Katu hatukubali Kunyamazishwa


editor's picture

Na editor - Imechapwa 20 October 2010

Printer-friendly version

KATIKA ukurasa wa mbele wa gazeti hili tumechapisha tishio la serikali kutaka kutufunga mdomo. Kinachoonekana katika tishio hilo, ni serikali kuishiwa uvumilivu na sasa imeamua kufanya kazi isiyoihusu.

Imepanga kufunga chombo hiki cha habari na vingine ambavyo vimekataa kulamba viatu vya watawala.

Gazeti jingine lililohatarini kufungiwa au kufutiwa usajili ni Mwananchi.

Kisingizio kinachotumiwa na serikali, ni gazeti kuandika habari za uchochezi zinazolenga kuhatarisha usalama wa taifa.

Kwa upande wa gazeti hili, onyo la serikali linakuja baada ya kuandika habari iliyokuwa na kichwa kisemacho, “Njama za Kuiba Kura Hizi Hapa.”

Habari hiyo ya uchunguzi, ilikuwa inaeleza kuhusu taarifa kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefanikiwa kupenyeza wachakachuaji kura katika mchakato wa kupiga na kuhesabu kura uchaguzi mkuu ujao.

Gazeti lilisema, mpango wa kuchakachua matokeo utafanywa kwa ustadi mkubwa kwa ushirikiano na kitengo cha IT katika ofisi isiyo rasmi ya CCM iliyopo Mtaa wa Undali, Upanga, Dar es Salaam.

Kazi nzuri iliyofanywa na gazeti hili, ni kutoa taarifa za kuwepo tuhuma dhidi ya CCM, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na usalama wa taifa. Tulisema huu ni uvumi na umeenea nchini. Basi!

Kutokana na ujasiri wa kufichua njama hizo, tulistahili pongezi kutoka kwa wote wanaolitakia mema taifa hili, badala ya kutuhumiwa kufanya “uchochozi.”

Tunaendelea kusisitiza tena, kwamba tulichokiandika ni tuhuma; taaluma inatuelekeza kuwa hata uvumi ni habari.

Lakini uvumi ukibaki ukijulikana kwa wachache, wakati unahusu na una uwezo wa kuathiri wengi; na ukabaki bila kushughulikiwa, unaweza kuwa na madhara makubwa na mapana kwa jamii.

Tunachokiona sisi, serikali inataka kutumia mabavu kutunyamazisha. Inataka kuua chombo hiki cha wananchi. Hata ilipoamua kutumia mabavu kutufungia mara ya kwanza, Oktoba 2008, bado tunaamini kuwa hatukuwa na makosa.

Hivyo basi, tunaiomba serikali isijiruhusu kutumiwa na wasiolitakia mema taifa hili. Ifanye kazi zake kwa mujibu wa taratibu. Taifa hili ni letu sote, hivyo hatukubali kunyamazishwa.

0
No votes yet