Kawambwa kuwambwa bungeni


Aristariko Konga's picture

Na Aristariko Konga - Imechapwa 30 June 2009

Printer-friendly version
WAZIRI wa Miundombinu, Shukuru Kawambwa

WAZIRI wa Miundombinu, Shukuru Kawambwa leo anatarajiwa kusulubiwa bungeni kutokana na miradi ya wizara yake kuwa na utata mwingi.

Taasisi nne zilizoko chini ya wizara yake ndizo chanzo kikuu cha mazingira magumu, ambayo yanafanya bajeti yake ionekane kuwa ya mzaha au udanganyifu.

Kwanza, ni Kampuni ya Reli (TRL). Hii iliomba Sh. 6.74 bilioni kwa ajili ya mishahara, lakini bajeti ya wizara imetoa Sh. 1 bilioni.

Bado kutakuwa na maswali mengi, kwa mfano, kwa nini TRL ipewe hata hizo fedha wakati menejimenti yake ya kampuni ya RITES kutoka India imeshindwa kazi na haionekani kuwa na mwelekeo wa kuendeleza usafiri wa reli.

Pili, ni Kampuni ya Kupakia na Kupakua Makontena bandarini – Tanzania International Container Terminal Services Limited (TICTS). Kampuni hii imethibitika, kwa viwango vyote, kushindwa kazi.

Wakati Bunge linajadili bajeti ya wizara, kampuni ingekuwa imefukuzwa bandarini tangu mwaka jana.

Notisi ya siku 90 ya kuvunjwa kwa mkataba wake na serikali, iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari, E.N. Mgawe, ilitolewa kwa mara ya kwanza tarehe 5 Mei 2008.

TPA ilisema, kwa mwenendo wake wa utendaji, tayari TICTS ilishavunja mkataba.

Tatu, ni Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL). Kampuni iliomba Sh. 20 bilioni lakini bajeti ya wizara imetoa Sh. 1 bilioni kwa ajili ya madeni na kustaafisha wafanyakazi.

ATCL sasa haina mbawa, kwa maana ya ndege na kuchechemea kwake kunaweza kuzimika wakati wowote.

Nne, ni Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Wakala wanakabiliwa na kupanda kwa gharama za ujenzi; mahali pengine kufikia zaidi ya mara mbili ya bei ya awali.

Aidha, kwa mtindo wa sasa wa wakala kukatisha mikataba ya ujenzi kwa sababau mbalimbali, serikali inadaiwa zaidi ya Sh. 100 bilioni – kiasi ambacho ni mzigo mkubwa katika mazingira ya sasa.

Tayari imefahamika kuwa wale ambao miradi yao imekatishwa, kwa sababau mbalimbali, wameanza kwenda mbele ya sheria na huko wameshinda mashauri yao.

Hatua hii ya serikali kushindwa inaendelea kuisokomeza katika matatizo ambako sharti irejeshe wazabuni, iwalipe fidia na ikubali kuendeleza miradi, tena kwa gharama mpya zilizoongezeka.

“Katika wizara hii tunakwenda kujadili mazingaombwe. Mtu anaweza kufikiri kuwa wazabuni wengine wamesitishwa ili waweze kushinda na kuzawadiwa…” ameeleza mbunge mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyetaka asitajwe jina.

“Nasema hii inaweza kuwa hujuma ya kawaida tu, vinginevyo kuna haja ya kupima hasara na faida kabla ya kuchukua hatua,” ameeleza mbunge huyo.

Kuhusu hasa TICTS, msongamano wa makontena Dar es Salaam umesababisha wengi kuacha kutumia bandari hiyo na badala yake kuhamia Mombasa, Kenya.

Na bado serikali ilionyesha kigugumizi mapema kuhusu suala hilo ambalo ililiunda yenyewe ilipoamua kuongeza muda wa mkataba wa awali ilhali TICTS haijamaliza hata miaka mitano ya mkataba uliopaswa kuishia 2010.

Wakati mkataba ndio kwanza umefika miaka mitano mwaka 2005, serikali iliongeza muda wa miaka 15 ikimaanisha mkataba utamalizika mwaka 2025.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovic Utouh amesema mkataba huo haukuzingatia Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004.

Akijibu swali bungeni Aprili mwaka huu, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema mkataba huo ni mzigo mkubwa kwani umeshindwa kuleta ufanisi.

Baadhi ya wabunge wameshangaa kuona kampuni hiyo inaendelea na kazi ambayo hakika haiiwezi.

Wiki iliyopita, wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Fedha na Uchumi ya Bunge waliilaumu serikali kwa kuendelea kuibeba TICTS licha ya kushindwa kuwajibika na kusababisha uchumi kuzorota.

Kwa upande wa TRL, serikali imekuwa ikikiri kuwa kampuni ya RITES imeshindwa. Sasa inakabiliwa na migomo ya wafanyakazi ambao imeshindwa kuwalipa mishahara.

Nayo TANROADS inakabiliwa na migogoro na kesi zinazohusu ukatishaji mikataba ya ujenzi wa barabara kati yake na makandarasi.

Wakati hayo yakiendelea wizara ya miundombinu juzi Jumatatu, hata kabla ya kuwasilisha bajeti yake bungeni, ilitiliana saini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Korogwe-Handeni na Dumila-Kilosa.

Mkataba huo wa ujenzi ulisainiwa katika Hoteli ya Veta mjini Dodoma huku majibu ya serikali iwapo ilitumia fedha za bajeti kwa barabara ya Chalinze-Segera hayajawasilishwa bungeni.

Mwanzoni mwa mkutano wa bajeti, mbunge wa Nzega, Lucas Selelii aliomba mwongozo wa spika juu ya serikali kutumia fedha za barabara bila kuidhinishwa na Bunge.

0
No votes yet