Kazi ya Chama Vs Kazi ya Siasa


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 18 August 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

MWAKA 1903, ulitokea mgogoro mkubwa baina ya viongozi wawili wakubwa wa chama cha wafanyakazi nchini Urusi.

Vladmir Lenin na Julius Martov, walikuwa na ugomvi mkubwa juu ya ni watu gani wanastahili kuwa katika bodi ya uhariri ya gazeti la Iskra lililokuwa likimilikiwa na taasisi hiyo.

Mwaka 1902, ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya kuibuka kwa mgogoro huo, Lenin alikuwa ametoa kitabu kilichoitwa What Is To Be Done. Kitabu hicho kilieleza kwa kirefu kazi za chama cha siasa, viongozi, wanachama wa kawaida na makada.

Lenin alitaka kundi dogo tu la makada wa chama hicho ndiyo wawe wajumbe kwenye bodi ya uhariri ya gazeti hilo.

Kwamba gazeti litatoa kitu gani, kwa namna gani na wakati gani linapaswa kuwa suala linalojulikana na watu wachache. Si kila mwanachama ana haki ya kujua.

Martov alikuwa na mawazo tofauti. Alitaka wanachama wote wawe na haki ya kujua nini kitatoka kwenye gazeti lao.

Kwa maana nyingine, alitaka wanachama wote wa chama cha wafanyakazi kuwa wajumbe wa bodi hiyo kwa njia moja au nyingine.
Ndipo hapo sasa chama hicho kilipoamua kufanya mkutano maalumu wa wanachama kuamua njia ipi ilikuwa sahihi kati ya hizo mbili.

Lenin alipata ushindi mkubwa. Martov akashindwa. Waliomuunga mkono Lenin, wakaanza kufahamika kwa jina la Bolsheviks – waliowengi- na Martov na wafuasi wake wakaitwa Nemasheviks – wachache.

Kwa hiyo basi, gazeti la chama likakubalika litengenezwe na kundi dogo la watu wachache kwenye bodi ya uhariri. Lifanye kazi ya chama. Na Lenin akapata ushindi wake wa kwanza dhidi ya Martov.

Funzo kubwa katika mkasa huu wa zamani ni kwamba; ndani ya chama cha siasa kuna kazi mbili kubwa za kufanya. Kuna kazi za chama na kazi za kisiasa.

Nimeulizwa maswali mengi na watu kuhusu nini hasa ambacho Naibu Mkurugenzi wa Propaganda wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tambwe Hizza, anakisaidia chama chake.

Kuna wanaohoji iwapo uteuzi wake ulikuwa sahihi. Wengine wanaohoji mantiki ya CCM kumpa mwanasiasa huyo machachari nafasi hiyo nyeti ndani ya chama.

Mawazo yangu ni kwamba, CCM ilikosea kumpa Tambwe nafasi hiyo. Kazi anayoifanya sasa ni ya chama ingawa ninafahamu angefanya vizuri zaidi kama angepewa kazi ya siasa kufanya.

Kuna tofauti kubwa kati ya kazi ya chama na kazi ya siasa. Kazi ya chama inatokana na itikadi ya chama. Inatokana na utaalamu uliojengwa ndani na nje ya chama. Ni kazi ya kujenga chama.

Mtu yeyote anayepewa nafasi kubwa ya uongozi ndani ya chama anapaswa kuwa kada wa chama. Anayekijua chama nje na ndani. Ambaye chama kipo kwenye damu yake.

Kwa mujibu wa Lenin na wale Bolsheviks, kiongozi wa chama anatakiwa kuwa mtu aliye tayari kukifia chama. Mtu ambaye anaweza kubadili sera na mwelekeo wa chama wakati wowote inapobidi hata kama atabaki mwenyewe ndani ya chama.

Kazi ya siasa ni shughuli yoyote ambayo itakisaidia chama cha siasa kuingia madarakani, kubaki madarakani, kuongeza wanachama wapya na kupunguza au kumaliza kabisa nguvu ya upinzani.

