Kauli ya Rostam Aziz haivurugi serikali?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 18 November 2009

Printer-friendly version
Gumzo

ZIMWI la mkataba kati ya serikali na kampuni ya Richmond Development Company (LLC) bado linaitesa serikali; lakini zaidi linamzonga Rostam Aziz.

Jumanne iliyopita mfanyabiashara na mbunge huyo wa Igunga, ambaye mara nyingi ametokea kuisemea au kuitetea serikali, alionyesha mkakati mpya wa juhudi zilezile za kale za kuitetea serikali kuhusu Richmond. Anapinga Kamati ya Bunge.

Rostam amenukuliwa akisema, “Yaliyomo ndani ya ripoti ile (ya kamati ya bunge) ni uwongo mtupu.” Hii ni kauli inayokuja miezi 21 baada ya Kamati Teule ya Bunge kuwasilisha ripoti yake na bunge kukubali mapendekezo yaliowasilishwa.

Juni 2006 serikali kupitia aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, iliagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuingia mkataba wa miaka miwili wa kuzalisha megawati 100 za umeme na kampuni ya Richmond. Ni mkataba huu uliomg’oa Lowassa kwenye nafasi ya waziri mkuu.

Rostam anasema msimamo wake wa kupinga ripoti hiyo ulikuwapo tangu pale Kamati ya Bunge ilipowasilisha ripoti yake. Anasisitiza, “Ili mambo yaishe ni vema uchunguzi huru ukafanyika.”

Anasema alitaka kukosoa ripoti ya kamati bungeni, lakini Spika wa Bunge, Samwel Sitta alimnyima nafasi ya kuzungumza.

Kuna nini hapa? Ukimsikiliza Rostam kwa makini utagundua kuwa anataka kushawishi umma kuwa bunge lilimwonea Lowassa, serikali ilidhalilishwa na haki haikutendeka.

Kauli ya Rostam inazaa mashaka. Lowassa yuko kimya, hata kama anaongea kupitia wengine; lakini Rostam anapiga mbiu. Huu ulikuwa mkataba wa nani? Kama ulikuwa mkataba wa serikali, basi hakuna sababu ya Rostam kuendeleza mjadala kwani serikali inajua inachofanya.

Kama ulikuwa mkataba wa Lowassa, basi aache Lowassa ajisemee au aseme alivyohusika kuingiza serikali katika mkataba huo. Kama Rostam anaona anahusika na mkataba huu, lakini yalifanyika makosa ukamponza Lowassa na sasa analazimika kumtetea, basi aseme hivyo dunia ipate kutoa hukumu.

Haitoshi kwa Rostam kuendelea kulalama kwamba Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwe Sitta alimnyima fursa ya kuzungumza bungeni; na kwamba Kamati Teule iliwasilisha ripoti yake bila ya yeye na Lowassa kupewa nafasi ya kujitetea.

Kinacholeta mashaka zaidi ni kwamba mara nyingi Rostam amesikika akikana kuhusika na Richmond. Amefika mbali na kutaka kushitaki wanaosema anahusika na Richmond. Ni nini hasa kinachomfanya aweweseke na Richmond huku akidai haijui?

Labda anafanya hivyo kwa kuwa aliona kuwa katika ripoti ya kamati ya bunge amesogezwa karibu na wahusika au kama siyo kwa kigugumizi anaona angetajwa moja kwa moja. Lakini hili la kila mara kuonekana anamtetea Lowassa zaidi linatoka wapi?

Ni mashaka hayo ambayo yanafanya wengi waanze kufikiri, kama siyo kuamini, kuwa Rostam anapata presha kutoka sehemu mbalimbali ili ahakikishe anamtetea Lowassa na kwa nguvu zote. Swali dogo ni hili hapa: Kwa nini amtetee? Mbona Lowassa ni msemaji bora kuliko Rostam?

Hata madai ya Rostam yanatoa mashaka. Anasema Spika Sitta na Dk. Harrison Mwakyembe, mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, walitenda kazi zao kwa visasi vya kukosa madaraka.

Hii ina maana gani? Kwamba Rostam alikuwa anagawa vyeo? Au, kwamba alikuwa na uwezo wa kushawishi Rais Jakaya Kikwete kuteua yule ambaye yeye, Rostam alipendelea, alitaka au alihitaji? Wangapi hawana vyeo nchini na wako kimya?

Kauli za Rostam zinatuongoza katika kuamini kuwa kuna kitu kikubwa zaidi. Kwamba Sitta na Mwakyembe walitaka vyeo lakini wakavikosa? Vyeo hivi vinahusika vipi na Richmond? Mbunge huyu wa Igunga aseme jingine; hili halitafuniki.

Kama ingedaiwa kuwa Mwakyembe na Sitta walikataliwa hisa katika Richmond, hilo lingeweza kufanyiwa uchunguzi. Lakini kwamba hawakupewa vyeo ndani ya serikali na kwamba sasa wana visasi na ndiyo maana wakaweka jina la Lowassa na Rostam katika taarifa ya bunge, ni kauli isiyo na mashiko.

Leo hii Sitta ni spika wa bunge la Jamhuri. Ni kiongozi wa moja ya nguzo tatu za dola. Hii ni nafasi kubwa kuliko ya waziri mkuu, hata kwa mizengwe ya kubadili katiba na kufanya waziri mkuu awe anachukua nafasi ya rais pale rais au makamu wake wasipokuwepo. Iweje kuwe na kisasi cha kuchukua nafasi ya chini?

Inawezekana Rostam anataka kusema kuwa yeye na Lowassa waliwanyima akina Sitta na Mwakyembe nafasi za juu katika uongozi? Je, walitaka kuwapa nafasi gani; ya urais? Mbona rais alikuwepo tayari? Makamu wa rais? Mbona anapatikana kwa njia tofauti kabisa na siyo kwa upendeleo wa mfanyabiashara wa Igunga?

Lakini Rostam bado anaendeleza mjadala nyaufu kwamba alinyimwa fursa ya kuzungumza bungeni. Kwanza, kanununi za bunge zinaruhusu mbunge kuwasilisha hoja binafsi ya kupinga maelezo ya Kamati Teule mara kamati inapomaliza kuwasilisha ripoti yake.

Kanuni ya 60 (13) ya kanuni za bunge inatoa uhuru kwa mbunge kutoa maelezo bungeni ya kupinga ripoti au taarifa ya Kamati Teule. Hakuna mahali popote katika kumbukumbu za Bunge panapoonyesha kuwa baada ya ripoti kuwasilishwa bungeni, Rostam au wabunge wengine waliwasilisha hoja kupinga ripoti iliyowasilishwa.

Badala yake, kumbukumbu zinaonyesha kuwa Rostam alikuwa miongoni mwa wabunge zaidi ya 45 waliochangia ripoti ya kamati. Mchango wake aliuwasilisha kwa maandishi na ulinukuliwa ndani ya bunge na Dk. Mwakyembe.

Hivyo basi, madai kwamba alizuiwa kuzungumza bungeni, ama yanalenga kuficha ukweli au anataka kuhamishia tatizo kwa wengine. Hadi sasa, si Rostam mwenyewe wala wapambe wake waliosikika wakisema kuwa walichangia kwa maandishi kwa kuwa walinyiwa fursa ya kuongea.

Hata baada ya bunge kutoa maazimio yake, bado Rostam au mbunge mwingine yeyote aliyekuwa anaamini kwamba kuna mtu ameonewa au ripoti haikuwa sahihi, alikuwa na nafasi ya kueleza hilo bungeni.

Hii ingefanywa kupitia Kanuni ya 64 (1) ambayo inaruhusu mbunge kujadili jambo lililojadiliwa na kutolewa maamuzi katika mkutano unaoendelea au uliopita.

Kilichotakiwa kwa mbunge ni “kutoa hoja mahususi inayopendekeza kupitiwa upya uamuzi wa awali.” Sasa ni karibu miaka miwili; si Rostam wala wapambe wake waliowasilisha hoja hiyo bungeni.

Vilevile Rostam hajatumia kanuni ya 150 (1) inayosema, “Kanuni yoyote ya Bunge hutenguliwa kwa idhini ya Spika.” Katika mazingira hayo, hoja ya Rostam ya kutaka kuundwa jopo la majaji watatu inatoka wapi?

Nimesoma Kanuni za bunge na kujiridhisha kuwa kuna njia nyingi ambazo Rostam angechukua ndani ya bunge kufikia anakotakwa kwenda. Ni hapo ninapojiuliza, vipi mwanasiasa huyu ashindwe kutumia fursa zilizopo bungeni na badala yake akimbilie tume ya majaji?

Wala Rostam kwa uzoefu wake wa kuwapo bungeni kwa muda mrefu, hawezi kusema kuwa hafahamu kanuni hizi za bunge zinazoruhusu jambo hili kurudishwa tena bungeni. Anazifahamu tena vizuri sana .

Rostam amekuwa bungeni tangu mwaka 1994 kabla ya hata bunge la kwanza la vyama vingi kuwapo. Kanuni nyingi za sasa zinazotumika bungeni zimetungwa baada ya serikali kuruhusu mfumo wa vyama vingi.

Hivyo kwa ukongwe huu, na kwa yeye kushiriki kutunga na kupitisha kanuni na sheria mbalimbali zinazotumika sasa, Rostam hawezi kusema kuwa hajui kinachotendeka ndani ya bunge.

Bali ni wazi kwamba Rostam si msemaji bungeni. Ni “mbunge bubu.” Si katika mambo ya Richmond tu, bali hata katika mambo mengine yanayohusu wapigakura wake wa Igunga.

Kumbukumbu za bunge zinaonyesha kuwa Rostam hazungumzi, haulizi maswali na ikibidi huwasilisha mchango wake kwa maandishi. Inawezekana ni kwa msingi huo, ndiyo maana anatafuta mahali pakuibukia.

Kanuni ya 60 (8) “Mbunge yeyote haruhusiwi kusoma maelezo bungeni, isipokuwa kwa madhumuni ya kutilia nguvu maelezo yake.” Inawezekana hapa ndipo ilipo siri ya Rostam.

Hicho ambacho Rostam anatuhumu Sitta kukizuia kupelekwa bungeni ni “maelezo binafsi.” Haya hayawezi kutolewa kiholela bila kufuata kanuni za bunge.

Tayari suala la Rostam kutohojiwa na Kamati lilishaelezwa na Kamati ya Mwakyembe; kwamba alitumiwa wito wa kuitwa mbele ya Kamati, lakini hakutokea.

Lakini kamati ilisisitiza kwamba haikuona umuhimu wa kumuita Lowassa kwa sababu (kwa kujua tabia na utendaji wake) angeingilia uchunguzi uliokuwa unafanywa, ambao ulishaonyesha kwamba yeye ni sehemu ya tatizo.

Hata hivyo, Lowassa alipewa nafasi ya kujitetea mara baada ya kamati kuwasilisha ripoti yake; lakini hakufanya hivyo. Alizuia hata mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba aliyetaka kumtetea.

Serukamba aliposimama bungeni kujenga hoja, kuwa Lowassa hakutendewa haki, haraka Lowassa aliinuka na kusema, “Hilo nitalizungumza mwenyewe wakati nitakapopewa nafasi.”

Lakini ilikuwa ni kinyume chake. Alipopewa nafasi ya kujieleza, Lowassa aliishia kujiuzulu. Alituhumu kila mmoja, “…tatizo ni uwaziri mkuu.”

Kuhusu hoja ya Kamati ya Bunge kudhalilisha serikali kwa “maslahi binafsi ya kisiasa,” hakika hili siyo la Rostam kujadili. Hii ni kwa sababu, tayari sasa imethibitika kwamba ripoti hii ilipelekwa kwa Rais Kikwete kabla ya kuwasilishwa bungeni. Naye rais aliiona. Aliisoma ukurasa kwa ukurasa.

