ya kuitishwa kura ya maoni.Makamba alieleza kikaoni kwamba pendekezo la muafaka kupelekwa kwa wananchi ili upigiwe kura ya maoni, lilitolewa kwao na Rais Karume na kwamba “kwa upande wetu wanakamati tumeliridhia.”

Kutoka hapo, ndipo walipoibuka makada wahafidhina kutoka Zanzibar na kutoa kauli zilizomtisha Kikwete na akajikuta anakubali muafaka ukwame.

Makada waliotoa kauli za vitisho dhidi ya Kikwete na kejeli kwa Maalim Seif, ni pamoja na Asha Bakari Makame, Mahmoud Thabit Kombo na Mustafa Ahmada ambaye licha ya kuwa mgeni katika NEC, alinukuliwa akisema:

“Kulikoni! Kuna nini ndani ya CCM? Viongozi wetu mmetufikisha wapi? Utaratibu unasema bwana, nyinyi (CUF) hamna chenu. Tunajadili nini hapa?

“Mnaturudisha nyuma. Wapinzani Zanzibar hawana wanachotambua; kwao mapinduzi haramu, serikali haramu na maendeleo haramu… mnatupeleka wapi?”

Ahmada alikiambia kikao, “Wanatuita (wapinzani) wahafidhina, mahafidhina. Watasema… ‘tumeshawaweza.’ Leo sisi CCM, haki ya Mungu na Mtume, hatutashika tena madaraka Zanzibar.

“Mnatuacha wenzenu? Mnatuacha! Leo Seif (Maalim Seif Shariff Hamad) huyuhuyu ambaye hataki mapinduzi, mnakaa naye eti kuridhisha wafadhili? Mimi sikubali hili. Mapinduziiii!”

Hata hivyo, kulingana na mapendekezo katika hoja ya Abubakar, mengi yaliyokuwa katika rasimu ya muafaka, ndiyo yaliyopitishwa na baraza na wajumbe wa CCM walishiriki hadi wakati Spika alipoitisha kura na kutoka sauti ya pamoja ya “Ndio” ikimaanisha wajumbe wote wamekubali hoja.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: