Katili wa vita Liberia ageuka mchungaji


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 12 January 2011

Printer-friendly version
  • Yuko tayari kushitakiwa The Hague
JOSHUA Milton Blahyi

JOSHUA Milton Blahyi sasa ni mchungaji. Anaombea waumini wa kabila lake la Krahn nchini Liberia. Anataka wapone kutokana na masahibu mbalimbali yanayowakabili.

Akiwa na umri wa miaka 39 sasa, Blahyi anasema yupo tayari kupelekwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa kivita (ICC) iliyoko The Hague, nchini Uholanzi, ili kujibu mashitaka ya ukatili alioufanya kwa miaka kadhaa.

Alitumikia jeshi la uasi lililokuwa likipigana na serikali ya Liberia tangu akiwa na umri wa miaka 11 kama mmoja wa maelfu ya watoto waliopewa mafunzo ya kijeshi na kujumuika katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Ni mwaka 1982 na ikiwa inaingia magharibi, watu wa kabila lake la Krahn wanajiandaa kumsikiliza (mchungaji wao) akianzisha maombi.

Sauti ya nguvu inaanza kusikika. Anajitenga na walipo waumini. Anasimama madhabahuni. Hana nguo.

Waumini wazee wanamsindikiza msichana mdogo, wanamvua nguo na kumpaka udongo mwilini, mchungaji naye anamsinga.

Maombi yanayodumu kwa siku tatu, yanaishia kwa moyo wa msichana huyo na viungo vyake vingine vya mwili kuondolewa. Ni chakula. Bado katika kipindi hicho, Mchungaji anaamini anayo dira mahsusi: anakutana na shetani anayemwambia atakuwa shujaa mkubwa.

Anasema ili kuongeza nguvu yake, anahitajika kuendelea kuombea watoto na kula nyama zao. Sasa maombi yamekamilika. Mchungaji amekuwa miongoni mwa viongozi wenye nguvu kubwa katika Afrika Magharibi.

Mchungaji ana umri wa miaka 11. Mchungaji huyu mvulana amekua ili kuja kuwa mmoja wa wapiganaji wa vita wabaya kabisa. Ni jenerali aliyejianika hadharani.

Yeye na wanajeshi wake watoto wanaingia vitani wakiwa hawana nguo zaidi ya viatu na bunduki. Kazi ya maombi aliyoifanya kwa miaka 11 na ya kwanza maishani mwake ilimpelekea kuua karibu watu 20,000 na leo anaungama kwa kuhusika na mauaji hayo na kuwa tayari kushitakiwa.

Wapinzani wake wanapinga idadi hiyo wakisema hawezi kuithibitisha.

Lakini, wakati huohuo, kinachobishaniwa ni kwamba katika kipindi cha miaka 14 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe Liberia, jenerali huyo alikuwa mmoja wa wanajeshi katili kupindukia katika historia ya vita barani Afrika.

Baada ya mwenyewe kukiri mbele ya Tume ya Ukweli na Maridhiano ya Liberia (LTRC) mwaka 2008, kuhusika na matendo katili, mwanablogu mmoja aliuliza:

Hivi huyu ndiye mtu katili mkubwa aliyewahi kuwepo?

Uhalifu aliofanya ukihusisha kupiga kafara watoto, kula nyama ya binadamu, kugeuza watoto kuwa ni wanajeshi na kuuza dhahabu ili kupata silaha na madawa ya kulevya, ambayo aliwalisha watoto hao askari wakiwemo wenye umri wa miaka tisa.

Leo, anajitambulisha kama mtu aliyerudi kwa mola: ameokoka. Julai 1996, alifanya sherehe ya majusi – sherehe kuhusu elimu ya sayari.

Miaka 14 ndani ya matendo mabaya dhidi ya binadamu, jenerali alijiwa na wahyi akitakiwa akome kuua na aungame na kutubu au aendelee na kusulubiwa.

Huyo ndiye anaitwa Joshua Milton Blahyi. Ameoa na ana watoto watatu. Anaishi maisha ya kichungaji.

Anasema iwapo alibadilika, hakuna asiyeweza kubadilika. Sasa anahimiza kukoma migogoro ya kikabila inayohusisha watoto wadogo, mauaji ya kikatili na ulaji wa binadamu. Anaamini matendo hayo yanaendelea Liberia.

Tume ya Ukweli na Maridhiano ya Liberia iliyoundwa kuchunguza matukio ya kikatili wakati wa vita, ilitoa ripoti yake mwaka 2009 na kushauri Blahyi asamehewe kwa sababu ameungama kijasiri.

Katika mahojiano na gazeti la The Mail on Sunday la Uingereza, Blahyi anasema yuko tayari kushitakiwa ICC.

Anafichua siri ya ukatili wanaofanyiwa watoto wakati wa vita pamoja na vitendo vya majenerali kula nyama ya mtu kama matendo aliyoshiriki – na kwamba amebadilika.

Anapokiri kushiriki matendo ya kikatili anazusha hoja ya kama ni sahihi mtenda maovu kama huyo kustahili kusamehewa. Binafsi anajiuliza.

Ukiacha Ethiopia, Liberia ndiyo nchi pekee ambayo asili ya watu wake haitokani na wakoloni wa Europa. Ilibainika na kutawaliwa na watumwa wa Kimarekani katika miaka ya mwanzo ya 1820.

Ila, historia yake ya miaka mingi baadaye, imegubikwa na gharika ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kati ya mwaka 1989 na 2003, vita vya kikabila vilisababisha vifo vya watu 250,000 na zaidi ya milioni moja kuhama makazi na kugeuza mmoja katika kila watoto watano kuwa ni askari.

Wakati wa vita, Liberia ilikuwa kituo kikuu cha biashara ya kubadilishana almasi na silaha, madawa ya kulevya na kuimarisha vita kwa kutumia fedha zinazotokana na mtandao wa kigaidi wa kundi la Al Qaeda.

Ukosefu wa amani ulioikumba Liberia kwa muda mrefu umeambukiza nchi nyingi jirani yake na zaidi ya hapo.

Blahyi alikuwa mmoja wa mabwana wakuu wa vita akipigana na makundi ya askari wa msituni wakiwemo walioongozwa na Charles Taylor, aliyekuja kuwa Rais wa Liberia na ambaye sasa anakabiliana na mashitaka ya uhalifu wa kivita The Hague.

Wakati wa mahojiano, Blahyi alikutwa hoteli ya maeneo ya mavumbi ya Zeos, masafa ya dakika 15 kwa gari kutokea Monrovia, mji mkuu wa Liberia.

Alichagua kuishi hapo kwa kuwa baada ya kuelezea matendo hayo mbele ya Tume ya Ukweli na Maridhiano, alianza kupokea vitisho vya kuuawa. Mwandishi aliyemhoji anasema ilimchukua miezi kadhaa kufanikiwa kumpata Blahyi kwani alikuwa akiishi mafichoni baada ya tishio la kuuawa.

Mwandishi anasema aliipata namba yake kutoka kwa mtaalamu wa filamu wa Kiliberia anayeishi mjini New York.

Muitiko wa simu ulikuwa wa kuogofya. Lakini alipofahamu anayempigia, Blahyi alichangamka na kuendelea kuongea kirafiki. Baadaye, alikuwa akipiga mara kwa mara simu ya mwandishi huyo.

Maelezo ya Blahyi yatajumuishwa katika igizo la Mmarekani litakalotangazwa wakati wa tamasha la filamu la Sundance mwaka huu.

Kilichomvutia mwandishi ndicho kilichovutia watengeneza filamu: Inawezekana kweli mtu anayedai kushiriki maovu makubwa akabadilika na kuwa mchungaji?

Blahyi anaomba msamaha, anaumia kwa matendo aliyoyatenda nyuma, anahofia adhabu kwa mola; na mara nyingi anasikitika na kukata tamaa. Ana akili sana, juburu na mchangamfu.

Bali kwa alivyo, ametukanika.

Umbo lake linajieleza. Ameacha jeshi zaidi ya muongo mmoja, lakini sura yake ingali inatisha sana. La pili ni macho yake – akifikiria kile alichotenda, anajisuta.

Tumeketi baa. Tunatembea kando ya barabara. Yeye anakunywa mvinyo usio ulevi.

Mabega na mikono yake imebana kwenye fulana yake ya khaki. Anapoguswa na jambo fulani, anashtuka haraka, uso wake unasawijika. Ni kuonyesha uzito wa jambo lenyewe kila akilikumbuka.

Wakati fulani, anagonga chupa mezani tulipoketi. Bila ya kuniangalia, anaivunja na vipande kutawanyika chini. Misuli yake inabaki madhubuti daima.

Alikuaje utotoni kwake? Anaeleza alivyoambiwa na baba yake, halafu alivyosimuliwa na babu zake namna alivyozaliwa kuwa shujaa.

Kwa simulizi za mababu, alichukuliwa kutoka kwa mama yake baada tu ya kuzaliwa. Akiwa na miaka saba, baba yake alimkabidhisha kwa mababu waliomfundisha namna ya kuendesha maombi.

Baada ya kufundwa kiimani, alikuwa kijana shababi ambaye watu wa kabila lake walimheshimu sana.

Mwaka 1982, akiwa mchungaji umri wa miaka 11, Blahyi anakumbuka alivyokuwa akiendesha maombi kwenye makao ya rais wa Liberia wakati huo, Samuel Doe ili kumkinga na maadui.

Doe naye alikuwa na asili ya kabila la Krahn; na aliingia madarakani kwa mapinduzi ya umwagaji damu ya mwaka 1980.

Mwaka 1990, alikamatwa kwenye Ikulu na akauawa na majeshi ya kiongozi wa waasi – tukio lililozidisha mgogoro ambao ulimalizika miaka 13 baadaye.

Muda wote huo, Blahyi alikuwa mchungaji mkubwa. Moja ya kazi zake kuu ni kuendesha maombi kwa kutoa watoto kafara na kula watu.

Nchini Liberia leo, asilimia 75 ya watu wake ni Wakristo, asilimia 20 ni Waislam na waliobaki wanafuata dini za makabila yao zinazoamini katika maombi.

Lakini wakati wa vita, wataalamu wanadai kuwa watu wengi hujishirikisha katika maombi yanayozingatia makabila yao.

Katika kitabu chake kiitwacho The Mask Of Anarchy, Profesa Stephen Ellis wa Chuo Kikuu cha Free University, mjini Amsterdam, anathibitisha hiyo ndiyo ibada kuu inayofanywa na makabila wakati wa vita.

0
No votes yet