Kifimbo cha Nyerere na imani za kale


Aristariko Konga's picture

Na Aristariko Konga - Imechapwa 01 November 2009

Printer-friendly version

KWA miaka mingi watu wamekuwa wakitoa maelezo kadha wa kadhaa kuhusu kifimbo ambacho Mwalimu Julius Nyerere alibeba kila alipokwenda.

Kuna ambao wamesema siyo kifimbo cha kawaida na kuna wanaohusisha kifimbo hicho na zindiko.

Mjadala juu ya kifimbo ulipata nguvu baada ya Mwalimu Nyerere kuhutubia kwenye sherehe za Siku Kuu ya Wafanyakazi duniani mjini Mbeya, 21 Mei 1995.

Wakati wote akihutubia, Nyerere alikuwa akikigongagonga mezani, huku akisisitiza jambo au kuonyesha kukasirishwa na suala fulani.

Kuna ambao bado wanasema kifimbo cha Nyerere kilikuwa na nguvu fulani ya asili na ya kimila ambayo ilimfanya aheshimike na kuogopwa.

Mwandishi wa vitabu, W.E. Smith, katika kitabu chake kuhusu maisha ya Mwalimu Nyerere, ananukuliwa akizungumzia nguvu za jadi kwenye kabila lake la Wazanaki.

Katika kitabu hicho Smith ananukuu baadhi ya maoni ya Mwalimu kuhusu nguvu za jadi, hasa katika jamii za Kiafrika.

Anaeleza kuwa Mwalimu, Aprili 1966, aliulizwa kama angeweza kueleza katika lugha ya Kiingereza kuhusu manyoya ya mbuzi, ambayo yalichanganywa na nywele zake, ili kusababisha mbuzi waliyepewa na ndugu zake aswagwe kwa urahisi hadi nyumbani kwao.

Smith anamnukuu Mwalimu Nyerere akisema: “Nilipokuwa na umri wa kiasi cha miaka 10, siku mmoja baba (Chifu Nyerere Burito) alinituma nifuatane na mke wake wa kwanza, mmoja wa mama zangu wa kambo, kwenda katika kijiji kingine, umbali wa maili nane au 10 hivi, ambako mmoja wa jamaa zake huyo mama, alikuwa amefariki.

“Tulipokaribia kuondoka katika kijiji hicho, kurudi nyumbani, ndugu zake wakampa mbuzi. Lakini mbuzi yule alikataa kutii. Na wakati nilipokuwa nakurupushana naye, mmoja wa jamaa za mama yangu wa kambo akasema, ‘usiwe na wasiwasi. Nitakurahisishia kazi.’

“Basi, akang’oa nywele kidogo kutoka kichwani kwangu na manyoya kidogo kutoka katika kichwa cha yule mbuzi. Akazichanganya na mizizi fulani, akatafunia pamoja na halafu akampa mbuzi, akala.

“Akasema ‘sasa mbuzi atakufuata.’ Na kweli mbuzi akanifuata njia yote mpaka nyumbani. Ndiyo, alikuwa ameelekea kabisa. Alinifuata kama mbwa,” anasema Mwalimu katika kitabu cha Smith.

Smith anamnukuu Mwalimu akisema, “Mimi sidhani ni vigumu kama watu wanavyofikiri. Katika maisha ya kikabila, kijana anapofikia umri wa miaka 12 huwa karibu amehitimu. Ndiyo, unajua mambo mengi ya maisha katika umri wa miaka 12.

“Unayajua yote unayotakiwa uyajue, ambayo hujulikana hadharani. Lakini lazima unafichwa sana siri za wazee.”

Mwandishi anamnukuu Mwalimu enzi hizo akisema kuwa wakristo wanayakataa mawazo ya kikabila, huku wakiwa na sababu chache za kufanya hivyo, kwa sababu hata wenyewe wanaamini vitu ambavyo haviwezi kuelezeka.

“Ninalofahamu mimi ni kwamba yule mbuzi alinifuata. Na nikijitahidi sana kufikiri naweza tu kusema, sijui,”anaeleza Mwalimu.

Masimulizi kuhusu mbuzi ndiyo yamefanya wengi kuamini kuwa kifimbo cha Mwalimu kinaweza kuwa na nguvu za asili kama nguvu za kufanya mbuzi afuate mtoto kama mbwa, badala ya kuswagwa.

Aidha ile tabia yake ya kuwa nacho popote alipokwenda, iliongeza tetesi na kukuza mjidala. Je, kulikuwa na nguvu yoyote ya kijadi ndani yake?

Bali kuna taarifa kuwa Mwalimu hakuwa na kifimbo kimoja. Makumbusho yake yaliyopo Butiama, Musoma Vijijini, yanaonyesha kuwa vipo vifimbo vyake vingi na mkwaju aliotumia wakati wa kupigania uhuru.

Bado kitendawili hakijateguliwa na bado wanahistoria wana kazi kubwa ya kufanya utafiti wa kifimbo cha Nyerere.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: