Katiba mpya haihitaji masharti


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 15 October 2010

Printer-friendly version
Uchambuzi
Celina Kombani

MSUKUMO wa kudai katiba mpya “katika mazingira ya amani” ili kuepusha vurugu nchini, umezidi kuimarika.

Jaji mstaafu Robert Kisanga anasema, “…katiba yetu imeshawekwa viraka vingi na sasa haiwezi kupokea viraka zaidi…” Ametaka serikali kuanza mchakato wa kupata katiba mpya, akionya isije kuwa kama Kenya ambao waliisaka kwa kasi baada ya maafa. Jaji anatoa mifano miwili kuhusu katiba.

Kwanza, analinganisha katiba na kiumbe hai; na pili, anailinganisha na shati. Kiumbe hai: “…katiba inakua kama binadamu na lazima tujue mahitaji ya binadamu huyu yanabadilika kadri anavyokua.”

Hapa ana maana kuwa mazingira ya sasa ya taifa yanahitaji katiba mpya; kwa vile hii iliyopo iliishamaliza kazi iliyoundiwa. Shati: “…kama ni shati tulimshonea mtoto mdogo, kila alipokuwa anakua na shati kumbana, tunalitanua kwa kuweka kiraka.

Lakini hatuwezi kuendelea kulitanua na kulitanua kwani kipimo cha awali kimekwisha kabisa. Katika hali kama hii, tunahitaji kumshonea binadamu huyu shati jipya linalomtosha maungoni mwake.

Kauli ya jaji mwenye umri wa miaka 77 inalenga kufafanua kuwa mazingira ya sasa yahudumiwe na katiba ya sasa; kwani kumekuwa na mabadiliko mengi ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata kiutamaduni ambayo yanadai kuhudumiwa na katiba mpya.

Huo ndio msimamo wa wengi ambao tayari wamejadili umuhimu wa katiba mpya kwa mazingira mapya. Ukitoka kwenye kauli pevu za magwiji wa sheria, unakutana na akina Celina Kombani – yule waziri wa sheria na katiba – wanaodai kuwa hawajui au hawaoni tatizo la katiba ya sasa na kwamba wenye kutaka mabadiliko wawapelekee orodha ya madai yao!

Ukitoka kwa wanasheria, wanasiasa na wanaharakati – wale wajuzi wa sheria, utawala, menejimenti ya siasa na watetezi wa haki za binadamu na utawala bora – unakumbana na waziri anayedai kutoelewa au kupuuzia kinachozungumzwa kuhusu umuhimu wa katiba mpya.

Ni matumaini ya kila mmoja kuwa waziri wa sheria na katiba awe anajua vema katiba inasema nini. Hata kama kuna maeneo ambako katiba inanyima haki, inatarajiwa waziri awe anajua ili aweze kutetea vema waliompa kazi. Kwa msingi huo, hatua ya sasa ya kudai katiba mpya inachukua sura ya ushawishi.

Mahali pengine inachukua sura ya kukumbushana. Kwingine inachukua sura ya kuzinduana. Ni hatua ya kistaarabu. Hatua ya sasa ya kutaka katiba mpya, wala haihitaji kuwataka watawala kuwauliza wananchi iwapo wanataka hili au lile.

Hapana. Inataka watawala wajipapase; watulize mbongo zao na kuona wapi wamepora haki za wananchi wao; na kukaa chini na kufikiri jinsi ya kuwarejeshea haki zao.

Hii ina maana wale walioko kwenye orodha ndefu ya sasa ya kudai katiba mpya, hawataki rabsha. Wanataka katiba ipatikane katika utulivu, ili kila raia apate haki yake ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, kitamaduni na kifikra bila kupitia njia ya majuto.

Siyo ustaarabu basi kuchukua muda mrefu bila ya kuwa na katiba inayolingana na matakwa ya wakati huu; lakini pia siyo ustaarabu kuwauliza wananchi iwapo wanataka katiba mpya; iwapo wanataka haki yao.

Wananchi hawakupoteza haki zao. Waliporwa. Hawakusahau haki zao kwenye mahame. Walinyang’anywa. Hawakukabidhi haki zao kwa yeyote kuwatunzia. Waliibiwa. Kwa hiyo zoezi lolote la kwenda kwa mwananchi na kumuuliza iwapo anataka haki yake; siyo tu litalenga kuchelewesha uhuru wa raia, bali ni dhihaka; ni uchokozi. Chukua mfano wa mwizi aliyeiba shati au blausi yako.

Anakuja kwako na kukwambia kuwa aliiba nguo yako. Anakuuliza iwapo unataka akurudishie au asikurudishie! Si atakuwa anachumbia kisirani? Tena mwizi huyohuyo, anayekuuliza kwa jeuri, anakuwekea muda na taratibu za kurudisha nguo yako ikiwa ni pamoja na wewe kuifuata atakakokuelekeza. Huko si kuleta kisirani? Tumia mfano huu.

Watawala wanajua kuwa kwa kuweka sharti la kuwa mwanachama wa chama cha siasa ndipo ugombee uongozi, tayari walipora haki ya mtu binafsi. Hapa wanakuuliza nini kama siyo kuchumbia kisirani? Kwa sharti hilohilo, wana maana kwamba wasio katika vyama hawana akili wala uwezo wa kuwa viongozi wa siasa.

Sasa kwa matusi haya, unakwenda kuwauliza wananchi kwa nia ipi, kama siyo kutafuta milipuko? Wanaodai katiba kwa njia ya ustaarabu wanajua vema kuwa rais, waziri mkuu, mawaziri na viongozi wengine wanajua kasoro ndani ya katiba ambazo zinawanyima wananchi haki zao, lakini zinawapa wao ubabe na fursa ya kuendelea kokoromea wananchi.

Chukua mfano mwingine. Rais aliyeko madarakani anaweza kujua kuwa hakika ameshindwa katika uchaguzi. Lakaini katiba inasema, vyovyote itakavyokuwa, asiwepo wa kuchunguza wala kuhoji matokeo yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi.

Kwa mtindo huu, katiba inaruhusu wizi wa kimasomaso alimradi umefanywa kumpendelea rais. Siyo lazima wizi wa kura peke yake. Kuna anjia mbalimbali za kukiuka taratibu, kanuni na hata sheria yaa uchaguzi.

Rais anayajua hayo. Waziri mkuu anayajua. Mawaziri wanayajua. Wanasiasa ndani ya chama kikubwa na cha zamani wanayajua. Bali hawataki kiwepo kipingele cha kuhoji matokeo ya uras; kwa kuwa wanataka kuendelea kukalia madaraka, kwa wema au kwa hila.

Kuna msululu wa wateule wa rais kuanzia ngazi ya wilaya hadi mkoa na taifa. Walioko ngazi ya wilaya ndio hao wasimamizi wa uchaguzi. Ni haohao pia ambao wanaambiwa kuwa hapo walipo, rais akikosa kura au kupata chache, wajue hawana kazi. Rais anajua hayo. Waziri mkuu, mawaziri na wanasiasa wengine wanajua hayo.

Ni watendaji haohao ambao tume inaajiri kwa msimu kusimamia uchaguzi. Wanasimamia ili waleta mataokeo yanayolingana na utashi au amri ya waliowatuma kazi. Inahitaji moyo kwa mkurugenzi wa wilaya kusimamia uchaguzi kwa moyo safi, bila upendeleo. Kuna ushahidi kuwa pale ambapao wakurugenzi walitiliwa shaka na kuonekana kuwa hawatapindika, walihamishwa kabla tarehe ya uchaguzi mkuu. Ufisadi mwingine!

Si hayo tu, ukakasi katika katiba, kama anavyosema Hashim Mbita, aliyekuwa Katibu wa kamati ya Ukombozi ya uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika, umo katika maeneo mbalimbali ya usimamizi na utawala. Wananchi wataendelea kudai katiba mpya.

Walioko madarakani wanajua fika, kipi walipinda kwa makusudi ili waendelee kukaa madarakani bila upinzani au kwa upinzani dhaifu. Wanajua kipi waliweka ndani ya katiba ili kunyamazisha umma na kutaka kuendelea kuuswaga kama kondoo.

Wanajua walichopora na wanachostahili kurejesha bila kuwauliza walioibiwa. Kuchelewa kufanya hivyo ni kukaribisha misuguano isiyo ya lazima na kutaka kuingia kwenye orodha ya waasisi wa machafuko yaletayo maangamizi. Tusifike huko. Katiba mpya ndiyo jawabu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: