Kashindye: Nitumeni wana Igunga


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 28 September 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
Joseph Mwandu Kashindye

HANA majigambo. Anasikiliza kila mmoja. Ni Joseph Mwandu Kashindye, mwalimu aliyeamua kuacha chaki na kujitosa katika kinyang’anyiro cha ubunge jimboni Igunga, mkoani Tabora. Anagombea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI wiki hii, Mwalimu Kashindye, pamoja na mambo mengine, anatuhumu Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuingiza watu kutoka nje ya jimbo la Igunga ili kuwachagulia mbunge wao.

Anasema, “Kila mbunge anachaguliwa na wale wanaomhitaji kwa kazi maalum ya uwakilishi wao. Lakini bila kujua kwamba mbunge atakayekuja hatakuwa wa watu walioletwa kutoka Dar es Salaam, bali atakuwa wa wananchi wa Igunga, CCM wameingiza watu kutoka nje ya Igunga ili kuwachagulia wananchi mbunge wao.”

Hivyo anasema ni vema wananchi wa Igunga wakaachwa wachague mbunge wanayemtaka na wanayeamini kwamba atawatumikia, badala ya kuwanyonya.

“Hawa (wananchi wa Igunga) ni watu wenye kuelewa. Wengine wamepata elimu, tena nzuri tu; huwezi tena kudanganywa. Wanafahamu kuwa nani hasa anataka kuwawakilisha na nani amekuja ili kujinufaisha binafsi. Ni vema matakwa yao yakaheshimiwa,”anasema Mwalimu Kashindye.

Anasema hatimaye mbunge atakuwa mbunge wa Igunga; hivyo wananchi ndio wanajua nani, miongoni mwao anafaa kuwa mwakilishi wao.

Anasema, “Igunga kuna madini ya dhahabu na chokaa kwa wingi. Kuna mifugo na ardhi yake ina rutuba inayofaa kwa kilimo cha pamba, mpunga, karanga, tumbaku, ufuta na choroko, lakini wananchi wake wengi wanakakabiliwa na umasikini wa kupindukia unaotokana na kukosa mwakilishi mwenye kuwajali.”

Anasema ni jambo la aibu kuona Igunga, miaka 50 baada ya uhuru, wananchi wake wakiwa wamebaki masikini wa kutupwa wakati kuna rasimali za kila aina.

“Igunga kuna dhahabu nyingi sana. Wataalam wanasema hapa ndipo patakapojengwa mgodi mkubwa kabisa kuliko yote nchini. Je, katika mazingira haya, wananchi wanapaswa kuchagua mgombea kutoka wizara ambayo imeingiza nchi katika mikataba ya kinyonyaji ya madini?” anahoji.

Anasema, “Bila shaka wananchi wa Igunga wanahitaji mbunge mwenye kujua matatizo yao. Mbunge anayefahamua matatizo hayo na ambaye anaona yeye ni sehemu ya umma anaotaka kutumikia.

“Huyo si mwingine, bali ni mimi Kashindye, nitakayehakikisha raslimali za jimbo letu zinatumika kizalendo ili wananchi wanufaike nazo,” anajitaka Kashindye kwa mbwembwe.

Akichangia katika bajeti ya wizara ya nishati na madini kwenye mkutano wa bunge uliomalizika, mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli alilitaja jina la Dk. Peter Kafumu, mgombea wa CCM, zaidi ya mara tano na kisha kusema, “…Kafumu, wewe mtu wa Kahama mwenzetu, huna aibu? Umegawa ardhi kwa wawekezaji kiasi hiki, utazikwa wapi?”

 Alipoulizwa mbinu atakazotumia kufanikisha mipango hiyo, Mwalimu huyo aliyeamua kuacha chaki na kujiunga na harakati za kisiasa anasema, “Jambo la kwanza, baada ya kupata ridhaa ya watu wa Igunga, ni kuhakikisha raslimali zilizopo zinatumika kikamilifu kuleta maendeleo kwa wananchi.”

 Anasema atawashawishi wananchi wa Igunga kujiunga katika ushirika wa wachimbaji wadogo wadogo ili waweze kunufaika na madini yao, kwa kupata mafunzo ya uchimbaji na kuwa na sauti ya pamoja ya kutetea maslahi yao, huku yeye mwenyewe akihakikisha anafuatilia kila hatua ya kinachofanyika.

 Akichaguliwa, anasema Igunga hayatatokea yale yanayofanyika katika maeneo mengine ya migodi, ambako wananchi wanadhulumiwa haki zao, huku wale wanaojiita wawekezaji wakiendelea kuchota dhahabu na kutokomea nayo nje ya nchi.

 Mwalimu Kashindye alizaliwa 20 Novemba 1959 akiwa ametoka katika familia masikini wilayani Igunga.

Alipata elimu yake ya msingi kati ya mwaka 1970 hadi 1976. Hakubahatika kuchaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari.

Mwaka 1982 alijiunga na mafunzo ya ualimu kwa njia ya UPE. Ni katika kipindi ambacho serikali iliweka msingi mkuu wa kukabiliana na tatizo la uhaba wa walimu nchini. Alimaliza mafunzo yake mwaka 1984.

Mara baada ya kumaliza mafunzo yake hayo, mwaka 1985 Mwalimu Kashindye aliajiriwa kama mwalimu wa daraja la III C katika shule ya msingi ya Sakamariwa iliyopo wilayani Igunga.

 Aliamua kujiendeleza kwa kujiunga na masomo ya sekondari kwa njia ya posta. Mwaka 1990 alimaliza masomo yake hayo.

Mwaka 1992, alijiunga na Chuo Cha Ualimu Kabanga kilichopo wilayani Kasulu, mkoani Kigoma kwa mafunzo ya miaka miwili ya cheti cha ualimu daraja la A.

 Kama mpiganaji na kamanda asiyechoka kutafuta anachokitaka, baadaye alijiunga na chuo cha uwalimu Mpwapwa ambako alisomea mambo mawili kwa mpigo.

Kwanza, Mwalimu Kashidye alijiendeleza kwa masomo ya Kidato cha VI na papo hapo akichukua Diploma ya ualimu. Alihitimu masomo yake chuoni hapo mwaka 1999.

Mara baada ya kumaliza masomo yake, aliteuliwa kuwa mratibu wa ualimu katika kituo cha ualimu Simbo. Ametumikia nafasi hiyo kwa miaka mitano, kabla ya kuteuliwa kuwa mkaguzi wa shule mwaka 2004.

Hata hivyo, bado Mwalimu Kashidye hakuridhika na kiwango hicho cha elimu. Mwaka 2002 alijiunga na Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) kwa mafunzo ya shahada ya kwanza ya ualimu.

Alitunukiwa shahada ya kwanza ya ualimu akiwa amebobea katika masomo ya Kiingereza na Fasihi ya lugha mwaka 2010.

Kati ya mwaka 2010 mpaka anajitosa katika kinyang’anyiro cha ubunge jimboni Igunga, amekuwa mkaguzi mkuu wa shule wilayani humo, akiwa amefundisha na kufanya kazi karibu katika shule zote za Igunga.

Alipoulizwa kilichomsukuma kuachana na taaluma yake ya ualimu na kujitosa katika siasa, Mwalimu Kashidye anasema, “Ni moyo wangu wa kujitoea.”

Alisema anafahamu “matatizo ya wananchi wangu ninaotaka kuwakilisha. Nimezaliwa Igunga. Nimekulia Igunga. Nimesomea Igunga na nimefanya kazi Igunga. Najua wanachotaka.”

“Sijaja Igunga kutafuta ubunge. Mimi ni sehemu ya Igunga na naelewa vema matatizo yake. Nafahamu kuwa wananchi wana matatizo mengi ambayo yanaweza kutatuliwa kwa kuwapo mbunge mwenye uelewa wa matatizo yao.”

Kwa mfano, anasema, “Nafahamu kwamba wananchi wa Igunga wanakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa maji. Nikiwa mbunge, nitahakikisha nasimamia vema bajeti ya maji katika halmashauri ya wilaya. Nitafanya hivyo pia katika elimu na maeneo mengine.”

Anasema, “Nitaibana serikali hadi ijenge makazi ya walimu.” Shule nyingi za sekondari za kata hazina nyumba za walimu na hiyo ni moja ya sababu inayowafanya walimu kuzikimbia.

0
No votes yet