Kicheko cha Ban Ki-moon kuzimwa


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 25 February 2009

Printer-friendly version
Uchambuzi
Ban Ki-moon

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon anayetua Dar es Salaam kesho kwa ziara ya kikazi, huenda asifurahie ziara yake.

Lakini hii itategemea udadisi na ujasiri wa waandishi wa habari na ukweli utakaoonyeshwa na maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete.

Siyo shwari jijini New York, kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN). Kuna malalamiko dhidi ya Katibu Mkuu. “Anashiriki kunyanyasa Waafrika.”

Si hilo tu. Watanzania wawili, akina mama wenye upeo na uwezo uliothibitika, Profesa Ana Tibaijuka na Asha-Rose Migiro wanaangaliwa kwa jicho la husda, lakini pia wanazongwa kwa nia ya kutaka kuwachomoa kwenye umoja huo.

Barua ya Waafrika, maofisa wa UN, iliyopatikana New York, inaorodhesha matukio mbalimbali ambayo wengi wameanza kuyachukulia kuwa hatua ya katibu mkuu wa sasa ya kuondoa au kupunguza Waafrika na “hasa wateule wa Kofi Annan kwa kiwango kikubwa kutoka UN.”

Yote haya yalianza kwa madai kuwa Waafrika wamekuwa wengi UN. Pale alipoteuliwa Asha-Rose Migiro kuwa Naibu Katibu Mkuu, uvumi ulienezwa kuwa mama huyo hafai, hajui kazi na kwamba amependelewa.

Taarifa kwenye blogu mbalimbali, za watu binafsi wanaofahamika na wasiofahamika kwa majina yao halisi, zilibeba kejeli na kebehi kwa Asha-Rose Migiro ambaye Watanzania wanajua vema alivyo makini.

Shabaha kubwa ya kampeni kupitia taarifa hizo ni kumdhoofisha; kumjaza woga na kumnyima fursa ya kufikiri na kutenda kwa uhuru. Migiro anaonekana kuwa nyongeza kwenye wingi wa Waafrika katika umoja huo.

Migiro aliteuliwa na Ban Ki-moon yapata mwaka mmoja tangu Profesa Anna Tibaijuka ateuliwe na Katibu Mkuu aliyemaliza muda wake, Koffi Annan, kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya UN mjini Nairobi.

Kwa fikra za mahasidi, Migiro na Tibaijuka wakawa kwanza, “Watanzania wengi” katika UN na pili, wakawa sehemu ya “Waafrika wengi” kwenye umoja huo. Ni zogo. Ni mshikemshike. Balozi wa Tanzania UN, Augustine Mahiga atakuwa anajua vita hivi.

Profesa Tibaijuka ana nafuu kidogo. Amekuwa Katibu Mkuu Mwandamizi wa UN na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi (UN-HABITAT).

Hii ni nafasi aliyoshika kwa vipindi viwili mfululizo vya miaka minne kila kimoja na amekuwa ofisa mwandamizi wa UN kwa miaka saba sasa. Anamaliza kipindi cha pili mwakani. Nafasi hii inathibitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Nafasi nyingine aliyonayo ni ile ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya UN iliyoko Nairobi (UNON); nafasi ambayo aliteuliwa na mtangulizi wa Ban Ki-moon. Anashika nafasi hii kwa miaka minne.

Hivi sasa kuna piga-nikupige kutafuta kumwondoa Prof. Tibaijuka katika ofisi za Nairobi kwa madai kuwa nafasi hiyo inapaswa kushikwa kwa mtindo wa “kupokezana,” ingawa haijasemwa kupokezana kwa miaka mingapi.

Tibaijuka anashika nafasi hii kwa kustahili; akiwa ofisa mwandamizi katika UN na mwenye uzoefu wa kazi za shirika hilo kwa miaka saba sasa.

Taarifa za mjini Washington ambazo Balozi Mahiga anapaswa kuwa nazo, zinasema anatafutwa kijana mmoja Mjerumani ili akalie ofisi hiyo. Ni ofisa wa Ujerumani aliyekuwa kwenye ofisi hiyo kabla haijakabidhiwa kwa Tibaijuka.

Kundi la Waafrika kwenye umoja huo linapinga mpango wowote wa kukatisha umri wa nafasi hiyo ili kuweka mtu mwingine. Hata hivyo, katibu mkuu, hata akiwa anataka, hawezi kufanya mabadiliko hayo kwa kuwa anafungwa na kanuni za umoja huo.

“Huo ndio uswahili kwa ngazi ya kimataifa. Hata huku majungu na kijicho vipo,” ameeleza Mtanzania kwa njia ya ujumbe wa simu (smS0 kutoka New York.

Anaweza kutokea mtu na kusema Ban Ki-moon hana tatizo na uteuzi wa Migiro. Hatua hii inatokana na cheo cha Migiro kutokuwa katika mfumo wa UN bali kinategemea utashi binafsi wa katibu mkuu wa sasa.

Hili linamweka Migiro katika hali ngumu. Nafasi yake haina muda maalum; kwa mfano kuwa na kipindi cha miaka mitatu au minne ya utumishi. Inategemea katibu mkuu aliyeunda nafasi hiyo ambaye pia anafahamika kuwa rafiki wa Rais Jakaya Kikwete.

Habari za kibalozi kwenye umoja huo zinasema naibu katibu mkuu angekuwa anatoka nchi nyingine, huenda angekuwa ameondolewa zamani. Sasa Ban Ki-moon anaingia Dar es Salaam kesho.

Taarifa za Dar es Salaam zinasema wizara ya mambo ya nje ilikuwa imependekeza Migiro apewe angalau miaka mitatu lakini mbinu zilizopo zinashinikiza apewe mwaka mmoja tu.

Kwa wanaoelewa uzito wa nyadhifa kubwa kwenye vyombo kama Umoja wa Mataifa, wataelewa kuwa kumpa Migiro mwaka mmoja pale UN ni kuonyesha alikuwa amepewa “kibarua” tu. Hawezi kufanya kazi yoyote muhimu ya kuleta mabadiliko.

Ban Ki-moon anakuja Tanzania. Waandishi wa habari hawawezi kumwachia. Maofisa wa ofisi ya mambo ya nje hawawezi kukaa kimya. Rais Kikwete asikose kumnong’oneza:

  1. Vipi Migiro anapewa kibarua cha muda mfupi?
  2. Vipi Watanzania wanasakamwa kuwa ni wengi na wewe huchukui hatua?
  3. Vipi unataka ofisi ya UN ya Nairobi ichukuliwe na mtawala mpya kabla muda wa Prof. Tibaijuka haujamalizika?
  4. Mjerumani unayetaka achukue nafasi ya Nairobi hana ujuzi wala uzoefu wa viwango vya Prof. Tibaijuka. Kwa nini iwe hivyo?
  5. Mbona unataka kuvunja kanuni za UN wakati unajua kuwa umoja huo ni wa wanachama na wewe kazi yako ni kuulea kwa vizazi vijavyo?
  6. Mbona Watanzania UN hawapati promosheni?
0
No votes yet