Kasulumbayi: Nimeshinda kwa nguvu ya umma


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 17 November 2010

Printer-friendly version
Sylvester Kasulumbayi Mhoja

JAPOKUWA kinadharia kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu zilitawaliwa na matumizi makubwa ya fedha, wako wabunge wanaoweza kujitokeza kifua mbele na kusema hawakushinda kwa nguvu ya fedha ila nguvu ya umma.

Miongoni mwao ni mbunge mpya wa jimbo jipya la uchaguzi la Maswa Mashariki kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Sylvester Kasulumbayi Mhoja (59).

“Nina imani kuwa huenda mimi ndiye mbunge masikini kuliko wote katika bunge hili. Kwa lugha ya mjini ningesema mimi ni mbunge ‘choka mbaya’ kuliko wote. Nimeshinda kwa sababu wananchi ndio walionitaka. Ni nguvu ya umma,” anasisitiza.

Katika mahojiano na MwanaHALISI, Kasulumbayi alikiri kuwapo kwa matumizi makubwa ya fedha katika mchakato wa kuwania ubunge, jambo alilosema ni hatari kwa mustakabali wa taifa.

Ingawa hii ni mara yake ya kwanza kuwa mbunge, Kasulumbayi si mgeni katika siasa za Maswa. Amekwa diwani wa Kata ya Ipililo katika jimbo hilo kuanzia mwaka 1994 hadi sasa.

Amekuwa diwani wa kata hiyo akiwa na vyama viwili tofauti, Chama cha Wananchi (CUF) kuanzia mwaka 1994 hadi mwaka 2008 na Chama cha Ustawi (CHAUSTA) kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka huu.

“Ukiangalia historia yangu, utaona kwamba nimekuwa diwani kwa vyama viwili tofauti na sasa mbunge kwa chama kingine. Watu wa Maswa wananiamini na ndio wanaonipa nafasi hizi.

“Mimi maisha yangu ya kisiasa yanategemea nguvu ya umma. Ninaishi vizuri na watu na ninahakikisha kuwa ninafanya kila ninaloweza kukidhi matarajio yao,” anasema mwanasiasa huyo.

Kasulumbayi ni mwalimu kitaaluma na katika maisha yake yote ya ualimu, takribani miaka 21, amekuwa mwalimu katika shule zilizoko wilayani Maswa na anasema ndiyo maana anafahamika sana.

“Mimi ni mwalimu na katika fani yangu hii nimejifunza mambo makubwa mawili. Kwanza kwamba siku zote watu wa hali ya chini huwa ni walipaji wazuri wa fadhila.

“Kama umewahi kumsaidia maskini, ujue ipo siku na yeye atakulipa tu. Sasa mimi kama mwalimu nimekuwa nakutana sana na wazazi wa wanafunzi wangu ambao ni watu maskini. Kwa hiyo, kama unawahudumia vizuri, hawawezi kukutelekeza.

“La pili, watu huwa hawapendi watu wajivuni. Kama mtu una dharau na unabagua watu, huwezi kufika mbali katika siasa. Ukija Maswa, si rahisi kunikuta niko peke yangu kwa dakika 20. Kila wakati niko na watu na wao ndiyo wanaoniwezesha,” anasema.

Anasema kwa sababu ya kuishi vizuri na watu, alipata misaada mingi kama vile magari, mafuta na vitendea kazi vingine vya kampeni; mambo ambayo asingeweza kuyamudu kwa uwezo wake wa kifedha.

Hata hivyo, mwanasiasa huyu anaamini kwamba bunge la sasa linatakiwa kufanya kazi ya ziada kuhakikisha kwamba rushwa za uchaguzi zinakomeshwa kwa mujibu wa sheria.

“Rushwa inavuruga kabisa taratibu zetu tulizojijengea tangu zamani ambapo uongozi ulikuwa utumishi. Ikifika wakati watu wanamtazama mtu kwa uwezo wake wa kifedha badala ya uwezo wa kuhudumu, ujue nchi inakwenda kubaya,” anasema.

Changamoto

Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Kasulumbayi anasema ni kushughulikia kero kubwa mbili ambazo kwa miaka nenda rudi zinawasumbua wananchi katika jimbo lake la ubunge.

Kwanza ni suala la ugawaji holela wa ardhi unaofanywa na baadhi ya watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa wakishirikiana na wajanja wachache.

Pili, kwa kushirikiana na halmashauri ya Maswa, mbunge huyo atahakikisha huduma za jamii kama vile elimu, afya na nyinginezo zinapatikana katika kiwango cha kuridhisha.

“Wajanja wanawarubuni wananchi maskini wanauziwa ardhi wakifanikishwa na watendaji mafisadi wa halmashauri. Hili ni jambo la hatari na kuna migogoro mingi ya aina hii Maswa,” anasema.

Kuhusu elimu na afya, Kusulumbai atalazimika kufanya kazi kwa ushirikiano na halmashauri ili wapatikane walimu wa kutosha kwa ajili ya shule zilizopo na wauguzi ili huduma ya afya ipatikane bila matatizo.

Mkakati huo unatokana na sababu kwamba, katika siku za karibuni, imekuwa kawaida walimu na wauguzi kukataa kwenda kufundisha na kutoa huduma ya afya katika maeneo kama Maswa, na ndiyo maana ubunifu unahitajika katika kuwavutia waende katika maeneo ya pembezoni.

“Kwa bahati nzuri, nikiwa diwani wa Ipililo, nimeweza kufanya mambo mengi ambayo serikali ya CCM inafikiria kuyafanya kwa wananchi wa vijijini.

“Kwa mfano, hakuna mwananchi wa Ipililo ambaye anatafuta maji umbali wa zaidi ya mita 400 kutoka alipo. Hili ndilo lengo la serikali lakini sisi tayari tumepita huko na nitafurahi kama Maswa Mashariki yote itafanikiwa kufika hapo.

“Pia, vijiji vyote vya Ipililo vimeunganishwa katika barabara kuu na hili limerahisisha mno mawasiliano. Ningependa pia kuona hali ikiwa hivi jimboni kwangu.

“Hata hivyo, haya siwezi kuyafanya mimi mwenyewe. Nitahitaji ushirikiano kutoka kwa halmashauri, serikali kuu na wananchi kwa vile mimi ni mtumishi na mwakilishi wao tu,” anasema.

Historia

Mbunge huyu mpya alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya msingi Didia iliyopo Shinyanga Vijijini na elimu yake ya sekondari aliipata katika shule ya Kwiro iliyopo Morogoro.

Alipata elimu ya ualimu katika Chuo cha Ualimu Monduli kilichopo mkoani Arusha na kituo chake cha kwanza cha kazi kilikuwa ni Shule ya Msingi Lalago iliyopo Maswa mnamo mwaka 1973.

Kasulumbayi alikuwa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo na anasema tangu aanze ualimu, amekuwa akiteuliwa kuwa mwalimu mkuu katika shule zote alizowahi kufundisha.

Kasulumbayi ni baba wa watoto 17, aliowapata kwa wake zake watatu alionao. Mke wake wa kwanza ana watoto tisa, wa pili ana watoto saba na watatu ana mtoto mmoja. Wake zake wawili wa kwanza ni walimu.

Alipoulizwa na MwanaHALISI ni yupi kati ya wakeze hao ndiye First Lady wa Maswa Mashariki, mbunge huyu mcheshi alijibu kwa kucheka, “Mke wa Kwanza.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: