Kenya: Minyukano yaongezeka ndani ya ODM


Hilal K. Sued's picture

Na Hilal K. Sued - Imechapwa 01 December 2010

Printer-friendly version
Raila Odinga

WAZIRI Mkuu wa Kenya Raila Odinga amewapa changamoto ‘waasi’ ndani ya chama chake cha upinzani, Orange Democratic Movement (ODM) kujiondoa mara moja, akiwaambia uongozi wa juu wa chama hicho hautakubali kamwe kuendelea kupata vitisho.

Raila, ambaye ni kiongozi mkuu wa ODM alikuwa akizungumza katika mkutano wa Baraza Kuu la chama hicho mjini Nairobi Ijumaa iliyopita. Alisema kwamba wako viongozi wengi wengine waaminifu ndani ya ODM ambao wako tayari kuchukua nafasi zao.

Bila kutaja majina, Raila alikuwa anamzungumzia Naibu wake William Ruto ambaye wiki iliyopita alidokeza kujiondoa kwenye chama hicho cha upinzani.

Raila alisema: “Hatuko tayari kumbembeleza mtu yeyote ambaye anataka kujitoa. Mwanachama yeyote au kiongozi wa ODM anayetaka kuondoka yuko huru kufanya hivyo.”

Alisema ODM ni taasisi ambayo haitakubali kamwe kuyumbishwa na watu wachache katika safari yake ya kuingia Ikulu ifikapo mwaka 2012. “Hata kama ni Raila mwenyewe akijitoa, chama kitabaki bila kutetereka,” aliongeza.

Kauli hiyo ya Raila ilijibiwa haraka na wabunge wa ODM pamoja na viongozi wengine katika Mkoa wa Rift Valley ambao walimtuhumu kiongozi huyo wa ODM kwa kauli za vitisho.

Viongozi hao, Elijah Lagat (Mbunge wa Engwen), Julius Kones (Konoin) na Sammy Mwita (Baringo Central), walisema kwamba William Ruto hajaingilia chochote katika shughuli za ODM kwani alikuwa bado ni naibu kwa Raila.

Mkoa wa Rift Valley ndiyo ngome kuu ya ODM na ndiko anakotoka Ruto ambaye ni Mbunge wa Eldoret North na anaonekana kuhamasisha wabunge na viongozi wengine wa ODM kufanya uasi dhidi ya Raila.

“Labda Raila afafanue anachosema badala ya kutoa kauli za kijumla jumla tu—aseme lini na wapi Ruto amekuwa akivuruga shughuli za chama,” alihoji Lagat.

Lagat aliongeza kwamba ODM ni chama bora kwa yeyote yule mradi tu viongozi wake waondokane na mielekeo ya ki-imla kama ilivyokuwa wakati wa utawala wa chama kimoja.

Naye Dk Kones alisema Raila hakuwa na kitu kipya, ni kitu ambacho daima alikuwa nacho moyoni ila tu sasa ndiyo kakitoa hadharani.

Viongozi wengine wa ODM wa Rift Valley wamesema kwamba wanasubiri Ruto na wenzake wajiondoe kutoka kwenye chama ili wawafuate kwa wingi ili kukidhoofisha chama katika mkoa huo muhimu.

Ruto na wabunge wengine kutoka mkoa huo hawakuhudhuria mkutano wa Baraza Kuu la ODM siku ya Ijumaa. Hali ya mvutano mkubwa baina ya viongozi hao wawili (Raila na Ruto) iliibuka kutokana na tofauti zao kuhusu ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi wa Desemba 2007 na suala la kuwahamisha watu kutoka Msitu wa Mau ulioko mkoani Rift Valley.

Wachunguzi wa mambo wanasema Ruto na wenzake wanacheza na muda tu, kwani wanatafuta muda muafaka wa kujiondoa ODM na kujiunga na chama kidogo na kisichojulikana kiitwacho United Democratic Movement (UDM).

Vyanzo vya habari vya kuaminika vinasema Ruto na wabunge wanaomuunga mkono wamepanga kutwaa uongozi wa chama hicho ili kujiandaa kwa uchaguzi wa mwaka 2012 ambapo Ruto anatarajiwa kugombea kiti cha urais.

Chini ya Sheria ya Vyama nchini humo iliyorekebishwa mwaka juzi, iwapo Ruto na wabunge wenzake watajitoa ODM, watapoteza viti vyao vya ubunge.

Siku hiyo hiyo ya Ijumaa, Ruto alikutana na Waziri wa Fedha, Uhuru Kenyatta katika kile kilicoonekana kufanya maandalizi ya ama kujiunga na UDM au kuunda muungano mpya ambao utajumuisha vyama vingine kadha.
Kenyatta ni kiongozi wa KANU ambacho kimo katika muungano wa PNU ambao ndiyo, pamoja na ODM, viliunda serikali ya pamoja.

Baadaye Ruto alikutana na Waziri wa Nishati, Kiraitu Murungi katika mazungumzo ambayo yalilenga suala hilo hilo la kuunda muungano mpya kwa ajili ya uchaguzi wa 2012.

Vyanzo vya habari vinaongezea kusema kwamba viongozi hao, wameazimia kuendelea kukutana ili kufanya mazungumzo zaidi.

Na katika kuelezea hatua hizo za wapinzani wake katika ODM, Raila aliwaambia waandishi wa habari kwamba wazo la kuunda umoja baina ya Wakalenjin (Mkoa wa Rift Valley) na Wakikuyu (kutoka Mkoa wa Central) hautafanikiwa kwani enzi za ‘siasa za ukabila’ nchini Kenya ilikwisha miaka mingi iliyopita

Hata hivyo, haijaeleweka vema iwapo mazungumzo kati ya Ruto na Kenyatta yataathiri mpango unaoandaliwa muungano wa PNU kuwataka waziri wa zamani wa Usalama wa Ndani, Prof George Saitoti na Makamu wa Rais, Kalonzo Musyoka wakabiliane katika kura za awali za maoni katika PNU ili kumpata mgombea mmoja wa urais mwaka 2012.

Mara aliposimamishwa uwaziri Oktoba 19, 2010 Ruto alisema angetoa mwongozo mpya kwa wafuasi wake ifikapo mwisho wa mwaka.

Naye Raila amekuwa akiwazuia viongozi wenzake katika ODM kutochukua hatua ya kumfukuza Ruto, lakini katika mkutano wa Baraza Kuu la ODM Ijumaa iliyopita, kiongozi huyo wa chama alitoa dokezo kwamba uchaguzi wa ndani wa chama hicho utafanywa mapema mwaka ujao ili kukisafisha chama kutokana na ‘waasi’ waliojikita katika ngazi mbali mbali.

Raila aliwaambia wajumbe: “Hata wakati ambapo tunajaribu kukumbatia hali ya ‘ndoa’ ya maridhiano baina yetu na wapinzani wetu wa PNU (chama cha Rais Mwai Kibaki), tusikubali kuyapoteza malengo yetu.”

Aliwashambulia ‘waasi’ ndani ya ODM ambao wamekuwa wakiipinga Katiba mpya iliyopendekezwa. Ikumbukwe kwamba Ruto alipiga kampeni kali kuipinga Katiba hiyo ambayo wananchi wengi wa Kenya waliikubali katika kura ya maoni mwezi Agosti mwaka huu.

Aidha Raila alimshangaa Ruto kwa hatua yake ya kuzunguka nchi nzima kuwashukuru wananchi kwa kuipinga Katiba mpya wakati ambapo wananchi wengi waliiikubali kutokana na kura ya maoni.

Akikifananisha chama cha ODM kama ‘simba’ Raila alisema chama hicho kimejizatiti vilivyo katika mikoa ya Kati (Central) na Mashariki (Eastern) maeneo ambayo chama hicho hakikuwa kimefanya vizuri katika uchaguzi wa mwaka 2007.

Mkutano wa Baraza Kuu la ODM ulihudhuriwa na wenyeviti wa matawi kote nchini na kuhudhuriwa na wabunge zaidi ya 70 wa ODM, wakiwemo Naibu Waziri mkuu Musalia Mudavadi, mawaziri Anyang’ Nyong’o (Katibu mkuu wa ODM), Henry Kosgei (Mwenyekiti wa ODM) na wajumbe wengine Joseph Nyagah, Mohammed Elmi, Najib Balala, Paul Otuoma, na James Orengo.

Mudavadi, ambaye pia ni mmoja wa manaibu wa Raila, alisema inapasa ODM ikazanie kukuza ufuasi wake wa mashina kabla ys uchaguzi wa mwaka 2012.

0
No votes yet