Urais ni taasisi. Rais ana vyombo vyake na vyombo vingine vya dola. Bila shaka alivishirikisha katika kusoma ripoti hiyo. Asingekubali ripoti hiyo ipelekwe bungeni kama asingekuwa amejiridhisha kuwa ina ukweli wa kutosha ndani yake.

Kama ripoti ingekuwa inavunja hadhi ya serikali, basi ingezimwa palepale kwa rais na kutupwa kapuni. Haikutupwa na kamati haijawahi kulalamika kuwa iliingiliwa na rais katika utendeaji wake. Kwa ufupi basi, ripoti ilikuwa inajenga; ilikuwa inainua uso wa rais mbele ya wananchi.

Katika mazingira hayo, Rostam anapata wapi uwezo wa kudai kuwa “ripoti ilidhalilisha serikali,” wakati mwenye serikali yake hajasikika kulalamika?

Madai mengine ya Rostam kwamba ripoti iliyowasilishwa haikuwa na vigezo vinavyostahili, nayo yanatia mashaka. Hivi katika hili, nani anapima vigezo? Ni Rostam au bunge?

Kama ripoti ya bunge haikuwa na vigezo, kwa nini rais aliikubali? Je, ripoti isiyokuwa na vigezo inawezaje kumuondoa “mwanamme wa shoka” katika madaraka – kwa mujibu wa kauli za “kicheni pate” za waziri Sofia Simba?

Ukiangalia kwa undani zaidi utaona kuwa Rostam anataka kusema kuwa bunge lilipitisha azimio kwa ripoti feki. Kama hivyo ndivyo, basi hayo ni matusi kwa bunge ambamo mbunge huyuhuyu ni mtunga sheria.

Kinachoonekana hapa ni kimoja. Rostam anataka kuaminisha umma kuwa wabunge wanaweza kuzushiana uwongo, kufitiniana na hata kuhujumu serikali. Ana kazi ngumu ya kuthibitisha haya.

Wala hapa si mahali wala wakati wa kuunda majopo ya majaji; na hakuna atakayekubaliana naye katika hilo. Katika mazingira ya sasa Rostam ana njia mbili za kufanya.

Jopo la majaji huundwa pale tu rais anapotaka kumchunguza Jaji husika, kumwachisha kazi kwa kukosa sifa.

Kwanza, kuwasilisha hoja bungeni kutaka mjadala huu uanze upya. Pili, kufungua shauri la kikatiba mahakamani. Huko aweza kushitaki mwanasheria mkuu wa serikali, Spika na hata akipenda mwenyekiti wa Kamati Teule. Ubavu huo anao?

Rostam asubiri ripoti ya serikali ya utekelezaji wa maazimio ya bunge kuhusu wote waliohusika na mkataba wa Richmond. Ni mkutano ujao wa bunge. Huko aweza kusema atakacho.

Lakini tatizo kubwa la Rostam ni kujiona kuwa yeye ni ana uraia wa viwango vya juu kuliko wengine. Anajiona mbia katika utawala wa Kikwete. Na kwa kuwa karibu na rais, anadhani ana kinga kama ile aliyonayo rais.

Vinginevyo, haingii akilini Rostam kushinikiza kuundwa jopo la majaji, wakati hilo halipo katika kanuni za Bunge. Hapa anamshinikiza nani kama si rais?

Na hili si yeye tu. Hata wasaidizi wengine wa rais na wale wanaojitangaza kuwa maswahiba wa Rais Kikwete, wapo kama alivyo Rostam.

Hoja hii inaleta hisia kwamba Rostam anazidi kujibanza kwa Kikwete na kumtumia kama kinga. Bahati mbaya, anafanya hivyo wakati rais na wasaidizi wake wanafanya jitihada kuaminisha umma kwamba Rostam si mwenzao tena.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: