Kichefuchefu cha hukumu 2005-2010


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 05 January 2011

Printer-friendly version

AHADI ya Binadamu wote ni ndugu zangu inafanana na msemo wa “Wanyama wote ni sawa” uliomo katika kitabu cha Shamba la Wanyama (The Animal Farm).

Lengo lake lilikuwa kuonyesha mshikamano, umoja, upendo na kuheshimu misingi ya usawa iliyokuwa inafuatwa baada ya wanyama kuondokana na udhalimu wa binadamu.

Baada ya uhuru, wanyama wote walikuwa wanagawana sawa kwa sawa raslimali za nchi, chini ya kiongozi wao Napoleon wa jamii ya nguruwe, lakini baadaye zikaanza kuonekana tofauti.

Awali sheria zilizokuwa zinatumika katika kesi zilijali usawa lakini baadaye, tabaka tawala likapindisha na kujipa upendeleo katika umiliki wa mali na vitu vinono.

Wanyama waliochoshwa na ukoloni mamboleo, wizi, ufisadi, na hasa madhila ya kukosekana kwa haki kwa wanyonge wakaandika upya kaulimbiu hiyo. Ikasomeka Wanyama Wote Ni Sawa, lakini Baadhi ni Bora Kuliko Wengine.

Tanzania ya sasa haina tofauti na Shamba la Wanyama kwa kosa hilohilo moja la mlalahoi kutupwa jela miaka 30, huku aliyenacho akiachiwa huru.

Wezi wakubwa wa fedha katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) iliyoko Benki Kuu (BoT) badala ya kushtakiwa walipewa msamaha na Rais Jakaya Kikwete.

Aliwapa muda warejeshe, na aliahidi kuwa “watakaoshindwa watafikishwa kortini.” Hakusema lolote kuhusu walioiba kupitia kampuni za Kagoda, Deep Green, Meremeta na waliojimilikisha mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira.

Kuhusu mradi wa kifisadi wa Dowans, Dk. Harrison Mwakyembe anasema kampuni hiyo ilirithi mkataba feki kutoka Richmond hivyo haiwezi kutambuliwa; Samuel Sitta anasema hakuna uhalali wa kulipa fidia mpaka kwanza hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC), iliyoipa haki Dowans dhidi ya Tanesco, isajiliwe Mahakamu Kuu ya Tanzania.

Lakini Mwanasheria Mkuu, Frederick Werema ambaye anaakisi msimamo wa Rais Kikwete, anasema mjadala umefungwa, Dowans lazima ilipwe. Dk. Mwakyembe, Sitta na Werema wote ni wajuzi wa sheria, kwa nini wanatofautiana wakati wanasoma vifungu vimoja?

Ukweli mafisadi wanaitumia serikali ipindishe sheria ili wanufaike kwa gharama ya umaskini wa Watanzania. Athari za rushwa zinajionyesha katika hukumu nyingi.

Miaka mitatu iliyopita, vijana watatu wa familia za wafugaji akiwemo mwanafunzi, walitiwa hatiani wilayani Serengeti kwa madai ya kuingiza mifugo eneo la mwekezaji wa Kampuni ya Grumeti.

Awali eneo hilo lilikuwa kwa ajili ya wafugaji lakini baada ya serikali kumpa mwekezaji, wananchi wakazuiwa kulitumia.

Hakimu akawahukumu vijana hao kifungo cha miaka mitatu jela. Lakini cha kushangaza, hakimu alitumia vifungu vya sheria ya elimu vinavyoeleza adhabu kwa atakayehusika kuzuia mtoto kwenda shule.

Baada ya asasi za haki za binadamu kulalamikia hukumu hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza Aishieli Sumari aliitisha faili hilo, akapitia vifungu vya sheria na kubaini hukumu hiyo ilikuwa batili wakati tayari vijana wale walikwishakaa jela mwaka mmoja.

Je, hapa mtu atadai ni kwa vile vijana wale na wazazi wao hawakuwa wanajua sheria? Kwa nini hakimu ambaye ni mjuzi wa sheria, alipindisha sheria?

Machi 2009 Deus Mallya alifunguliwa kesi ya kusababisha ajali iliyoua mjini Dodoma na akafungwa jela miaka mitatu baada ya kupatikana na hatia.

Kwanza ni kwa kuendesha gari kwa uzembe, pili ni kusababisha kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, na tatu kuendesha gari bila leseni. Mallya hakupewa dhamana.

Mahakama ya Wilaya ya Singida, ilimhukumu dereva wa basi la kampuni ya Adventure ya jijini Mwanza, Robert Willison (37), kifungo cha miaka 153 na miezi sita jela baada ya kupatikana na makosa 49 tofauti likiwamo la kusababisha vifo vya watu tisa mwaka 2008.

Robert alisomewa mashitaka matatu: la kwanza lilikuwa na makosa tisa ya kusababisha vifo vya watu tisa; la pili makosa 36 ya kusababisha watu 36 kujeruhiwa na shitaka la tatu lilikuwa na kosa moja la kuendesha basi bila leseni kutoka mkoani Kigoma kwenda Dar es Salaam.

Lakini mahakama hiyohiyo ilimwachia huru dereva wa basi la kampuni ya Mohamed Trans ya jijini Mwanza, Kharabu Jordan (43) ambaye alikabiliwa na shitaka la kusababisha ajali iliyoteketeza abiria 25 kwa moto na kujeruhi wengine kadhaa.

Mahakama ilidai ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka dhidi ya Jordan ulikuwa dhaifu.

Wiki iliyopita, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kinondoni-Kivukoni, Kwey Rusema alimtia hatiani aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge na kumhukumu kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh. 700,000.

Makosa yaliyosababisha Chenge, ambaye awali alishitakiwa kwa mauaji na baadaye kubadilishiwa mashitaka yakawa, atiwe hatiani ni kuendesha gari kwa uzembe, kusababisha ajali iliyowaua Beatrice Constantine na Victoria George, kuharibu mali na kuendesha gari lisilo na bima. Hakimu alithibitisha kuwa Chenge alighushi bima.

Tofauti na Mallya au dereva wa Mohamed Trans, Chenge ambaye ni Mbunge wa Bariadi Magharibi na mwenyekiti wa nidhamu wa CCM, alipewa fursa ya kulipa faini ya Sh. 700,000 hivyo akakwepa kifungo cha miaka mitatu jela.

Kushiriki katika uhalifu au kushiriki kupanga njama za kufanya uhalifu, polisi wanasema ni kosa la jinai na mhusika anaweza kutiwa jela.

Lakini Jaji aliyesikiliza kesi ya kuuawa wafanyabiashara watatu wa Mahenge, mkoani Morogoro, na dereva teksi mmoja mwaka 2006, alisema katika hukumu yake kwamba aliyeua hajulikani, akawaachia polisi wote walioshiriki.

Katika tukio hilo, wapo polisi walikiri kubeba vijana wale na kuwapeleka msitu wa Pande walikouliwa, wapo walioshuhudia bunduki ikifyatuliwa, wapo waliochukua maiti kupeleka Muhimbili – jaji hakuona ushiriki wao isipokuwa alitaka aliyeua.

Utetezi mkubwa wa wataalamu wa sheria ni kwamba watu wengi hawazijui sheria. Je, hiyo ndiyo sababu ya kuwakomoa walalahoi kwa adhabu kali kwa kosa ambalo mjuzi wa sheria anaachiwa huru?

Ukweli tatizo si wananchi kutojua sheria zilizopo, bali ni kukosekana uadilifu, ujuzi makini, utashi wa majaji na mahakimu na kukithiri kwa rushwa kunakosababisha mahakimu na majaji kutumia vifungu batili au kutoa tafsiri iliyopinda ili kuwaridhisha mafisadi.

Hata mashtaka huandaliwa katika namna ya kukandamiza walalahoi na kuwaokoa wakubwa.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Ukiwaona Ramadhani Ditopile Mzuzuri, baada ya gari lake kugongwa na basi la abiria (DCM) alishuka, akatoa bastola na kumtwanga risasi dereva na kumuua.

Polisi wa serikali wakafika kusoma hali, wakafikiria jinsi ya kumwokoa, wakapima na kuandika ripoti.

Ripoti ikasomeka Ditopile aligongwa, akashuka kwenye gari lake kwa bahati mbaya, akachukua bastola kwa bahati mbaya, akamgongea dirisha dereva wa DCM kwa bahati mbaya, akamlenga na kumuua kwa bahati mbaya.

Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) aliposoma akafungua kesi ya kuua bila kukusudia, na akapewa dhamana. Hiki ni kichefuchefu.

0
No votes yet