Kashfa ya EPA: Vigogo hawakuhojiwa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 26 August 2008

Printer-friendly version
Mwanyika, Mwema waingia mitini
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula

TIMU ya Rais Jakaya Kikwete ya kuchunguza ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), haikuwahoji watu muhimu katika kufanikisha kazi yake, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa za karibu na wajumbe wa timu hiyo, zinasema Timu ya Rais haikumhoji aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula.

Msingi wa kumhoji Mangula yalikuwa madai kuwa fedha za EPA zilitumiwa na CCM katika uchaguzi mkuu wa 2005. Wakati huo Mangula alikuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.

Hata hivyo, Mangula aliithibitishia MwanaHALISI juzi Jumatatu, katika mahojiano ya simu, kwamba Timu ya Rais haikupata kumuita na kumhoji juu ya tuhuma kwamba baadhi ya mabilioni yaliyokwapuliwa katika Akaunti ya EPA yalitumika katika kampeni za CCM. 

Swali: Una maoni gani kuhusu hotuba ya Rais Kikwete bungeni wiki iliyopita, kuhusiana na fedha za EPA hasa matumizi yake?

Jibu: Mhm! Kuhusu hilo la fedha za EPA kuingizwa katika kilimo, hicho kwetu wakulima ni kicheko (huku sauti yake ikionyesha kufurahishwa). Lakini ndugu yangu siwezi kusema zaidi kwa kuwa sikufuatilia vizuri hotuba yenyewe kwa vile niko huku kijijini.

Swali: Kuna madai kuwa CCM ilitumia fedha za EPA katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Ni kweli?

Jibu: Sisi tulikuwa na njia zetu za mapato, si katika EPA (kimya kirefu). Tulikuwa na harambee zetu.

Swali: Uliwahi kuhojiwa na Timu ya Rais kuhusu fedha za EPA?

Jibu: Hapana.

Swali: Unasema hujahojiwa?

Jibu: Sikuhojiwa kwa hilo (ghafla akaanza kuita Halo! Halo! Halo!).

Swali: Kama hukuhojiwa kwa hilo ulihojiwa kwa lipi? (Simu ilikuwa imekatika na majibu kwa swali hilo hayakupatikana).

Juhudi za kumtafuta tena na tena kabla gazeti kuingizwa mitamboni zilifanywa, lakini mara zote simu yake ilikuwa inajibu, “Simu unayopiga haipatikani kwa sasa.”

Mjini Dar es Salaam zimepatikana taarifa kuwa mmoja wa wajumbe wa Timu ya Rais alifika nyumbani kwa Mangula jijini, mara baada ya Timu kuundwa na kumtaarifu kuwa timu yao ilikuwa na mpango wa kwenda kumhoji.

Imeelezwa kuwa Mangula alikubali kuhojiwa, lakini kwa sharti kwamba katika mahojiano hayo sharti wawepo watu wawili muhimu: Benjamin Mkapa na Mkurugenzi wa zamani wa Usalama wa Taifa, Cornel Apson.

Baada ya simu kukatika na kutopatikana tena, haikuwezekana kupata uthibitisho wa Mangula kuhusu tukio hilo.

Hata hivyo, haikufahamika pia iwapo sharti la kuhojiwa mbele ya wengine ndilo lilifanya timu isimhoji Mangula.

Taarifa za kuthibitisha iwapo Mkapa alihojiwa na Timu ya Rais hazikuweza kupatikana kutoka kwa chanzo chetu cha habari.

Mwenyekiti wa Timu ya Rais, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika hakupatikana kujibu kwa nini Timu yake haikumhoji Mangula.

Inspekta Jenerali wa Polisi, Saidi Mwema alitafutwa kupitia simu ya mezani ya MwanaHALISI ili asaidie kujibu swali hilo. Msaidizi wake alijibu haraka, “Mzee yupo ndani ana kikao, acha ujumbe atakupigia.”

Dakika tatu baadaye msaidizi huyo alipiga simu ya mkononi ya mwandishi wa habari hizi na kusema, “Nataka kuongea na Kubenea.”

Alipojibiwa kwamba anayeongea ni yule anayemtafuta, alijibu haraka, “Nilikuwa nahakiki namba iliyoachwa.”

Kwa muda sasa, kumekuwa na madai kutoka viongozi wa kambi ya upinzani kwamba fedha za EPA zilitumika kusimika Kikwete madarakani.

Hata hivyo, kwa nyakati tofauti viongozi wa CCM, akiwamo Katibu Mkuu wake, Yusuph Makamba, wamekana tuhuma hizo.

Karibu viongozi wote wa CCM ambao wangekabwa ili waseme wajuacho hawako madarakani hivi sasa.

Mkapa na Mangula ni wastaafu; na Salome Mbatia – aliyekuwa Mwekahazina wa CCM wakati huo, na Gavana wa BoT, Daud Ballali ni marehemu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: