Katibu Mkuu Afya lawamani


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 19 May 2009

Printer-friendly version
Atuhumiwa kusababisha hasara serikalini
Blandina Nyoni

KATIBU Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni ametengua uteuzi wa Mwambata wa Afya katika ubalozi wa Tanzania nchini India katika mazingira ya kutatanisha, MwanaHALISI limeelezwa.

Tarehe 6 Agosti 2008, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Wilson Mukama alimteua Daktari Msaidizi Mwandamizi katika wizara hiyo, Edward Sawe, kuwa Mwambata wa Afya nchini India.

Taarifa zinasema uteuzi wake ulitenguliwa miezi minane baadaye kwa madai kuwa Dk. Sawe hakuwa na “sifa za kushika nafasi hiyo.”

Tayari uamuzi wa Nyoni umeisababishia serikali hasara ya dola 25,000 (sawa na Sh. 30 milioni) zilizolipwa kwa ajili ya pango la nyumba mjini New Delhi ambako Dk. Sawe angeishi na familia yake. Nyumba hiyo ilipangwa tangu tarehe 1 Oktoba mwaka jana.

Gazeti hili limepata taarifa kuwa tarehe 6 Januari 2009, Nyoni alimuandikia barua Dk. Sawe kumtaka aripoti Ofisi ya Damu Salama (National Blood Transfusion Services) wakati akisubiri kukamilika kwa mipango ya safari.

Lakini miezi mitatu baadaye Nyoni alimwandikia Dk. Sawe na kumweleza kuwa hakuwa na sifa ya kushika wadhifa huo.

Barua ya Nyoni kwa Dk. Sawe inasema, “…Baada ya kupitia wasifu wako, imeonekana kwamba haukidhi matakwa ya kuwa Mwambata wa Ubalozi kuhusu masuala ya Afya nchini India...Kwa msingi huo, tutakupangia kazi nyingine hivyo uripoti kwa katibu mkuu kwa kupangiwa kazi nyingine.”

Akizungumza na MwanaHALISI wiki iliyopita, Nyoni alikiri kutengua uteuzi wa Sawe, lakini alisema hatua hiyo haikulenga kubeba mtu, bali kwa sababu “Serikali inataka kupeleka mtu mwenye sifa.”

“Uteuzi wake umetenguliwa kwa mujibu wa kanuni za utumishi. Mimi kama mwajiri ndiye ninayepanga kazi. Hivyo ndivyo nilivyofanya kwa Sawe. Kule India, hatupeleki karani. Tunapeleka daktari bingwa ili kutimiza lengo lililokusudia,” alisema kwa sauti ya ukali.

Nyoni alisema daktari anayehitajika ni yule atakayeweza “kujadiliana na madaktari wa India ili kujua wagonjwa tunaowapeleka wanahitaji huduma gani na kuhakikisha wanahudumiwa kutokana na magonjwa yanayowasumbua.”

Alikuwa akijibu hoja kwa nini Dk. Sawe ambaye amekuwa katika kitengo cha kusafirisha wagonjwa wa Tanzania kwenda nchi za nje asiweze kuwa na sifa za kuwa mwambata wakati kazi hiyo haihusishi ubingwa katika tiba.

Alipong’ang’anizwa kutoa maelezo zaidi kuhusu mashaka yake kwa Dk. Sawe, na kwa nini Mukama aliona anafaa au yeye alitaka kuweka “mtu wake,” Nyoni alisema “Naomba uje ofisini kwangu tuzungumze.”

“Ninakuheshimu sana kwa sababu ya msimamo wako. Siwezi kuzungumzia mambo ya ajira katika simu. Nakuomba uje ofisini kwangu tuzungumze,” alisema kwa upole.

Alisema, “Kaka yangu hapa kuna majungu mengi sana. Watu wa hapa hawataki mtu wa kuwasimamia. Kuna majungu kila kona hapa. Watu wananisakama. Nakuomba usiingie huko.”

Alipoambiwa kwamba tayari kuna madai kuwa ameteua “mtu wake,” mwanamke aliyetajwa kwa jina la Dk. Chale na ambaye hana sifa ya kushika nafasi hiyo kwa kuwa si mtumishi wa serikali, mara hii Nyoni aling’aka akisema:

“Hapana. Njoo hapa, nitakuonyesha CV zake. Ni mtumishi wa serikali. Huyu unayemtaja yupo Muhimbili (Hospitali ya taifa). Anafanya kazi pale kama daktari bingwa,” alisema.

MwanaHALISI ilimuuliza Mukama kutaka kujua iwapo aliteua mwambata asiyekuwa na sifa, naye alisema, “Muulizeni mhusika. Mimi sipo huko tena.”

Taarifa za ndani ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Hazina zinasema Sawe alishagharamiwa safari pamoja na familia yake kwenda India na kwamba alijulishwa usitishaji dakika za mwisho.

Sawe alijulishwa mabadiliko baada ya kusubiri ruhusa ya Nyoni kwa muda mrefu kinyume na matarajio yake kwa kuwa mipango mingine ilikuwa imekamilika ikiwemo mkewe kupata likizo kazini kwake.

Daktari mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe aliiambia MwanaHALISI kuwa kazi ya mwambata haihitaji daktari bingwa. “Hiyo itakuwa kupoteza mtaalamu anayehitajika zaidi nchini. Hapa anahitajika daktari wa kawaida anayemudu kutambua magonjwa mbalimbali,” amesema.

Uzoefu unaonyesha kwamba madaktari wanaofuatana na wagonjwa waliotoka nchini huwa hawatibu isipokuwa kutoa maelekezo tu ya historia ya mgonjwa na kuratibu tiba yake itakavyokuwa inafanyika.

Serikali imeamua kuteua daktari wa kushughulikia jukumu hilo nchini India kwa vile ndiko wagonjwa wengi wanakopelekwa baada ya tiba zao kushindikana kwenye hospitali za nchini.

Tanzania inapeleka wagonjwa wengi wa maradhi mbalimbali kila mwaka nchini India.

Uteuzi wa mwambata wa afya unafuatia ziara ya Makamu wa Rais, Mohammed Shein nchini India, Machi mwaka jana alipoagiza ubalozi uwe na ofisa wa kushuhgulia masuala ya afya (Medical Attache).

Barua ya ubalozi wa Tanzania mjini New Delhi, Kumb. THC/ND/PF.186 ya tarehe 23 Oktoba 2008 iliyosainiwa na Yahya A. Mhata kwa niaba ya balozi inatoa mchanganuo wa gharama za pango la nyumba ya mwambata.

Kwa mujibu wa barua hiyo, Rupia 80,000 ni pango kwa mwezi na kwa mwaka inakuwa Rupia 960,000, wakati gharama ya wakala wa nyumba ni Rupia 40,000. Jumla ni Rupia 1,000,000 (sawa na dola 25,000 wakati huo).

Barua ya balozi ilikuwa ikijibu barua ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Kumb. AB 226/580/01/114. MwanaHALISI inayo mawasiliano yote kuhusiana na suala hili.

0
No votes yet