Kelele za udini ni ghiliba za watawala


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 19 January 2011

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

Tangu mwaka 1995 Dk. Willibrod Slaa alipochaguliwa katika mazingira magumu ya kisiasa kuwa mbunge wa Karatu, hakuna mtu aliyemwangalia kama Mkatoliki.

Kadhalika, hata mwaka 2000 na baadaye mwaka 2005 Dk. Slaa alipogombea ubunge kwa mara nyingine na kushinda, hakuna pia aliyemuona kama Mkatoliki.

Nina hakika hata kama mwaka jana angegombea ubunge na kushinda bado asingeonekana kuwa ni Mkatoliki.

Kwa maneno mengine, Dk. Slaa ambaye hajawahi kuficha ukweli kwamba alikuwa padri wa Kanisa Katoliki na kupanda madaraja humo ndani hadi kuwa Katibu wa Baraza la Maaskofu (Tec), eti leo kuna ugunduzi umefanywa kuwa ni Mkatoliki na kwa maana hiyo ni hatari!  

Hajawahi kuficha na wala hajawahi kusimama kokote hadharani akiwa mbunge na kujitangaza kwamba yeye ni mbunge wa Wakatoliki achilia mbali Wakristo kwa umoja wao.

Lakini mara tu, Dk. Slaa alipoombwa na Kamati Kuu ya chama chake – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kugombea urais, hoja ya Slaa kuwa Mkatoliki iliibuka.

Wa kwanza kuibua hoja hiyo ni gazeti moja la kila siku la Mtanzania linalomilikiwa na mtuhumiwa mkuu wa ufisadi nchini, Rostam Aziz lililosema, “Slaa kutumia Ukatoliki wake kusaka urais.” 

Nilikuwa miongoni mwa watu waliosoma habari hiyo na zilizofuata baadaye katika magazeti dada ya hilo la kila siku, lakini sikuwa na cha kusema ila kushangaa kwamba ghafla yule Dk. Slaa ambaye wanahabari karibu wote wapenda taifa lao wanamuona kama mpiganaji amekuwa si kitu kingine isipokuwa Mkatoliki.

Niliwaza sana kiasi cha kujiuliza hivi katika wagombea urais wote aliyekuwa na dini wakati huo alikuwa ni Dk. Slaa tu. Niliwaza na kuwazua, lakini sikupata jibu.

Hata hivyo, kadri kampeni zilivyokwenda, kidogo kidogo nilijua ni kwa nini Dk. Slaa alipandikiziwa hoja ya Ukatoliki.

Hoja hii ilipikwa na kuenezwa kwa njia ile ile Chama cha Wananchi (CUF) kilipata kupachikwa majina kadhaa ikiwamo chama cha Kiislamu, chama cha kigaidi na mengine mengi.

Lakini kubwa ni pale aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Omar Mahita, bila soni alisimama hadharani kwenye televisheni na kuonyesha visu vya kukatia nyanya na vitunguu vikiwa na mpini wa bluu na mwekundu kuwa ni vya CUF.

Mahita alidai kuwa visu hivyo vimeletwa nchini na CUF na kwamba vimelenga kufanya fujo na mauaji katika uchaguzi wa mwaka 2005!

Kama ilivyo ada, wapo Watanzania waliomuamini Mahita, wakidhani kwamba alikuwa anazungumza ukweli. Lakini miezi miwili baadaye ukweli ulikuwa dhahiri.

Mahita alikuwa anaandaa watu kisaikolojia ili watakapofanya ubedui wao umma uamini kwamba kweli polisi walikuwa wanapambana na magaidi. Watu wenye visu vya kukatia nyanya na vitunguu jikoni! 

Mwaka huu mauaji hayajatokea Pemba, yametokea Arusha, safari hii ni wafuasi wa CHADEMA wameuawa na watu wengine waliokuwa wanapita njia.

Wamejeruhiwa watu wakiendelea na shughuli zao mjini Arusha, na hata wengine kulazimishwa kunasabishwa na watu kutoka mkoa wa Mara, kwa nia ya kujenga uongo na kuutakatisha; kazi na mbinu zile zile chafu za Jeshi la polisi.

Lakini baada ya polisi kufanya mauaji haya, yaani watu watatu na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa, wameibuka na utetezi wa kitoto ambao hakika ule wa Mahita unaweza kuwa na nafuu.

Polisi wamejitahidi kutumia vyombo vya habari, magazeti na televisheni kusambaza utetezi wao wa kijinga kabisa juu ya vurugu za Arusha.

Wanajitetea kuwa viongozi wa CHADEMA ndio wa kuwajibika kwa mauaji ya raia kwa kuwa eti walihamasisha wananchi kuandamana na kufanya fujo, lakini wao wakajihami kwa risasi za moto na kuua raia.

Utetezi huu wa kitoto ukiendelea polisi wanashindwa kujua kuwa wanachofanya ni kuzungumzia matokeo, lakini hawagusii kabisa chanzo cha kadhia yote hii ni nini.

Polisi hawataki kukiri kwamba wao ndio walipanda mbegu ya kadhia hii; walioutibua umma jijini Arusha, na walishindwa kutumia busara na hekima kusaidia wananchi kutumia haki zao kikatiba, kukutana na kuandamana.

Utetezi huu mwepesi wa polisi ukiendelea kurudiwa kwenye vyombo vya habari ili kusafisha mikono yao iliyojaa damu, lakini kumbe wanazidi kujiumbua, hoja ya udini iliyoanza mwaka jana kwenye mchakato wa uchaguzi, inarudiwa tena na tena.

Polisi wakiendelea na utetezi huo, watu wale wale walioanzisha hoja ya udini nao wapo kazini kwa kasi ya ajabu waendeleza ulevi wao wa kuchochea hisia za kidini. Wanataka kuaminisha nchi kwamba Dk. Slaa sasa ule Ukatoliki wake ameuambukiza kwa CHADEMA yote.

Kwamba sasa CHADEMA imekuwa Katoliki, kwamba inaendesha kampeni za kutaka nchi isitawaliwe kwa sababu ya kanisa.

Lakini kwa bahati mbaya wanaoeneza ulevi huu mbaya wanakosa kabisa subira ya fikra ambayo ya kuwasaidia kutambua ukweli kuwa kama wanaeleza CHADEMA ni jumuiko la Wakatoliki, wanakifungamanisha na chama hicho na Wakristo, je, ni chama cha Wakristo kinachopingana na serikali ya nani? Je, serikali ni ya Kiislamu?

Upuuzi huu wa watetezi wa hoja mfu, nyepesi na ambazo hazina mashiko kwamba CHADEMA wanasukumwa na kanisa kudai haki ya kuporwa haki yao Arusha, pamoja na kutaka mabadiliko ya kimfumo kwa maana ya sheria za uchaguzi, tume ya uchaguzi na katiba ya nchi kwa ujumla wake, ni hoja ya kanisa dhidi ya msikiti?

Unapotazama msokoto wa hoja za udini ambazo kwa bahati mbaya mno, Rais Jakaya Kikwete kwa staili ile ile aliyobeba kwenye ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2005 suala la mahakama ya kadhi, na hili la udini amelibeba zima zima kwenye hotuba yake.

Swali gumu linabakia pale pale, nani anaeneza udini? Mbona hoja ya udini imeshupaliwa na vyombo vya  habari ambavyo kwa mlango wa nyuma vinashikamana na watu wanazunguka waliko madarakani.

Mbona utunzi wa habari nyingi za kutaka kusadikisha nchi kujaa udini zinasukumwa na vyombo hivyo hivyo tu ambavyo vimeamua kuachana weledi wa habari na sasa ni kutaka kupotosha?

Je, Watanzania wanataka kuaminishwa kwamba udini wa nchi hii ni kazi ya mikono ya Dk. Slaa?

Nafikiri wakati umefika watu kuwajibika kwa mujibu wa waliyoomba kutenda, kwamba watu wajilize maswali magumu yanayolenga kujipima na kujitathmini kwamba nini kimefanyika kuwakomboa wananchi.

Tathmini ya namna hii itasaidia kusaidia watu kujitambua waliko katika kuleta mageuzi ya kweli ya kiuchumi nchini.

Uasi wa umma ni juu ya umasini wao dhidi ya wale waliopewa dhamana ya kuuondosha, si udini!  Tujiulize maswali magumu kwamba imekuwa je ghafla Watanzania wamehamasika juu ya haki zao; ni udini au wameamka kiasi cha kutambua haki zao.

Leo ni Dk. Slaa Mkatoliki, kesho akiibuka Mlutheri, au Muangilikana au Mpetekoste au Muislamu, itakuwa ni udini wa nani dhidi ya nani. Tusisahau ghliba za watawala, hoja ya udini ni mojawapo.

0
Your rating: None Average: 4 (4 votes)
Soma zaidi kuhusu: