Kesi za ufisadi ziendeshwe kwa Kiswahili


Alloyce Komba's picture

Na Alloyce Komba - Imechapwa 14 January 2009

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

KUNA msemo katika masuala ya utoaji haki mahakamani uendao hivi: “Haki siyo tu itendeke, bali pia ionekane imetendeka.” Huu ni msemo maarufu katika mwenendo mzima wa usilizaji kesi au shauri.

Je, haki huwa imetendeka pale kesi inapoendeshwa katika lugha ambayo wasikilizaji hawajui? Je, si vyema kutumia lugha inayoeleweka kwa wengi, wakiwemo washitakiwa na washitaki, hata kama itakuwa na istilahi za taaluma ya sheria kuliko kutumia lugha ya kigeni?

Hata kama lugha ya mahakama nchini, katika kuweka kumbukumbu ni lugha ya Kiingereza, isipokuwa kwa mahakama za mwanzo, wananchi wengi wanaelewa masuala mengi kwa lugha ya Kiswahili hasa pale wanapotaka kujua mambo yanayohusu haki zao.

Kiswahili ndiyo lugha inayofikisha ujumbe halisi na kwa urahisi kwa Watanzania wengi kuliko lugha yoyote. Ndio maana hata vyombo vingi vya habari hususan magazeti, hutumia lugha ya Kiswahili. Hii haitokana tu na kiwango cha upeo wa ki-elimu walichonacho Watanzania, bali ni kwamba Kiswahili hivi sasa kinachukua nafasi hata ya “lugha ya mama” – ya mahali ulipozaliwa.

Kwa hiyo ukitaka kumnyima haki Mtanzania katika kufahamu masuala yanayomhusu, basi zungumza au andika kwa lugha nyingine yoyote ya kigeni kama Kiingereza. Nimegundua hali hii hata kwa wasomi wengi. Ukitaka wasomi wengi wa Tanzania wawe huru kuchangia mada yoyote ile wanayoifahamu, basi waruhusu kuzungumza kwa Kiswahili.

Hii ina maana kwamba utawafanya wawe bubu kama utawaambia wachangie au kuuliza maswali kwa Kiingereza au lugha nyingine za kigeni. Hata waandishi wengi wa habari wako hivyo; ni wepesi na wanajua kuandika habari kwa wepesi na ujuzi kwa kutumia Kiswahili kuliko lugha za kigeni.

Siyo siri kwamba kama lugha ya kuandika habari – kwa magazeti, redio na televisheni – ingekuwa Kiingereza tu, pengine yasingekuwepo magazeti mengi nchini kama tunavyoyaona. Kwa msingi huo, ni vema kukubaliana kuwa masuala ya maslahi ya nchi yanapaswa kuwekwa bayana kwa lugha ya Kiswahili.

Jaji Mkuu Augustino Ramadhani amewahi kunukuliwa akisema kwamba ni vizuri mahakimu na majaji wakawa wanaruhusu usikilizaji kesi au mashauri kwa Kiswahili, hasa kesi zenye mvuto mkubwa kwa jamii, bali kumbukumbu zake ziwe zinaandikwa kwa Kiingereza kama mwenendo wa kesi mahakamani unavyotaka.

Lengo la kutumia Kiswahili liwe ni kutoa nafasi ili HAKI IONEKANE INATENDEKA kwa kila aliyekuja kusikiliza mahakamani. Hii inasaidia pia kuwaelimisha wananchi wengi kuhusu masuala ya sheria na utendaji kazi wa mahakama.

Sasa iweje kesi za ufisadi, zenye mvuto mkubwa wa wananchi, zilizoanza kunguruma mahakamani, hasa zile za madai ya kuchota mabilioni ya shilingi kutoka akaunti ya madeni ya nje (EPA) zisikilizwe kwa Kiingereza?

Kwa mfano, kesi za utumiaji madaraka vibaya zilizowakumba mawaziri wa zamani, Basil Mramba, Daniel Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, zimeanza kusikilizwa kwa lugha ya Kiingereza ambapo wananchi wengi wanaohudhuria kesi hizo hawajui lugha hiyo, hivyo hawafuatilii kwa makini kile kinachoendelea.

Inashangaza hata upande wa mashtaka ambao unatakiwa kufahamu umuhimu wa mashtaka yake kujulikana kwa umma mpana wa Watanzania, hawajaziomba mahakama husika kwamba waendeshe kesi kwa Kiswahili; vivyo hivyo mawakili ambao ni maafisa wa mahakama.

Nilikuwa mmoja wa wasikilizaji wa maombi ya kupunguziwa masharti ya dhamana katika kesi inayowakabili Mramba na Yona katika Mahakama Kuu. Niligundua kwamba Kiingereza kilikuwa kikwazo kwa wasikilizaji wengi wa kesi hiyo iliyokuwa na mvuto mkubwa.

Walichokuwa wanazungumza mawakili wa utetezi na wale wa upande wa mashitaka, hakikuwa kinaeleweka kwa vile walizungumza kwa Kiingereza. Naye Jaji Njengafibili Mwaikugile aliuliza maswali na kutoa uamuzi kwa Kiingereza.

Ndugu wa washtakiwa walikuwa na hamu ya kujua hoja zinazotolewa na mawakili katika kuwasilisha maombi yao. Walitaka pia kujua wajibu maombi wanasemaje na maswali ya jaji ni yapi. Ilibidi wasubiri mahakama iahirishwe ili wakitoka nje ndipo waeleweshwe na mawakili ni kitu gani kilikuwa kinaendelea.

Hapa mahakama haikuwatendea haki wasikilizaji wa kesi hiyo. Watuhumiwa wenyewe, hata kama wanajua Kiingereza, lakini masuala magumu ya kisheria yanapokuwa katika lugha ngeni, yanaongeza ugumu wa kuelewa.

Kama Kiswahili hakitatumika katika kusikiliza kesi hizi ambazo wananchi wanaona zina maslahi makubwa kwao, mambo yafuatayo yanaweza kutokea:

Kwanza, taarifa za vyombo vya habari kuhusu kesi hizo zitakuwa sio sahihi kwani waandishi wa habari nao hawana upeo wa kuelewa masuala yanayozungumzwa kwa Kiingereza cha kisheria.

Pili, washtakiwa watashindwa kufahamu mwenendo wa kesi zao ili waweze kujiandaa vema kwa utetezi au kuwaelekeza vizuri mawakili wao.

Tatu, haki haitakuwa imetendeka kwa vile yanayozungumzwa hayaeleweki kwa wengi. Ni kama vile mawakili, waendesha mashtaka na mahakimu au majaji wananong’onezana tu. Haitatoa fursa kwa watu wengine nao kupima uzito wa ushahidi ili kuona kama wanaweza kuona uamuzi utakavyokuwa.

Jaji Mkuu Mstaafu Barnabas Samatta aliwahi kusema kwamba katika kuendesha kesi kuna majaji au mahakimu wa pande mbili ambao wote hutoa uamuzi kila mmoja kwa namna yake.

Alisema kuna jaji au hakimu yule anayesikiliza kesi ambayo inaendelea kusikilizwa mahakamani; lakini kuna “jaji” au “hakimu” mwingine asiye rasmi ambaye ni kila msikilizaji anayekuja mahakamani na ambaye hufuatilia mwenendo mzima hasa ushahidi unaotolewa.

Hatimaye, alisema Samatta, wakati jaji au hakimu rasmi anapojiandaa kutoa uamuzi au hukumu, msikilizaji naye huamua kutoa uamuzi au hukumu yake huku akisubiri kulinganisha na uamuzi wa jaji au hakimu rasmi.

Iwapo uamuzi au hukumu ikilingana na uamuzi au hukumu yake, hapo msikilizaji huyo, ambaye ni mwananchi wa kawaida kabisa, huona haki imetendeka. Lakini ikiwa ni tofauti huona haki haijatendeka labda kama akishawishiwa kwa sababu nyingine nzuri za kisheria.

Kutokana na mtazamo huo wa Samatta, mwananchi wa kawaida hawezi kuwa na wajibu usio rasmi wa ujaji au uhakimu kama hataelewa mwenendo wa kesi husika iwapo haelewi lugha inayotumika. Ni pale tu lugha inakuwa ya kueleweka na rahisi ndipo mwananchi anaweza kushiriki katika kusikiliza kesi na kutoa uamuzi wake utakaokuwa kipimo kwa utendaji haki wa mahakama.

Ni vizuri mahakama zinazosikiliza kesi za ufisadi zione umuhimu wa ushauri huu ambao una manufaa kwa watuhumiwa, mawakili na mahakimu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: