Katiba mpya ndilo jibu pekee


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 24 November 2010

Printer-friendly version
Uchambuzi
Wabunge wa CHADEMA wakitoka ndani Bunge

BAADA ya wabunge wa CHADEMA kumwacha Rais Jakaya Kikwete bungeni, kwa shabaha ya kusisitiza umuhimu wa katiba mpya na tume huru ya uchaguzi, watawala wameweweseka.

Huyu anadai CHADEMA wanataka kuvunja umoja, amani na utulivu wa Tanzania. Yule anafura mithili ya kufutu akidai CHADEMA “wahaini.” Mwingine analoloma kuwa CHADEMA ni wasanii; na mwingine anasema wafukuzwe bungeni.

Kila watawala wanapobanwa hukimbilia kauli zenye utata au uwongo wa moja kwa moja: kuwa wanaodai haki yao au ya jamii au taifa zima, wanataka kuleta vita na kuondosha amani na utulivu.

Hivyo ndivyo wananchi wamezoeshwa. Watawala hawataki wananchi wafikiri zaidi ya hapo. Kauli za “wanaotaka kuleta vita na kuondoa amani,” ni silaha kuu za watawala katika kunyamazisha umma na hata kuufanya usifikiri tofauti.

Kwa miaka 18 sasa kumekuwa na madai ya wazi kwenye majukwaa ya siasa kuwa nchi inahitaji katiba mpya na tume huru ya uchaguzi.

Watawala ama wametoa majibu ya kejeli au wamekaa kimya. Walichoona kwenye marekebisho ya katiba ni kutamka tu kwamba nchi ni ya mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Kamba, minyororo, pingu na magereza, vilivyomo ndani ya Katiba ya nchi na sheria za uchaguzi, vimebaki vilevile. Siyo kwamba watawala havioni. Wanaviona kuwa ni vya ubabe na katili, lakini wanaviacha viendelee kuwemo kwa kuwa vinawasaidia kubaki madarakani.

Tuchukue mfano halisi wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Jielekeze kwenye Ibara 41 (7). Inasema hivi:

“Iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais kwa mujibu wa ibara hii, basi hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.”

Chini ya utawala wa mfumo wa chama kimoja, lilikuwa kosa kumpinga rais. Kwanza, rais alikimbia peke yake kama mwendawazimu na hatimaye kijitangaza kuwa ameshinda. Alikuwa anashindana na nani?

Hapa kuna “Ndiyo” na hapa kuna “Hapana.” Ukiandika ndiyo ina maana kuwa ni yuleyule. Ukiandika hapana, ina maana kuwa hapana mwingine isipokuwa huyohuyo.

Yule ambaye chama tawala kimetaka awe rais, hata akipata “Hapana” nyingi, lazima ziwe au zionekane, au zisomeke au zionyeshwe kuwa ni “Ndiyo.”

Kwa kuelewa kuwa hatimaye taarifa zitavuja, kwamba “hapana” zimefanywa “ndiyo,” ibara ikasukwa ndani ya katiba, kwamba pale mtu atakapokuwa ametangazwa kuwa rais, isiwepo mahakama yoyote ile “itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.”

Mtu aweza kujiuliza: Kwa nini kuwe na katiba inayoruhusu mwanya wa kutenda uhalifu? Kwa nini kuwe na katiba inayotilia mashaka nguzo muhimu ya dola – mahakama – katika usimamizi wa haki?

Inawezekana watawala wanajua kuwa siyo wasafi? Kwamba hawana sifa isipokuwa ghiliba? Kwamba hawakubaliki isipokuwa kwa shinikizo? Kwamba hawawezi kumudu kushindanishwa na wengine mpaka kuwepo mwanya wa kukiuka taratibu, kanuni na sheria?

Kama kwamba hilo halitoshi, maandalizi ya uchaguzi yanakabidhiwa kwa tume iliyiochaguliwa kwa utashi binafsi wa rais. Ni tume hii inayopewa mamlaka kisheria ya kuandaa, kusimamia uchaguzi na kutangaza mshindi.

Hili tuliangalie hivi: Msimamizi wa uchaguzi ni mteule wa rais. Yule ambaye mteule wa rais atatamka kuwa ndiye mshindi, basi ndiye huyo. Huyo aliyetangazwa hapaswi kupingwa mahakamani.

Hii maana yake ni nini? Ni kwamba tume ya uchaguzi imepewa madaraka makubwa sana kiasi kwamba inaweza “kuchagua” nani awe rais; na ikiishatamka, basi aliyetangazwa hawezi kulalamikiwa mahakamani.

Kuna mwanya mdogo. Mlalamikaji aweza kulalamikia tume kwa kutofuata kanuni, taratibu na sheria; au kwa watendaji wake kukiuka sheria. Mahakama yaweza kutolea maamuzi malalamiko hayo.

Lakini hakuna uwezekano wowote kwa maamuzi hayo kumwondoa madarakani rais aliyepatikana kwa rushwa, wizi wa moja kwa moja; kwa fedha za mafisadi au kwa udanganyifu.

Faida pekee ya njia hiyo ni kuweka wazi kilichotendeka; nani walitenda nini na uhusiano kati ya yaliyotendekake na aliyetangazwa kuwa rais.

Kila baada ya uchaguzi mkuu, waliochaguliwa wamekuwa wakiapa kulinda katiba hiihii yenye upogo; ambayo ina uwezekano wa kuleta viongozi waliopatikana kwa njia chafu lakini hawawezi kuhojiwa mbele ya mahakama.

Si hayo tu, katiba ya Tanzania imejaa vipengele ambavyo havilingani na mazingira ya sasa ya mfumo wa vyama vingi.

Moja ya mifano inayotajwa mara kwa mara ni pamoja na ule wa katiba kutaja kuwa hii ni nchi ya “kidemokrasi na ya kijamaa.”

Hoja zinajengwa: Iko wapi demokrasi katika mazingira ya kukatalia mahakama kusikiliza malalamiko kuhusu aliyetangazwa kuwa mkuu wa nchi?

Ujamaa ni itikadi. Uko wapi utekelezaji wa itikati ya ujamaa chini ya utawala wa CCM?

Tunachoona ni uwezeshaji, kwa kauli, taratibu, kanuni na sheria wa makampuni na mataifa ya nje, kuingia nchini na kuvuna kana kwamba ni “shamba la bibi.” Hakuna ujamaa hapa.

Kwa msingi huo, CHADEMA wanapojaribu kuweka wazi, kilio chao na cha wananchi kuhusu umuhimu wa katiba mpya na tume huru ya uchaguzi, hakika wanastahili kusikilizwa.

Wasiposikilizwa wanatafuta njia mwafaka, kama ile ya juzi bungeni, ambako rais, watawala wenzake, wageni rasmi walipata ujumbe wa moja kwa moja; bila kuchujwa.

Bali bahati mbaya, wenye fikra za John Chiligati, Katibu mwenezi wa CCM, wanajitokeza na kudai kuwa CHADEMA wanataka kuleta “uvunjifu wa amani.” Kwa kudai katiba mpya na tume huru?

Nani hapa anatishia uhuru, umoja, amani na utulivu wa nchi, kama siyo yule anayelinda katiba iliyopitwa na wakati na ambayo wananchi wana kiu ya kuibadilisha lakini bila mafanikio.

Ni halali kusema hapa, kwamba kuendelea kuwa na katiba kama hiyo na sheria kandamizi, ndiyo kuvunja umoja, kuangamiza amani na kupoteza utulivu.

Ni sahihi kabisa kuanza sasa kuandika majina ya wote wanaong’anga’ania hali hii ya hatari – ya kuendelea kuwa na katiba iliyopitwa na wakati na isiyokidhi matakwa ya wengi – na kuyawasilisha mahakama za kimataifa.

Hii ni kwa kuwa ikitokea amani ikavunjika, wawe wa kwanza kuhojiwa kwa kusababisha hali hiyo. Kwa leo, tuanze kwa kufikiria kupeleka jina la John Chiligati.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: