Kawambwa anapwaya mno Elimu


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 09 February 2011

Printer-friendly version
Tafakuri
Shukuru Kawambwa

NILIKUWA miongoni mwa watu waliohoji sababu za msingi za Dk. Shukuru Kawambwa kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi alipoteuliwa mwaka jana baada ya uchaguzi mkuu.

Sikuhoji kwa sababu simjui Dk. Kawambwa, ila ni kwa sababu kwa miaka mitano ambayo mwanasiasa huyu amekuwa kwenye baraza la mawaziri, kuanzia 2006-2010, hakuwa na lolote la maana la kujitambulisha nalo kama mafanikio licha ya kuongoza wizara tatu tofauti.

Ngwe ya kwanza ya serikali ya awamu ya nne, Dk. Kawambwa aliongoza wizara tatu tofauti, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo; Waziri wa Maji; na Waziri wa Miundombinu. Kote alikopita, hana alichoacha kama kielelezo cha utendaji na uwajibikaji uliotukuka. Hana!

 Ukitafakari kwa kina utafikia hitimisho moja tu, kwamba Dk. Kawambwa mbali ya kuwa mwanasiasa ambaye ameibukia kwenye anga hizo baada ya kuwa katika anga za taaluma kwa muda mrefu, ni kama mtu anayelazimishwa kucheza mchezo wa siasa ambao kwa kweli hautaki na kama anautaka haumudu.

Hakuna ubishi kuhusu wasifu wa Dk. Kawambwa; huyu ni msomi wa ngazi ya juu si kwa viwango vya Tanzania tu bali duniani kwa ujumla, ana shahada tatu, ni mwerevu wa mambo. Lakini katika utendaji wake kama mwanasiasa kila nikimtazama nashindwa kujua kilichomsukuma Rais Kikwete kumpa nafasi ya uwaziri mara nne.

Ukitafakari zaidi mfululizo wa matukio ya migomo ambayo imekumba vyuo vya elimu ya juu tangu kuanza kwa mwaka huu, hakuna ubishi kwamba Waziri Kawambwa ameachwa gizani au tuseme alikuwa ameupiga usingizi wa pono.

Hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na Waziri Kawambwa mgomo wa kwanza ulipoibuka katika Chuo Kikuu cha Dodoma, hakuna alichofanya hata ilipoibuka migomo mingine kwenye vyuo vikuu vishiriki vya elimu vya Mkwawa na Dar es Salaam, lakini pia hata katika kero ya kushindwa kuwapangia walimu wapya vituo vya kazi ambao walivamia ofisi yake na yeye kuwakimbia bila hata kuwaambia chochote wakiwa mbele ya jengo la Wizara yake jijini Dar es Salaam wiki mbili tu zilizopita.

Nieleweke mapema tu kwamba sina nongwa yoyote na Dk. Kawambwa, ninamwona kama mtu mwadilifu, mpole na asiye na makuu, lakini kwa bahati mbaya nafasi aliyopewa safari hii kama ile ya Miundombinu aliyopewa, haitaki mtu mpole.

Wizara ya Elimu ni mshipa mkuu wa fahamu wa taifa. Ni wizara nyeti kuliko inavyoweza kuelezwa. Hapa anatakiwa mtu asiyepepesa macho, anayeweza kumwambia yeyote katika hili umeboronga basi tupishe.

Mwaka huu matokeo ya kidato cha nne waliofanya mtihani wao wa taifa mwaka jana mwishoni, yamethibitisha jinsi taifa hili linavyoelekea katika maangamizi makubwa; ni jambo la kushangaza kuona kwamba katika wanafunzi laki tatu na ushei waliofanya mtihani, ni asilimia 11 tu walifaulu, asilimia 88 ushei walifeli kwa maana ya asilimia 50 kupata daraja sifuri na zaidi ya asilimia 38 kupata daraja la nne, ambalo kimsingi halina tofauti sana na sifuri.

Hali hii inaamsha hofu juu ya mustakabali wa taifa hili katika mambo mengi, ushindani wetu na mataifa mengine katika majumuiko mbalimbali kama Jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini pia katika ushindani duniani kote.

Wakati tukijiuliza maswali haya, wiki hii Waziri Kawambwa alikwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sehemu ya Mlimani kuwasikiliza wanafunzi waliokuwa wanalalamika kuishi maisha ya dhidi kuu kutokana na kupewa posho ya chakula ya Sh. 5,000 kwa siku.

Kwa bahati mbaya, Waziri Kawambwa alifika Chuoni hapo bila kuwa na mkakati wowote wa maana wa kutatua tatizo hilo ambalo si tu linaathiri ufanisi wa utoaji wa elimu chuoni hapo, ila kwa vyuo vyote vya elimu ya juu ambavyo hupewa mkopo na serikali kupita Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB). Kote huko wanafunzi hawasomi, wanabangaiza, kisa njaa.

Nikimwangalia Dk. Kawambwa nashindwa kujipa matumaini kama ni mwanasiasa wa kuleta mageuzi katika sekta ya elimu nchini kwa sasa hasa changamoto zake zinapotazamwa kwa mapana yake.

Napata hofu zaidi kila ninapoona majibu ya Waziri Kawambwa ni kama yaleyale ya watangulizi wake kwenye wizara hiyo ambao kwa kutokutaka kuwaza kwa mapana manufaa na maana ya elimu, wameamua kuitazama katika mzania wa gharama za matumizi badala ya kuiweka kwenye mzania wa uwekezaji.

Watawala wetu kwa makusudi wameamua kuitazama elimu sawa na mtu anayegharimia vitu vya anasa.

Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba taifa hili kwa kutokujua limetekwa nyara na wanasiasa kiasi cha kukubali kila jambo linaloamuliwa hata kama athari zake ni zahama kwa taifa lenyewe.

Ni kwa maana hiyo unaweza kuona matukio kama haya ya kuporomoka kwa elimu ya watoto wetu kama matokeo ya kidato cha nne yalivyoonyesha na hata katika migogoro yote hii inayotokea katika vyuo vikuu nchini, bado jamii inajiona kuwa haina cha kufanya kubadili hali hii.

Mbaya zaidi ni pale wanasiasa na watawala wanapodhani kuwa wana hati miliki ya kuamua mustakabali wa elimu ya taifa hili hata bila kutaka kutafuta mjadala mpana wa kitaifa.

Kwa hakika katika miaka mitano ijayo kama mageuzi makubwa hayatafanyika kwa kuifanya elimu kuwa kitegauchumi ambacho kinagharimiwa na kodi za wananchi kwa nguvu zote, taifa hili litakuwa kwenye msiba mkubwa. Tutafakari hali hii.

0
Your rating: None Average: 5 (3 votes)