Kazi ya chama ni kuhakikisha kuwa kinaendelea kuwapo, madarakani au nje ya madaraka.

Tambwe si kada wa CCM. Hawezi kufa kwa ajili ya CCM. Hakijui chama hicho kinagaubaga na kwa kifupi hakifahamu. Katika mantiki hiyo, hawezi kufanya kazi ya chama ndani ya chama hicho.

Nina imani kwamba hajui mengi ya mambo yanayofanyika nyuma ya pazia ndani ya chama hicho. Kama hujui mambo ya ndani ya chama chako, huwezi kufanya kazi ya chama.

Katika nchi kama Marekani, kuna tofauti kubwa kati ya kazi hizi mbili. Barack Obama si kiongozi wa chama cha Democrat kinachotawala nchini humo kwa sasa.

Lakini kama mwanachama wa chama hicho, anafanya kazi kubwa ya kisiasa kwa ajili ya chama chake. Kama ataongeza uchumi wa Marekani, atakuwa amefanya kazi nzuri ya kisiasa kwa chama chake.

Kama atavutia wanachama wa Republican wazidi kuvutiwa na sera za Democrats, hiyo ni kazi nzuri ya kisiasa. Hata hivyo, wapo watu wanaofanya kazi za chama chake na yeye hajui kila kitu.

Tatizo kubwa ambalo limekuwa likiikabili nchi yetu tangu kuingia kwa mfumo wa vyama vingi ni kushindwa kwa vyama na wanasiasa kutofautisha kazi hizi mbili.

Kama CCM imemchukua Shaibu Akwilombe kutoka CUF kwa mfano, haipaswi kumtafutia nafasi ya uongozi ili kimtumie vizuri.

Kuna kazi kubwa tatu za chama chochote cha siasa; Kuongoza, kuhakikisha kinaendelea kuwapo na uamsho (vitendo kama kuitisha maandamano na kuelimisha).

Chama kinapomchukua mtu kutoka chama kingine, kitu cha kwanza inachomfikiria ni kumpa nafasi ya uongozi. Na nafikiri hapa ndipo lilipo tatizo kubwa.
Tambwe, Thomas Ngawaiya, Arcardo Ntagazwa, Fred Mpendazoe na wengine wanaweza kutumiwa katika kazi nyingine mbili nilizozitaja na si uongozi.

Tambwe, kwa mfano, alikuwa kifanya kazi kubwa kuhakikisha mamia kwa maelfu ya watu wanahudhuria mikutano ya hadhara ya CUF mwanzoni mwa miaka ya 2000.

CCM ingeweza kumtumia kuhakikisha mikutano yake inajaa watu wa kutosha wakati wa kampeni. Ingemtumia kwenye maandamano na uelimishaji wa wananchi kuhusu ubaya wa sera za upinzani.

Huku angekuwa anafanya kazi nzuri ya kisiasa. Angewaachia wenye CCM yao kufanya kazi za chama. Na makada wenye uwezo wa kushika nafasi aliyonayo Tambwe wako wengi, wengi sana.

Tatizo kubwa si Tambwe, tatizo ni vyama vyetu kutofuata tena itikadi bali kuwa zoazoa. Kama alivyopata kusema Horace Kolimba; …. “CCM haina dira wala mwelekeo.”

Chama kinachofuata itikadi na chenye sera na mwelekeo unaojulikana, hakiwezi kumpa ‘mgeni’ nafasi nyeti kama aliyopewa Tambwe.

Kama mgogoro wa Bolsheviks na Nemasheviks ulivyotufundisha awali, kuna chama na kuna siasa. Na wakati mwingine, maslahi ya chama yanaweza yasiwe mazuri kisiasa na mazuri kisiasa yakawa mabaya kichama. Vitu viwili tofauti.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: