Kashfa nyingine ya rushwa FIFA


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 20 October 2010

Printer-friendly version

SHAABAN Kado, kipa namba moja wa klabu ya soka ya Mtibwa Sugar, kwa ushujaa kabisa alieleza namna klabu moja isiyojulikana ilivyotaka kumhonga ili acheze chini ya kiwango katika mechi dhidi ya Simba.


Kado alimtaja mshambuliaji wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe kwamba ndiye alitumwa na watu wasiojulikana ampe kitita cha Sh. 400,000.


Kipa wa klabu ya Yanga, Yaw Berko ameibuka naye na kusema kuna vishawishi vingi wanapewa wachezaji ili wapokee rushwa katika mechi kubwa za Ligi Kuu ya Bara.


Kado hakupokea mzigo aliotumiwa na Berko anasema analinda heshima yake hivyo hatapokea rushwa kwa lengo la kupanga au kucheza chini ya kiwango au kuiangusha klabu yake.


Kauli za wachezaji wawili hao ni kielelezo kwamba soka ya Tanzania, kama ilivyo katika ngazi ya kimataifa, haiko salama.

FIFA

Mwandishi wa habari za uchunguzi, David Yallop, ni mtu wa kwanza kuweka wazi kashfa ya rushwa iliyochafua hadhi ya Rais wa FIFA, Sepp Blatter..


Katika kitabu kiitwacho How They Stole The Game, kilichochapishwa mwaka 1999,  Yallop alichunguza na kufichua namna rushwa ilivyotumika kumweka madarakani Sepp Blatter mwaka 1998.


Mwaka 2002, Rais wa Chama cha Soka cha Somalia, Farah Ado, alikiri hadharani kwamba alipewa dola 100,000 ili ampigie kura Blatter.


Katibu mkuu wa FIFA ambaye alihusika kutoa taarifa jinsi mchezo wa soka unavyoliwa Michel Zen-Ruffinen, alijiuzulu pia baada ya uchaguzi mkuu uliomrudisha madarakani Blatter mwaka 2002.


Hivyo, haishangazi kusikia kashfa nyingine ya rushwa ikiibuka na safari hii Marekani imehusishwa baada ya maofisa wake kudaiwa kutoa pesa ili iungwe mkono katika kampeni za kuandaa fainali za Kombe la Dunia.


Waandishi wa habari wa gazeti la Sunday Times la London, Uingereza walijipenyeza na kujifanya watu wanaoweza kusaidia Marekani kuandaa fainali za mwaka 2022.


FIFA imeomba maelezo juu ya uchunguzi uliofanywa na gazeti hilo na kuwasilisha nyaraka zenye rekodi ya tukio hilo. Maofisa wa FIFA wanaoshutumiwa kuhusika ni Amos Adamu wa Nigeria na Reynald Temarii wa Shirikisho la Soka la Oceania.


Katika kashfa hiyo Adamu alipigwa picha akiomba fedha kwa miradi binafsi ili aweze kuwapigia kura wakati Temarii inadaiwa aliomba fedha kwa ajili ya mradi wake wa shule ya soka.


Wakati mambo yote hayo yanafanyika, Shirikisho la soka la Marekani halikuwa na habari juu ya uchunguzi huo na wala maofisa wake hawajahusishwa moja kwa moja katika tukio hilo.


Adamu amekaririwa akisema kwamba anatarajiwa leo kuhojiwa na kamati ya maadili baada ya kuhusishwa katika kashfa hiyo. Adamu hakutaka kueleza matokeo ya kikao chake kifupi na Blatter ambaye amesisitiza ufanyike uchunguzi wa kina.


Taarifa kutoka ndani ya FIFA zimesema maofisa wawili hao wanaweza kuchukuliwa “hatua za muda” au kusimamishwa.

Mwaka 2000

Tukio hilo linakumbusha tukio jingine kama hilo ambapo Rais wa Oceania, Charlie Dempsey, alijikuta kwenye mazingira ya kupiga kura kuamua nchi moja kuandaa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2006 kati ya Afrika Kusini na Ujerumani.


Dempsey kutoka New Zealand alilazimika kukacha hatua ya mwisho ya upigaji kura, huku akitoa madai kwamba alikuwa anateswa na rushwa aliyopokea. Kwa hatua hiyo, kiongozi huyo alijiuzulu lakini maisha yake na ya familia yalibaki kuwa ya hatari kwa muda.


Dempsey mwenyewe baadaye alikaririwa akisema kuwa alikabiliwa na presha ya hali ya juu na alichoona heri kutopiga kura, hatua iliyoipa ushindi Ujerumani na kuipiku Afrika Kusini.


"Nilikuwa na sababu za msingi, ila sitazieleza,” alisema. "Sikuchukua uamuzi huo kwa wepesi. Huwa sifanyi maamuzi kwa wepesi hivyo."

Tanzania

Kwa Tanzania matukio ya rushwa katika soka huwa yanafumbiwa macho. Mwamuzi Othman Kazi alikula kibano kwa kutoa maelezo kwamba kuna watu walitaka kuwapa rushwa, lakini hakuwataja.


Mchezaji wa kiungo wa Yanga, Athumani Idd Chuji aliwahi kuikana saini yake katika usajili wa klabu ya Simba, lakini hadi leo hakuna taarifa zilizotolewa.


Katika ngazi ya klabu, wachezaji wanaotuhumiwa kula mlungula huwa wanatemwa, na siku chache husajiliwa katika klabu walizotuhumiwa.


Hata malalamiko ya Kado yamewekwa kapuni kwani kila polisi wakiulizwa walikofikia kuhusu uchunguzi wa tukio hilo, huambiwa wasubiri.


Chaguzi zote kubwa za viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (FIFA) hugubikwa na kashfa za rushwa lakini si polisi wala Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inayofuatilia na kutoa matokeo ya uchunguzi.


Hiyo ndiyo soka. Nani anasema hakuna pesa au rushwa kwenye soka?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: